Na Mwajuma Juma
KANISA la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar leo linaadhimisha miaka 138 tangu kukomeshwa kwa biashara ya Utumwa Afrika Mashariki na kati na kuwataka watanzania kuienzi historia ya siku hiyo.
Hayo yameelezwa na Msaidizi Katibu wa Kanisa hilo James Kaleza alipozungumza na waandishi wa habari ukumbi wa Kanisa hilo Mkunazini Mjini Zanzibar.
Alisema biashara ya utumwa ilikomeshwa Juni 6 mwaka 1873, ikiwemo kufungwa soko la watumwa lililokuwa katika eneo la Mkunazini mjini Zanzibar, baada ya kusainiwa mkataba kati ya Serikali ya Sultani na Muingereza.
Alisema biashara ya Utumwa ilisitishwa Zanzibar baada ya mvumbuzi Dk. David Livingstone kutoa hutuba kali nchini Uengereza ambayo iliwavutia wanafunzi wa vyuo vikuu vya Oxford na Cambridge
kuhusu madhila ya biashara ya utumwa yaliyokuwa yakifanyika Afrika
Mashariki.
“Leo hatuna tena biashara ya utumwa hapa Zanzibar wala Afrika soko lile halipo tena yapo mabaki ya Historia ambayo yamefichwa:, alisema Katibu Msaidizi huyo na kushauri siku hiyo iwe naadhimishwa kitaifa kulinda historia.
Alisema uhuru wa kwanza wa Muafrika ulipatikana Juni 6 mwaka 1873 baada ya kukomeshwa kwa biashara ya utumwa na kusisitiza umuhimu wa vizazi vipya kutembelea maeneo ya historia ikiwemo mapango yaliyokuwa yakihifadhiwa watumwa kabla ya kuuzwa katika soko la Ulaya.
Alisema biashara ya Utumwa ilianza kufanyika Zanzibar baada ya kuingia wareno na baadae iliendelea baada ya waarabu kushinda vita hadi ilipokomeshwa na Wamisionari walioingia Afrika Mashariki kupiga vita biashara hiyo.
Nae muongoza watalii katika eneo la Kumbukumbu la biashara ya watumwa Christopher Faraji alisema, historia ya biashara hiyo inatisha ndio maana wageni wengi wamekuwa wakimwagika machozi wanapohadithiwa madhila waliyokuwa wakiyapata watumwa.
Alisema mapango waliyokuwa wakihifadhiwa watumwa kabla ya kupelekwa sokoni yalikuwa yakipitisha hewa ndogo na huduma muhimu kama za vyoo na vyakula hazikupatikana, na waliwekwa katika msongamano mkubwa kwa
chumba kimoja watu 50.
“Mtumwa aliyechapwa viboko akawa halii, ndio aliyekuwa akipata bei lakini aliekuwa akilia aliendelea kubaki katika mapango na hicho ndio ilikuwa kipimo cha mtumwa bora”, alisema.
Karibu wageni 200,000 hutembelea kila mwaka kumbukumbu ya soko la Watumwa
No comments:
Post a Comment