Habari za Punde

DAFTARI LA WAPIGA KURA HADHARANI MWANYANYA

HEKA heka za uchaguzi mdogo wa ngazi ya Udiwani katika wadi ya Mwanyanya, Jimbo la Mtoni, zimepamba moto baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar kulianika hadharani daftari la wapiga kura.

Uchaguzi huo umekuja baada ya aliyekuwa Diwani wa wadi ya Mwanyanya Haji Hamadi Furaha, wa Chama cha CUF, kufariki dunia ikiwa imebakia siku moja ya kuapishwa kwake kushika nafasi hiyo katika Baraza la Madiwani Halmashauri ya wilaya Magharibi.

Kabla ya mauti hayo kumkuta Furaha, Tume ya Uchaguzi ilimkabidhi rasmi barua ya kumtangaza kuwa mshindi wa kiti cha udiwani katika Wadi hiyo Oktoba 30, 2010 na Novemba 10, mwaka huo alifariki dunia.

Kutokana na kifo hicho Tume ya Uchaguzi Zanzibar imelazimika kuandaa uchaguzi mdogo ndani ya kipindi cha mienzi minne ambapo uchaguzi huo ni wa kujaza nafasi hiyo.

Hapo awali katika wadi hiyo wakati wagombea hao wakijitayarisha na kuendelea na uchaguzi, Mwenyekiti wa Wadi hiyo alianguka ghafla na kupoteza maisha wakati akiwa katika kampeni kwenye Jimbo hilo.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Msimamizi wa Uchaguzi huo kwa Wilaya ya Mjini Suluhu Ali Rashid, alisema tayari maandalizi ya uchaguzi huo yamekamilika na jana waliweka dharani majina ya wapiga kura wa eneo hilo.

Alisema hatua ya kuanika majina hayo ni kuwawezesha wapiga kura kujitambua na kama kuna watu ambao wanawatilia shaka kuweza kuwawekea pingamizi.

Alisema hadi sasa wagombea waliojitokeza kutaka kiwania nafasi hiyo ni kutoka katika vyama vitatu ambapo ni CCM, CUF na CHADEMA.

Akitaja majina ya wagombea hao alisema CCM, ni Hamza Khamis Juma, Juma Ali Juma wa CUF na Salum Omar Salum wa CHADEMA.

Alisema kampeni za kujinadi kwa wagombea hao tayari zimeanza kufanyika na wanatarajia kuzikamilisha rasmi Aprili 16, mwaka huu, na uchaguzi utafanyika April 17, mwaka huu.

Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ulimalizika mwaka jana Oktoba 30, ambapo Chama cha CUF kilipata nafasi tatu za Udiwani wa Mjini huku CCM ikiwa na Madiwani zaidi ya 20.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.