Habari za Punde

MASHIRIKIANO YATASAIDIA KUPATIKANA MAENDELEO

Na Halima Abdalla

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Tahir Abdalla amesema mashirikiano kati ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muhimu katika kuendeleza maendeleo ya nchi.

Alisema ili yapatikane maendeleo ya haraka Tanzania, ni vizuri watalamu wa serikali hizo mbili kushirikiana na kubadilishana mawazo ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Alieleza hayo alipokkuwa akifungua kikao cha mashirikiano kati ya wakurugenzi wa wizara ya Maji kutoka serikali ya Mapinduzi Zanzibar na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mamlaka ya Maji iliyopo Gulioni Mjini Zanzibar.

Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Rasilimali za Maji kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) Naomi Lupimo, alisema tatizo la uharibifu wa mazingira katika maeneo ya vyanzo vya maji limekithiri hata kwa upande waTanzania Bara.

Alisema wananchi wamekuwa wakivamia maeneo ya vyanzo vya maji na kupelekea uharibifu wa miundombinu ya maji na kusababisha kukosekana kwa huduma ya maji.

Alisema wanachokifanya Tanzania bara kwasasa ni kuwaondoa wananchi wanaovamia katika maeneo ambapo yana vyanzo vya maji.

Akizungumzia kuhusiana na uchangiaji wa huduma ya maji Tanzania Bara Mkurugenzi wa Maji vijijini kutoka Tanzania Bara John Mukumria, alisema wananchi wenyewe ndio wanaopanga bei kuhusiana na huduma ya uchangiaji wa maji kwa kushirikiana na serikali za mitaa.

Alisema ili huduma iwe endelevu wananchi na wakaazi wenyewe wa mji husika vijijini na mijini ndio wanajipanga kuchangia huduma hiyo pamoja na utoaji wa maji taka kwa kuwekeana bei rahisi ya kuchangia ili wananchi wasishindwe kuchangia huduma hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ufundi kutoka Zanzibar Muhammed Ilias, alisema Wizara ya Maji,Makaazi ,Maji na Nishati Zanzibar inafanyakazi kwa kushirikiana na wizara mbali mbali ikiwemo wizara ya Kilimo na Maliasili, wizara ya mifugo pamoja na utalii.

Alisema Zanzibar hakuna anae miliki maji isipokuwa maji ni rasilimali ya taifa ambapo hapo mwanzo hapo mwanzo ilikuwa ni Idara na malengo yao ya baadae ni kuhakikisha Zanzibar kunazalisha maji kwa Afrika Mashariki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.