Habari za Punde

NDUNGAI: DAINI HAKI KWA KUTEKELEZA WAJIBU

Na Ramadhan Makame

NAIBU Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema watumishi wengi wa umma wamekuwa wakilia na kudai haki bila ya kujiangalia namna wanavyowajibika katika kutekeleza majukumu yao.

Ndugai alieleza hayo katika ukumbi wa ofisi ndogo za Bunge Tunguu wilaya ya Kati Unguja, alipokuwa akifungua mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Bunge.


Naibu huyo alisema kudai haki ni sawa, lakini msingi wake lazima uambatane na namna unavyowajibika katika kufanikisha majukumu ya kazi ulizopangiwa.

Aliwaeleza wafanyakazi hao wa Bunge kuwa wakati umefika wa kuwajibika kisawa sawa kwa kutekeleza majukumu yao kama inavyotakiwa hali itakayoondosha pingamizi pale watakapodai haki.

Alisema hivi sasa yapo malalamiko yanayotolewa na baadhi ya wabunge wakidai kutorishishwa na kazi za baadhi ya watumishi wa mhimili huo wa dola, na kuwataka wabadilike.

“Mnakumbuka kule Zambia wakati wa Rais Mwanawasa, wafanyakazi wote wa bunge la nchi hiyo waliachishwa kazi na kutangazwa upya kazi zao, waliokuwa wanawajibika walirejeshwa na wale wazembe walipoteza ajira”, alisema Ndugai.

Alisema ili bunge la Tanzania lisifikie huko ni wakati wa wafanyakazi wa bunge kujibadilisha na kuwa makini wakati wa kutekeleza majukumu yao kama inavyotakiwa.

Naibu huyo aliwapongeza wafanyakazi hao hasa kwa kuweza kukamilisha kumalizika kwa mkutano wa bunge la bajeti ambao ulikaribia kufikia miezi mitatu.

Alisema Tume ya Utumishi na Maslahi ya Bunge itaendelea kuangalia maslahi ya wafanyakazi wa bunge ili kipato chao kiendane na hali halisi ya maisha pamoja na hadhi ya chombo hicho wanachokifanyiakazi.
Naye Katibu wa chama cha wafanyakazi wa serikali kuu na afya (TUGHE), Ali Kiwenge alisema, uongozi bora unazoingatia ushirikishwaji ndio msingi imara utakaoleta mabadiliko kwenye sehemu za kazi.

Katibu huyo aliiomba Tume ya Utumishi ya Bunge iwe na mfumo unaolingana na hadhi ya utumishi katika chombo hicho pamoja na kungalia namna ya kuboreshewa maslahi yao wafanyakazi.

“Tusicheze na kazi tucheze na mishara, kwa sababu kazi ikikutoka hauipati tena lakini mshahara ukimalizika mwisho wa mwezi utapata mwengine”,alisema katibu huyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.