Habari za Punde

NI BAJETI YA KIMAENDELEO

·        Kuzingatia MKUZA 2, Dira ya 2020, MDGs·        Mishahara yasubiri Wizara ya Utumishi
·        Kodi kutopandishwa, kasi kuongeza mapato
·        Kilimo, Afya, Maji, Elimu, Miundombinu kuinuliwa

Na Mwandishi wetu

WAZIRI wa Nchi ofisi ya Rais Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo, amesema utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 italenga zaidi katika kutekeleza mikakati na miradi ya kimaendeleo iliyopo.

Waziri huyo alieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi uliopo Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar alipokuwa akiwasilisha bajeti mpya ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka mpya ujao wa fedha.

Alisema bajeti hiyo itaegemea kwenye utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA) awamu ya pili, kufanikisha malengo ya mipango ya milenia pamoja,  ilani ya Chama cha Mapinduzi na kuifikia dira ya maendeleo ya mwaka 2020.

Waziri huyo alisema ili kufikia malengo ya mipango hiyo mapema zaidi,  wananchi wanapaswa kuwajibika na kushiriki kikamilifu kwa kutumia fursa zinazojitokeza kwa kuzalisha mali na kujiongezea kipato.

Mzee alisema sekta za kilimo, mifugo na viwanda zikiboreshwa na kutiliwa mkazo, usindikaji wa mazao ya kilimo una nafasi kubwa ya kuchangia pato la taifa na kukuza ajira huku akieleza kuwa bajeti hiyo inalenga kuongeza jitihada za serikali za kuimarisha matumizi bora ya ardhi, miundombinu na mawasiliano.

“Napenda kuchukua fursa hii kumalizia kwa kusisitiza kuwa bajeti hii inalenga zaidi katika kuimarisha na kuleta maendeleo ya kiuchumi pamoja na maslahi ya wafanyakazi na wananchi kwa jumla. Tumeeleza changamoto zinazotukabili katika vyanzo vyetu vya ukuaji wa uchumi na ukusanyaji wa mapato. Hatuna budi kuwa na mikakati maaalum ya kukabiliana na changamoto hizo. Dhamira ya Serikali ni kujenga uwezo kwa watoto, vijana na wafanyakazi hatimae waweze kujenga uchumi wenye kuendana na ushindani katika dunia”,alisema waziri huyo.

Vipaumbele vyengine katika bajeti hiyo ni pamoja na kuimarisha  huduma za afya, msisitizo zaidi ukilenga katika ununuzi wa vifaa vya hospitali, dawa muhimu, kuiimarisha ubora wa elimu kwa kupunguza tatizo la uhaba wa madawati vifaa vya maabara, vifaa vya kufundishia na kumaliza ujenzi wa madarasa yaliyoanzishwa na wananchi katika maeneo yao.

Aidha huduma ya maji safi na salama, kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuendeleza shughuli za  umwagiliaji, mbegu bora, mbolea na matumizi ya matrekta pamoja na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuendeleza miradi ya barabara na umeme katika maeneo ya kilimo.

Alisema serikali katika bajeti hiyo haikusudii kupandisha kodi ila imekusudia kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato kwa vianzio vilivyopo na kuziba mianya inayotumika katika kuepuka, kupunguza au kukwepa kulipa kodi pamoja na kuendelea kufuatilia matumizi mabaya ya misamaha ya kodi nchini.

“Kabla ya kuongeza kodi, juhudi zinachukuliwa kwanza katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji na uwajibikaji wa ulipaji kwenye vianzio vilivyopo na kuhakikisha kuwa misamaha inayotolewa inatumika kwa dhamira iliyokusudiwa”, alisema.

Katika juhudi nyengine za kuongeza na kuimarisha mapato, Serikali katika mwaka ujao itaanza kupokea marejesho ya kodi ya mapato ya mtu binafsi kwa wafanyakazi wa taasisi za Muungano wanaofanyakazi Zanzibar, hatua hiyo imekuja kufuatia makubaliano yaliofikiwa kati ya SMZ na SMT katika juhudi za kushughulikia Kero za Muungano.

Katika suala la kuimarisha na kuibua vyanzo vipya vya mapato, serikali inaendelea na juhudi za maandalizi ya uchimbaji wa mafuta na gesi kwa upande wa Zanzibar kufuatia maamuzi yaliyotolewa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na hatimae kupitishwa na Baraza hilo juu ya kuliondoa suala la mafuta na gesi asilia katika orodha ya mambo ya Muungano.

Alisema uchumi endelevu unahitaji zaidi utulivu wa bei za bidhaa na huduma ambapo kasi ya mfumko wa bei kwa mwaka 2010 ilionekana kushuka na kufikia asilimia 6.1 ikilinganishwa na asilimia 8.9 mwaka 2009 huku  mwaka 2010, kasi ya mfumko wa bei kwa bidhaa za chakula ilishuka hadi asilimia 6.2 kutoka asilimia 9.6 mwaka 2009, wakati bidhaa zisizo za chakula, kasi yake ya mfumko wa bei ilipanda kidogo hadi asilimia 6.2 mwaka 2010 kutoka asilimia 6.1 mwaka 2009.

Kwa wastani, pato la mtu binafsi kwa mwaka 2010 liliongezeka kwa asilimia 7.6 kutoka shilingi 728,000 mwaka 2009 hadi kufikia shilingi 783,370 mwaka 2010 ikiwa ni sawa na dola za Kimarekani 561 kwa mwaka 2010 kutoka  Dola za Kimarekani 558 kwa mwaka 2009.

Ni dhahiri kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi maskini ambayo wastani wa kipato cha mtu binafsi kiko chini ya Dola za Kimarekani 950. Azma ya Dira ya Maendeleo ya 2020 ni kufikia katika kundi la nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2020.

Kwa upande wa usafirishaji wa bidhaa, thamani ya usafirishaji wa zao la karafuu, ilipungua kwa asilimia 29.1 kutoka Dola za Kimarekani 10.3 milioni kwa mwaka ulioishia Machi 2010 hadi kufikia Dola za Kimarekani 7.3 milioni mwaka ulioishia Machi 2011.

Kiwango cha usafirishaji wa zao la karafuu kilishuka kutoka tani 2,900 mwaka ulioishia Machi 2010 hadi kufikia tani 2,000 kwa mwaka ulioishia Machi 2011, wakati  bei ya karafuu iliongezeka kutoka Dola za Kimarekani 3,559.8 kwa tani  na kufikia Dola za Kimarekani 3,591.4 kwa tani kwa kipindi hicho hicho.

Hata hivyo, takwimu za usafirishaji wa zao hili pia zinaathiriwa sana na magendo na kueleza kuwa serikali katika mwaka wa fedha 2011/2012 imeandaa mipango madhubuti ya kupandisha mikarafuu mipya pamoja na kuwatafutia wakulima soko la uhakika ambalo litapelekea kuwapatia wakulima bei nzuri itakayokuwa na tija.

Katika kukabiliana na tatizo la ajira, alisema serikali imeweka mikakati maalum na utaratibu wa upatikanaji wa taarifa za nafasi za ajira huku kukiwa kumeshakamilika ujenzi wa kituo cha kutoa taarifa za nafasi za ajira kwa wanaoomba kazi na taarifa za biashara na masoko kwa wajasiriamali.

Alisema serikali iliahidi kuimarisha maslahi ya wafanyakazi kwa nia ya kuwapunguzia makali ya maisha pamoja na kuhakikisha kuwa wataalamu wanaofundishwa kwa gharama kubwa wanabakia nchini ambapo mishahara ya watumishi wa Umma, imefanyiwa mapitio na kuandaa mapendekezo mapya  ya mishahara ambayo itaanza kutumika mwaka wa fedha 2011/2012.

Alisema viwango vipya na taratibu zake zitatolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambapo mapendekezo hayo ya mishahara mipya yamezingatia vigezo mbali mbali ikiwa ni pamoja na elimu aliyonayo mtumishi, uzoefu na muda aliofanyia kazi.  Miundo ya Utumishi (scheme) imewapanga watumishi na nyongeza zao za mishahara kwa kuzingatia muda wa uajiri na kiwango cha elimu.

Akizungumzia sekta ya utalii alisema sekta hiyo ni muhimu na ina mchango mkubwa katika pato la taifa, ambapo inahusisha uingiaji wa wageni kutoka sehemu mbali mbali za dunia huku ukuaji wake unaangaliwa zaidi kutokana na shughuli za hoteli na mikahawa.

Alisema sekta ya utalii mwaka 2010 uingiaji wa wageni umeshuka kutoka watalii 134,954 mwaka 2009 hadi watalii 132,836 mwaka 2010 na hivyo, kusababisha kasi ya ukuaji wa shughuli za hoteli na mikahawa kupungua kutoka asilimia 5 mwaka 2009 hadi asilimia 3 mwaka 2010.

Akizungumzia sekta ya nishati, serikali ya Marekani inaendelea na utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa njia ya pili ya umeme kutoka Ras Kiromoni hadi Fumba ambao unatarajia kuongeza kiwango cha umeme kufikia Megawati 100 huku Kampuni ya Viscas Corporation ya Japan inaendelea na utengenezaji wa waya wa kulaza baharini.

Alisema kukamilika kwa mradi huu kutasaidia kuwa na umeme wa uhakika na serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi ina mpango wa kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia upepo na jua.  Juhudi za kuzalisha umeme kwa kutumia upepo ziko mbioni na tayari maeneo kama Makunduchi, Matemwe na Nungwi yameonesha kuwa na upepo ambao una uwezo wa kuzalisha umeme. 


Yusuf amesema katika kipindi cha miezi tisa ya awali ya mwaka wa fedha 2010/11, mapato yaliokusanywa yalifikia TZS 132.96 bilioni sawa na asilimia 100.9 ya makadirio ya kipindi hicho. Ikilinganishwa na mwaka uliopita (2009/2010) katika kipindi kama hicho, kunajitokeza ukuaji wa mapato kwa asilimia 16.7. Kati ya makusanyo hayo jumla ya TZS 126.10 bilioni zilitokana na mapato ya kodi ambazo ni sawa na asilimia 89.1 ya makadirio (sawa na ukuaji wa asilimia 16.8 kulinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2009/2010). Mapato yasiyokuwa ya kodi yalifikia TZS 6.86 bilioni sawa na asilimia 87 ya makusanyo ya kipindi hicho.

Kwa upande wa ukusanyaji wa mapato kitaasisi, katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka 2010/11, Mamlaka ya Mapato Tanzania imekusanya jumla ya TZS 55.73 bilioni sawa na asilimia 108 ya makadirio ya kipindi hicho. Ukuaji huo ni asilimia 27.2 ikilinganishwa na makusanyo ya kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita. Bodi ya Mapato ya Zanzibar kwa kipindi cha Julai – Machi 2010/2011 nayo  imekusanya jumla ya TZS  77.23  bilioni sawa na asilimia  96.3 ya makadirio ya miezi tisa, sawa na ukuaji wa asilimia 10.14 kwa  mwaka uliopita katika kipindi kama hicho.

Mapato yasiyokuwa ya kodi kutoka katika Wizara za Serikali yameendelea kuwa madogo, Yusuf jumla ya TZS 6.88 bilioni zilikusanywa ambazo ni sawa na asilimia 87 ya makadirio ya miezi tisa  ya awali.  Hali hii imetokana zaidi na viwango vya kutozea ada kuwa vidogo pamoja na baadhi ya sheria zetu kutoa mwanya kwa Waziri wa sekta kusamehe kodi.  Serikali katika juhudi zake za kuongeza mapato hasa yale ya mawizara yakiwemo ya ardhí inaandaa utaratibu wa kurekebisha kasoro hizo.

Kwa upande wa matumizi ya Serikali alisema ni dhahiri yatakuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka. Katika kipindi cha tathmini (Julai 2010 hadi Machi 2011), matumizi halisi ya Serikali yalifikia TZS 256.48 bilioni sawa na  asilimia 76.9 ya makadirio ya kipindi hicho. Matumizi kwa ajili ya kazi za kawaida yalifikia TZS 138.76 bilioni sawa na asilimia 95.7 ya makadirio, wakati yale ya kazi za maendeleo yalifikia TZS 142.23 bilioni sawa na asilimia 75.5 ya makadirio ya kipindi hicho. Kati ya matumizi hayo ya kazi za maendeleo, TZS 24.51 bilioni zilikuwa ni fedha za ndani na TZS 117.72 bilioni ni fedha za kigeni kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.

Serikali  imependekeza mbele ya Baraza hilo kwa mwaka wa fedha 2011/2012 kukusanya shilingi Mia Sita na Kumi na Tatu bilioni, na Sabiini na Sita milioni (TZS 613,076 millioni) pamoja na matumizi ya shilingi bilioni Mia Mbili na Thelathini na Nne, milioni Mia Moja na Sabiini na Tano (234.175 bilioni) kwa kazi za kawaida na shilingi bilioni Mia Tatu Sabiini na Nane, milioni Mia Tisa na Moja (378.901 bilioni) kwa kazi za maendeleo.
Baraza hilo limeakhirishwa hadi Jumatatu ambapo Wajumbe watajadili na kuichangia bajeti hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.