Na Mwantanga Ame
MAKAMU wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi amewashukia Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na Wasimamizi wa Fedha serikalini na kuwataka kujitayarisha kuchukuliwa hatua za kisheria wale watakaoshindwa kufuata sheria ya usimamizi wa fedha za serikali.
Kauli hiyo aliitoa alipokuwa akifunga kikao cha Baraza la Wawakilishi kilichokuwa kikifanyika Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif, alisema serikali inakusudia kuchukua hatua hizo kwa watendaji hao kwa kuona wanafuata sheria namba 9, ya mwaka 2005 ya manunuzi na kuziondoa mali za umma pamoja na kanuni za fedha zilizopo.
Alisema anachukua hatua ya kutoa agizo baada ya kubainika kuwapo kwa uendelezaji wa vitendo vya ukiukwaji wa taratibu na udhibiti wa fedha na mali za serikali kwa baadhi ya taasisi za umma.
“Natoa agizo kwa Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na wale wote wanaosimamia fedha wawajibike ipasavyo kwa kusimamia kwa ukamilifu mapato na matumisi ya fedha za serikali”, alisema Balozi Seif.
Aidha, alisema ni wajibu kwa mamlaka zote zinazohusika na usimamizi wa mapato kuona kuwa wanapanua wigo utaosaidia uendeshaji mzuri wa serikali na kutoa huduma za maendeleo ya jamiii na uchimi katika nchi.
Balozi alisema serikali hivi sasa imekuwa ikikabiliana na matatizo mbali yakiwemo suala la kupanda kwa bei za vyakula jambo ambalo linahitaji kulifanyia kazi kutokana na kuwa limewaongezea ugumu wa maisha wananchi.
Alisema chanzo kikuu cha kuwapo kwa matatizo hayo ni kutokana kupanda kwa kiasi kikubwa bei za vyakula katika soko la kimataifa jambo ambalo limeweza kuleta athari kwa wananchi wa Zanzibar.
Makamu huyo aliwataka wafanyabiashara hapa nchini kuzingatia bei zao ili zisiwaathiri wananchi kwa kuona wanapanga bei zao kwa kuzingatia vipato vya wananchi.
Aidha, Balozi Seif akiendelea kutoa hotuba yake hiyo alisema serikali hivi sasa imo katika utekelezaji mpango wake wa uwezeshaji wa wananchi na ni vyema wakaona haja ya kushiriki katika mpango huo ili waweze kuachana na vitendo viovu vikiwemo vya utumiaji wa dawa za kulevya.
Balozi Iddi pia alitoa onyo kwa baadhi ya watu wanaoendelea na tabia ya uharibifu wa mazingira kwa kushiriki vitendo vya uchimbaji wa mchanga, kukata miti ovyo na utupaji wa taka jambo ambalo serikali haitalivulia.
Kuhusu mambo ya Muungano, Balozi Seif alisema kuwa serikali itahakikisha hoja zilizobaki ambazo bado hazijapatiwa ufumbuzi serikali inazipatia majibu huku ikikabiliana na changamoto zilizobakia.
Aidha alisema kuwa sherehe za Muungano kwa mwaka huu zitafanyika Zanzibar, kwenye kiwanja cha Amaan ambapo tayari matayarisho yake yameanza kukamilika.
Makamu huyo pia alisema kuwa hali ya usalama barabarani bado hairidhishi kutokana na kuongezeka kwa ajali huku baadhi ya watu kuvunja sheria jambo ambalo bado Jeshi la Polisi watahitajika kuchukua jitihada zaidi kukomesha vitendo hivyo ikiwa pamoja na wasiovaa kofia za ‘helmet’.
Makamu huyo alikiahirisha kikao hicho hadi Juni 15, mwaka huu. Ambapo serikali inatarajiwa kuanza kwa kikao chake cha bajeti kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
No comments:
Post a Comment