Habari za Punde

TAARIFA YA IKULU - AJALI YA MELI

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejiandaa kuwahudumia wale wote waliopatwa na maafa wakiwemo waliokufa na walio hai kutokana na ajali ya kuzama kwa meli ya Spice Islander.


Ajali hiyo imetokea alfajiri ya kuamkia leo katika eneo la bahari ya Nungwi wakati meli hiyo ilipokuwa ikielekea kisiwani Pemba ikiwa ilimepakia abiria pamoja na mizigo.

Dk. Shein ambaye alifuatana na Mama Mwanamwema Shein walifika hapo Nungwi mapema asubuhi ambapo pia, viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Bi Asha Balozi, viongozi wa vyama na serikali pamoja na wananchi kutoka maeneo mbali mbali.

Dk. Shein akizungumza na wananchi huko katika ufukwe wa Nungwi ambako baadhi ya maiti na majeruhi walikuwa wakiokolewa, alieleza kuwa tukio hilo kubwa ni la kwanza kutokezea hapa Zanzibar na kueleza kuwa tukio hilo pia, limeathiri familia pamoja maendeleo ya nchi.

Alisema kuwa tayari taratibu zimeandaliwa kwa ajili ya kuweka mahali maalum kwa majeruhi pamoja na eneo maalum kwa ajili ya wale waliokufa.

Alieleza kuwa kwa wale waliookolewa wakiwa hai wengine wanapelekwa katika hospitali ya Kivunge iliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa ajili ya kuangaliwa afya zao na kwa wale ambao afya zao si nzuri sana watapelekwa katika hospitali Kuu ya MnaziMmoja.

Dk. Shein aliwaomba wananchi wote kuwa watulivu na kuwapa nafasi madaktari ili waweze kutoa huduma za afya kwa wananchi waliopata matatizo.

Alieleza kuwa wananchi hao wanahitaji huduma muhimu ikiwa ni pamoja na kupata hewa na matibabu mengine.

Alisisitiza kuwa serikali itakuwa inaendelea kutoa taarifa rasmi kwa wananchi kila mara ili wananchi waweze kufahamu hali inavyoendelea na kuwataka waandishi wa habari wanaotoa taarifa juu ya tukio hilo kushirikiana na Idara ya Habari Maelezo kwa ajili ya kupata taarifa sahihi.

Dk. Shein alieleza kuwa jitihada za serikali zinaendelea kuchukuliwa kwa mashirikiano ya vikosi vyote vya ulinzi na usalama vikiwemo vya SMZ na vile vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, alisema madaktari kutoka taasisi mbali mbali na mashirikika ya maafa yakiwemo Shirika la Msalaba Mwekundu wanaendelea kutoa ushirikiano wao katika kuwahudumia majeruhi.

Dk. Shein alieleza kuwa tayari muda si mrefu kikao maalum cha serikali kitakaa, Ikulu mjini Zanzibar kuzungumzia tukio hilo.

Akiwa hapo Nungwi Dk. Shein alipata nafasi ya kuwaangalia na kuwapa pole wale waliookolewa wakiwemo watoto, vijana na wazee wa kike na kiume.

Pia, Dk. Shein alifika katika hospitali ya Kivunge ambako alipata nafasi ya kuwapa pole wagonjwa wa tukio hilo ambao wamelazwa katika hospitali hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuondoka katika eneo hilo, Dk. Shein alisema kuwa serikali imeajiandaa vizuri na ndio maana imeunda Kamati maalum ya maafa ili kuweza kukabiliana na hali kama hiyo.

Aidha, alisema kuwa kutokana na Zanzibar kuwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndio maana imeona kuna haja ya kupata nguvu za ziada kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Polisi ili kusaidia juhudi za uokozi.

Mapema akitoa taarifa kwa Dk. Shein Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Pembe Juma Khamis alieleza kuwa mapema asubuhi waliokolewa baadhi ya watu na wamepelekwa katika hospitali ya Kivunge.

Mkuu wa Mkoa huyo pia, alieleza kuwa vyombo mbali mbali vya majini vimeweza kufika katika eneo la tukio na kusaidia kuokoa ikiwemo boti ya Sea Express ambayo iliokoa majeruhi 259 wakiwa hai na maiti 49 ambapo baada ya hapo boti hiyo ilielekea katika Bandari ya Malindi kutokana na kutoweza kufunga gati katika eneo la Nungwi.

Hadi Mhe. Rais anaondoka katika eneo la Nungwi bado juhudi za uokozi zilikuwa zinaendelea na majeruhi mbali mbali walikuwa wakiendelea kushushwa kutoka baharini na kupelekwa katika eneo hilo lililotengwa kwa ajili ya kupata huduma za afya.

Rajab Mkasaba

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.