Habari za Punde

DK SHEIN ATAKA WATUMISHI WA UMMA WAJITUME

Asisitiza wapewe haki, uadilifu kazini

Na Rajab Mkasaba, Dar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amezitaka taasisi zinazohusika na maslahi ya watumishi wa umma kutilia mkazo haki za watumishi ikiwa ni pamoja mafunzo ya watumishi, maslahi bora, kuwathamini na kuwawekea mazingira bora ya kufanya kazi.


Dk. Shein alieleza hayo jana katika viwanja vya Mnazimmoja mjini Dar-es-Salaam, alipokuwa akifunga mkutano wa kimataifa wa Utumishi wa Umma, ambapo alisema mambo haya ni muhimu kwani huwashajiisha watumishi wa umma kujituma na kuongeza ufanisi katika sehemu za kazi.

Alisema watumishi wa umma wote waelewe umuhimu wao katika jamii wanayoishi kwa lengo la kuleta maendeleo kwani, bila ya mchango wao ni vigumu kupata maendeleo endelevu, huku pia akisisitiza suala la uadilifu, ubunifu, kuimarisha ushirikiano na wawe ni wenye kwenda na wakati.

Akizungumzia Utumishi katika ngazi ya Kimataifa, alizitaka Jumuiya za Kimataifa kusimama kidete katika kutetea maslahi ya Watumishi wa Umma na kubainisha umuhimu wa kuzingatia haki za watumishi bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa lengo kuimarisha utumishi wa Umma katika ngazi  zote ni kuwapatia watumishi uwezo wa kuwahudumia vyema watu wa ngazi za chini wakiwemo walemavu, watoto, wanawake na wale wote wanaoishi katika mazingira magumu.

Alisema Zanzibar nayo haijaachwa nyuma katika suala zima la kuimarisha  utumishi wa Umma  ambapo alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa imeanzisha Wizara Maalum ambayo inashughulikia Utumishi wa Umma.

Alisema kuwa serikali pia, imeweka kipaumbele katika kuwapatia wafanyakazi haki zao, mafunzo, maslahi na mazingira bora ya watumishi.

Dk. Shein alisema kuwa maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma yatumiwe kutathmini fursa na changamoto zilizopo katika utumishi wa Umma ili kuimarisha hali ya wananchi wanaotumikiwa.

Alieleza kuwa Utumishi wa Umma ni wito wa kujikubalisha kuwatumikia watu kwa hivyo ni muhimu kwa kila mtumishi wa Umma kutoa huduma kwa kadri iwezekanavyo kulingana na nafasi yake.

Aidha, Dk. Shein aliwakumbusha Watumishi waelewe kuwa nafasi na mishahara yao inatokana na watu wanaowatumikia iwe ni kutokana na kuwapigia kura au ni kutokana na kodi wanazozilipa.

“Ni dhahiri kuwa wananchi wana mategemeo makubwa sana kutoka kwa watumishi, kwa hivyo ni lazima watumishi wajitahidi kukidhi matarajio hayo kwa kuimarisha zaidi huduma zao”, alisema. 

Aidha, Dk. Shein alitoa shukurani kwa Jumuiya ya Kimataifa kwa kuipa heshima  Tanzania kuwa Mwenyeji wa Maadhimsho ya Utumishi wa Umma ambapo zaidi ya wajumbe kutoka nchi 80 walihudhuria maadhimisho hayo.

Hii ni mara ya kwanza kwa maadhimisho haya kufanyika Tanzania ambapo pia, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wajumbe walioshiriki mkutano huo kuitembelea Zanzibar.

Pamoja na mambo mengine, Dk. Shein aliwapongeza watu wote waliozawadiwa  kwa utumishi bora, aliwaasa watumishi hao kuendelea kuwa watumishi wazuri na kuwa mfano kwa wengine na kuwataka watumishi wengine kuiga mifano ya wazawadiwa hao. 

Katika hafla ya ufungaji viongozi mbali mbali walihudhuria wakiwemo wa Kitaifa na Kimataifa, viongozi waandamizi kutoka Umoja wa Mataifa, Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimeti ya Utumishi wa Umma wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hawa Ghasia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Umma na Utawala Bora wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Haji Omar Kheir na viongozi mbali mbali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.