Habari za Punde

TAARIFA RASMI YA RAIS KUHUSU TUKIO LA AJALI YA MELI

TAARIFA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN,
KUHUSU TUKIO LA AJALI YA KUZAMA KWA MELI YA SPICE ISLANDER
TAREHE 10 SEPTEMBA 2011.

Bismillah Rahman Rahim

Ndugu Wananchi,

Assalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh

Alfajiri ya leo tarehe 10 Septemba kwa masikitiko na huzuni tumepokea taarifa ya kuzama kwa meli ya abiria na mizigo ya “Spice Islander” iliyokuwa ikisafiri kutoka Unguja kwenda Pemba. Ni dhahiri kuwa huu ni msiba mkubwa sana kwa Zanzibar na Taifa kwa jumla. Taarifa imebainisha kuwa katika tukio hili kuna watu wengi wameokolewa, wapo waliofariki na wengine hawajulikani walipo.

Baada ya kupata taarifa hii, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilichukuwa hatua za haraka za kulishughulikia tukio hili. Viongozi wa Kitaifa na wengineo wamekuwa katika harakati za kushughulikia jambo hili tangu alfajiri ya leo milango ya saa 9.00 alfajiri. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuvitumia vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyopo katika harakati za uokozi na kuwahudumia walioathirika na janga hili. Aidha, Serikali ilishirikiana na vyombo vya usafiri vya watu binafsi na taasisi mbali mbali za huduma.


Ndugu Wananchi,
Ni dhahiri kuwa katika tukio kama hili watu hupatwa na fadhaa na mshtuko lakini tukiwa waumini hatuna budi kuamini kuwa huu ni mtihani wa Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala. Ni wajibu wetu tuupokee mtihani huu na tushukuru. Mwenyezi Mungu anatutaka tuwe na subira katika kukabiliana na mitihani kama hii. Dini yetu inatufunza kuwa hapa duniani Mola atatupa mitihani mbali mbali ili kutupima imani zetu na bila shaka huu ni mmoja wapo. Mwenyezi Mungu anawapenda wenye kushikamana na imani na subira.

Ndugu Wananchi,
Natoa wito kwa wananchi wote tuwe wastahamilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba na maafa. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inashughulika kikamilifu ikiwa ni pamoja na kusaidia kuwatambua waliofariki, kuwasaidia waliookolewa na waliopata maumivu katika janga hili. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itashughulikia maziko kwa wale wote waliofariki. Kwa wale watakaotambuliwa, jamaa zao wataruhusiwa kuwachukua maiti hao kwa ajili ya mazishi na kwa wale waliokuwa hawakutambuliwa kwa vile wamefariki kwa maji ya chumvi wote watazikwa hapa Unguja katika eneo moja huko Kama lakini kila mmoja atazikwa katika kaburi lake. Mipango ya mazishi itatangazwa rasmi na Kamati ya Maafa ya Zanzibar kwa kushirikiana na Kamati ya Zanzibar ya Mazishi .

Kutokana na tukio hilo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatangaza siku tatu za maombolezo kuanzia kesho tarehe 11 Septemba, 2011. Aidha, katika kipindi hicho sherehe na tafrija zote hazina budi kusitishwa. Kadhalika bendera zitapepea nusu mlingoti.

Serikali itaandaa hitma maalum ya marehemu wote ambayo pia itahudhuriwa na baadhi ya viongozi wakuu. Aidha, Rais na viongozi wetu watapangiwa ratiba ya kwenda kwenye maeneo mbali mbali Unguja na Pemba kwa kuwapa pole wafiwa. Vile vile majina ya waliohai yatatangazwa kwa utaratibu maalum utatangazwa na Kamati ya Maafa. Ni vyema wananchi wakafuatilia habari sahihi za tukio hili kupitia vyombo vya habari ili kuepuka kupata taarifa zisizoaminika. Juhudi za uokozi zinaendelea na wananchi mtaendelea kuarifiwa ipasavyo.

Ndugu Wananchi,
Watu waliookolewa wakiwa hai ni 597 ambao wamepelekwa Hospitali ya Kivunge na wengine Hospitali ya Mnazi Mmoja. Baadhi yao wameruhusiwa kurudi majumbani mwao. Serikali itawahudumia waliokuwa hospitali kwa shida zao zote hususan chakula na mahitaji mengine ya msingi. Jumla ya watu 106 wamefariki dunia.

Kwa niaba ya Serikali, nachukuwa nafasi hii kutoa mkono wa pole kwa watu wote walioguswa na msiba wetu huu mzito. Pamoja na hayo natoa rambi rambi kwa wafiwa wote. Pia, nawatakia rehma na maghfira waliotangulia mbele ya haki na walionusurika nawaombea shufaa wapone haraka na Mwenyezi Mungu awasahaulishe kumbukumbu zote mbaya za tukio hili ili wapate kuendelea na maisha yao katika hali ya kawaida.

Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa hii kukushukuruni wananchi nyote kwa ushirikiano na utulivu mliouonesha na nawanasihi muendelee na hali hii katika kipindi hii chote. Wakati huo huo nazipongeza na kuzishukuru taasisi zote za ulinzi na usalama za Zanzibar na za Serikali ya Muungano wa Tanzania kwa namna zilivyoshiriki katika tukio hili. Aidha, nazishukuru taasisi za huduma mbali mbali wakiwemo wafanyabiashara, mabalozi, Wabunge, Wawakilishi na wale wote walizojitokeza kutoa misaada. Shukurani maalum ziwaendee wananchi wa Nungwi kwa ushirikiano mkubwa walioutoa katika uokozi pamoja na vyombo vya habari kwa kutoa taarifa kwa wananchi.

Kwa upande wake, Serikali itaendelea kuhakikisha wenye vyombo vya usafiri baharini wanatekeleza wajibu wao hasa kuhusu usalama ipasavyo. Uchunguzi utafanywa kutambua kikamilifu sababu ya ajali hii na taarifa rasmi itatolewa kwa wananchi.

Ndugu Wananchi
Nakuhakikishieni kuwa Serikali inathamini sana ushirikiano na michango iliyotolewa. Serikali ipo pamoja na wananchi wote katika maafa haya.
Inna Lilah Wainna Ilayhi Rajiun!
Ahsanteni sana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.