Habari za Punde

BORA BAJETI NDOGO INAYOTEKELEZEKA

Na Abdulla Mohammed Juma

MASIKIO ya Wazanzibari keshokutwa yataelekezwa katika kufuatilia bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa mwaka wa fedha 2011/2012, ambayo itawasilishwa katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yusuf Mzee, ambayo kwao itakuwa  muhimu na maana kubwa.

Bajeti ya mwaka huu ni ya kihistoria kwa wananchi wa Zanzibar kutokana na kuwa ya kwanza  tokea kuundwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo katika mfumo wa umoja wa kitaifa, baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana.

Umuhimu wa bajeti hiyo pia unakuja kutokana na kuwa ya kwanza kwa Serikali mpya ya awamu ya saba Zanzibar, iliyo chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein,  ambae tokea aingie madarakani alianza kutekeleza ahadi zake kupitia bajeti ambayo ilipangwa na serikali ya awamu ya Sita mwaka wa fedha 2010/2011 unaomalizika Juni 30 mwaka huu.

Bila shaka Wazanzibari watakuwa wanasikiliza bajeti hiyo kuanza kupima uhalisia wa utekelezaji wa ahadi za serikali hiyo, ambayo imejengewa matumaini makubwa kutokana na kuwa katika muundo wa mchanganyiko baina ya chama kilichoshinda uchaguzi mkuu cha CCM na chama chenye wawakilishi katika Baraza kutokana na kushinda kwenye baadhi ya majimbo ambacho ni CUF.

Muendelezo wa utekelezaji wa ahadi nyingi za Dk.Shein katika kampeni za uchaguzi zitaonekana katika mipango ya matumizi itayotangazwa kwenye bajeti hiyo, japokuwa umuhimu na hadhari vinahitajika ili kuanza na vipaumbele kutokana na ukweli kwamba mapato yanayokusanywa nchini hayawezi kukidhi kutekeleza ahadi zote.

Kwa watayarishaji wa bajeti hii ambao bila shaka ni Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, wanapaswa kuwa makini na kupanga bajeti halisi ambayo inaweza kutekeleza mipango itayopangwa katika kipindi husika cha mwaka wa fedha 2011/2012.

Bajeti hiyo ni lazima iweke vipaumbele katika utekelezaji wa ahadi hizo za Mheshimiwa Rais na mambo mengine aliyoyaahidi bila shaka yatatekelezwa katika muda uliobakia, ikizingatiwa kuwa ataongoza kwa miaka mitano.

Wachumi wetu hawa ni lazima wawe makini, huku wakizingatia utashi wa kisiasa ambao ndiyo dira kwao, pia wanapaswa kuzingatia kuwa ili kuleta mafanikio hayo ya kisiasa kwa kutenga fedha ambazo zitafanikisha mipango yote itayopangwa, badala ya kuahidi mambo lukuki ambayo wanatambua fika kuwa fedha za kuyatekeleza hazipo na hazitopatikana katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/2011.

Badala ya kudhani kuwa kuahidi kutekeleza mipango mingi itakuwa tunampandisha chati mheshimiwa Rais, itakuwa tunakosea kwani tutampunguzia imani waliyonayo wananchi kwake kuwa kila alichoahidi anakitekeleza, kwani fedha ya kufanya hivyo hatokuwanayo.

Kwa vile wananchi wa Zanzibar ya leo wanauelewa zaidi wa mambo yanavyokwenda nchini na duniani kote, ni vyema bajeti ikawa wazi japo kueleza kuwa suala fulani litawekewa jiwe la msingi na ujenzi wake kumalizwa mwakani, kuliko kutangaza kuwa litasimama jingo hali ya kuwa fedha zinazotengwa ni za msingi.

Naamini wachumi wetu wanaelewa japo kwa makisio kiasi cha fedha kitachokusanywa nchini na kutolewa na wahisani katika mwaka huo wa fedha, basi wajiamini na kutumia vyema takwimu zao ili kutayarisha bajeti inayotekelezeka.

Haitokuwa busara na itakuwa kosa kubwa kiuchumi na kisiasa kwa SMZ kutangaza bajeti ambayo yenyewe inaelewa fika kwamba haitekelezi, lakini lengo likiwa ni kuwafurahisha wananchi ambao baadae watakuja kuibana serikali pale itaposhindwa kutekeleza iliyoahidi kwenye bajeti hiyo.

Itakuwa vizuri kama bajeti hiyo itabainisha wazi mbinu mpya za kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuziba mianya ya uvujaji mapato ambao unaikosesha fedha SMZ kwa muda mrefu sasa.

Tukielewa kwamba sekta ya utalii ndiyo mhimili wa uchumi wa Zanzibar hivi sasa, bila kuoneshwa mikakati itayotumika kudhibiti uvujaji wa mapato katika sekta hiyo, ambayo inaongoza kwa kuikosesha mapato Serikali, ikiwemo mengi kuchukuliwa na wawekezaji hasa wa nje kuliko faida ya nchi na wananchi wake.

Aidha bajeti hiyo iweke wazi hatua zitazochukuliwa na Serikali ili kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuepusha misamaha ya kodi inayoendeshwa bila mpango maalum.

Kwa vile maendeleo ya Zanzibar yanafuata Dira ya Maendeleo ya 2020 na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondosha Umasikini Zanzibar (MKUZA), lazima bajeti hiyo ibainishe wazi wazi namna malengo yaliyomo kwenye mipango hiyo yatavyotekelezwa na kuondokana na utashi wa kuhamia mipango mipya.

Bila shaka kwa wafanyakazi Serikalini, jambo muhimu kwao litakuwa ni kuona mishahara yao na stahili zao zinaongezeka, kutokana na ukweli kwamba viwango vya sasa havikidhi hali halisi ya gharama za maisha, jambo ambalo linawafanya kuwa masikini wa kudumu.

Mpango mzima wa kuwafanya wafanyakazi wenye utaalamu kubakia kuitumikia jamii ya wazanzibari ni lazima utekelezwe kupitia bajeti hii, vyenginevyo gharama iliyoingia serikali kuwasomesha wataalamu hawa itakuwa haina maana kwa nchi na wananchi wake.

Bajeti hii ni lazima ihitimishe hasara ya Serikali kusomesha wataalamu na baadae kuchukuliwa na taasisi nyengine za nje kwa kivutio kimoja tu cha maslahi, ambacho iwapo wachumi wetu wanaopanga bajeti watakuwa makini wanaweza kuwapatia wataalamu wetu hawa wazalendo.

Wafanyakazi wa Sekta binafsi nao wanasubiri kupitia bajeti ya mwaka huu kusikia waajiri wakibanwa na kuwajibishwa kulipa kima cha chini ambacho angalau kitalingana na kazi wanazofanyishwa wananchi kwa kutishwa kufukuzwa kazi iwapo watadai zaidi.

Mipango ya serikali kuwezesha wananchi nayo itakuwa ikisubiriwa kwa hamu na wananchi walio wengi, wakiwemo vijana, kinamama na walio katika makundi maalum, ambao hali zao za kimaisha haziendani na malengo ya MKUZA, wala Dira ya Maendeleo ya 2020.

Ni wajibu wa bajeti hii kuainisha namna utekelezaji wa mpango wa kuongeza ajira utavyofanyika, ili kupunguza tatizo la uzururaji kwa vijana, pamoja na kuwanusuru na makundi mabaya kama vile ya ngono, uvutaji bangi na matumizi ya dawa za kulevya.

Suala la udhibiti wa ongezeko la gharama za maisha kutokana na kupanda bei bidhaa ni lazima lielezwe njia zitazotumika kulitekeleza vyenginevyo juhudi za kuinua maisha ya wananchi wa Zanzibar hazitofanikiwa hata wakipewa mishahara mikubwa kiasi gani.

Kwa vile kilimo bado ni uti wa mgongo wa uchumi wa Zanzibar na Serikali imetangaza mpango wake wa kuleta mapinduzi ya kilimo, bila shaka bajeti ya sekta hiyo itatononeka na kubainishwa namna mapinduzi hayo yatavyofikiwa.

Uvuvi na mifugo ni sekta zinazotegemewa katika kuendesha maisha ya idadi kubwa ya wananchi wa Zanzibar, kwa vile serikali tayari imetangaza kuboresha sekta hizo, bila shaka bajeti itakuwa imeliona hilo na kutenga fungu lenye muelekeo wa kuelekea kuzifanya sekta hizo kuwa za faida wahusika.

Bajeti ya Zanzibar mwaka huu pia inalazimika kutenga fedha kuweza kuinua sekta za huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, utamaduni na michezo, ambazo ni muhimu kujenga ustawi wa jamii.

Kutokana na kuongezeka idadi ya watu Unguja na Pemba, ongezeko la huduma za jamii haliwezi kuepukwa hivyo fungu kubwa la fedha za bajeti hii halinabudi kuelekezwa kuimarisha elimu na afya ya jamii.

Wananchi wanatarajia fedha zaidi kutengwa kuimarisha hospitali zetu na vituo vya afya, huku ujenzi wa skuli na ununuzi wa vifaa vya kusomeshea ukipewa umuhimu wake.

Kwa vile dunia ya sasa inategemea zaidi teknolojia ya mawasiliano TEKNOHAMA, bila shaka bajeti ya Zanzibar mwaka huu itatenga fedha nyingi kuhakikisha suala hili linatekelezwa badala ya kuzungumzwa midomoni tu kila siku.

Sambamba na hilo, vyombo vya habari vya Serikali navyo, ikiwemo, gazeti la Zanzibar Leo, TVZ na STZ vinatarajiwa zaidi kuwajuvya wananchi utendaji wa serikali yao, pamoja na wao kuiambia serikali kupitia vyombo hivyo, ambavyo kwa bahati mbaya viko hoi taabani.

Mafanikio ya utekelezaji wa bajeti hiyo itayotangazwa keshokutwa yatategemea zaidi uimara wa vyombo hivyo vya habari, hivyo bajeti ni lazima ivitengee fungu la fedha kuviwezesha kuwa vyombo vya habari, badala ya bajeti ya sasa ya kulipa mishahara pekee.

Katika mfumo huu mpya wa Serikali ya Mainduzi ya Zanzibar wa umoja wa kitaifa ni matarajio ya wananchi wengi kwamba, Wajumbe wa Baraza la wawakilishi nao watakuwa wanachangia kwa maslahi zaidi ya wananchi na nchi, kuliko kuendekeza maslahi ya kisiasa na uvyama kama ilivyokuwa huko nyuma.

Matumaini ya wananchi wa Zanzibar yamewekezwa zaidi kwenye bajeti hii, hivyo serikali na Wawakilishi wanapaswa kulingatia hilo katika mchakato huu wa bajeti.

Bora bajeti iwe ndogo inayotekelezeka, kuliko kubwa isiyotekelezeka bali ya kufurahisha wananchi.

0777471199
abdulladulla@hotmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.