Kuharakisha maendeleo ya elimu, viwanda na ICT
Hassan Hamad na Khamis Haji (OKMR), Bangalore, India
WAZIRI Kiongozi wa serikali ya Kanarnataka nchini India, D.V Sadananda Gowda, amesema serikali yake iko tayari kutiliana saini na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar juu ya makubaliano ya mashirikiano katika nyanja za elimu, viwanda na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (IT).
Sadananda amemueleza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad anayeongoza ujumbe wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar unaotembelea India huko Bangalore kuwa Karnataka imepiga hatua kubwa katika maeneo hayo na Zanzibar inaweza kunufaika chini ya makubaliano maalum.
Aidha, aliwataka wataalamu wa sekta hizo tatu wafanye mazungumzo na ujumbe wa Zanzibar ili wajue mahitaji halisi ya Zanzibar, ambapo ujumbe huo wa Zanzibar katika mazungumzo na watalaamu hao umeahidi kutumia fursa ya makubaliano hayo kupeleka watendaji wake na kujifunza mafanikio hayo katika mji mkuu wa Kanarnataka huko Bangalore.
Mapema, Maalim Seif akizungumza na Waziri Kiongozi huyo alisema malengo ya Zanzibar ni kuwa kituo maarufu cha teknolojia ya habari na mawasiliano katika eneo la Afrika Mashariuki na Kati, sekta ambayo hivi sasa imekuwa kichocheo kikubwa cha ajira na mafanikio katika sekta zote za maendeleo na uchumi.
Alisema mbali na Zanzibar kunufaika na utaalamu wa fani hizo kutoka Bangalore, lakini pia kuna fursa nyingi za uwekezaji kwa wafanyabiashara wa India katika visiwa vya Unguja na Pemba na wataweza kuichukua fursa ya kufunguliwa milango hiyo ya mashirikiano kufungua vitega uchumi.
Maalim Seif alieleza kwamba malengo ya Zanzibar kufanya ziara ya kujifunza katika miji ya India ni kupata utalaamu ambao baadaye utapelekwa kwa wananchi wakiwemo wakulima, wavuvi, wafugaji na wafanyabiashara wadogo, kwa nia ya kuwawezesha kufanya shughuli zao kitaalamu na kwa mafanikio makubwa zaidi.
“Malengo ya serikali ya Zanzibar ni kupata ujuzi na uzoefu wa shughuli za kiuchumi, elimu na maendeleo kwa ujumla na baadaye ujuzi huu utapelekwa kwa wananchi moja kwa moja wakiwemo wazalishaji na vijana wanaomaliza mafunzo katika vyuo mbali mbali kwania ya kuinua maisha yao”, alisema Maalim Seif.
Nae Waziri wa Elimu ya msingi na sekondari wa serikali ya Kanartaka, Vishweshwar Hedge Kageri amesema kuna fursa kwa Zanzibar kutumia ushirikiano uliopo kupeleka wanafunzi kujifunza elimu ya teknolojia ya habari kwa sababu Jimbo hilo limepata sifa kubwa duniani kote katika nyanja hiyo pamoja na elimu kwa ujumla.
Alisema baadhi ya miji ikiwemo ya Marekani imeamua kufanya tafiti mbali mbali katika ya sayansi na teknolojia ya habari na Mawasiliano (IT&C) katika mji wa Bangalore kutokana na sifa uliyojipatia Kimataifa na kasi ya ukuaji wa tekbolojia hiyo siku hadi siku.
Akizungumzia biashara, Katibu Msaidizi wa Shirikisho la wafanyabiashara wadogo na wakati wa Karnataka, Dorothy Salkdanha amesema wanapendelea kutoa mafunzo kwa wazalishaji wanawake wa Zanzibar na kuomba kupewa maelezo ya kina juu ya harakati za wazalishaji hao wa Zanzibar.
Alieleza kwamba wanawake wa India wanaonesha ushindani mkubwa katika kazi za biashara na wanaweza kutoa ujuzi wao kwa wanawake wa Zanzibar na kuwawezesha kukuza biashara zao kwa faida yao na nchi yao.
No comments:
Post a Comment