Habari za Punde

MAENDELEO ZIWANI YAKABILIWA NA CHANGAMOTO

Na Abdi Suleiman, Pemba

UKOSEFU wa vitendea kazi, jengo la ofisi na fedha za kutosha kwaJumuiya ya Maendeleo ya Jimbo la Ziwani Chake Chake Pemba, ndio kikwazo kikubwa kinachoikumba jumuiya pamoja na kurudisha nyuma
maendeleo yake.

Hayo yameelezwa na mwanachama wa jumuiya hiyo, Khamis Ali Khamis, aliposoma risala katika uzinduzi wa mradi wa kuelimisha sera na sheria ya uvuvi Zanzibar, katika ukumbi wa michezo Gombani kisiwani Pemba.


Alisema kuwa, kukosekana kwa fedha, ofisi na vifaa vya kisasa kama kompyuta, mashine ya fotokopi hurudisha nyuma maendeleo ya jumuiya yao katika ulimengu huu wa sayansi na teknolojia, ambayo ndio roho ya maendeleo.

Alifahamisha kuwa, licha ya kuwepo kwa changamoto hizo, lakini tayari wameshatekeleza mradi wa maji safi na salama kwa wakaazi wa vijiji vinne ndani ya jimbo hilo ambavyo ni Michungwani, Kukuchuni, Kichuwani na Birikau uliofadhiliwa na Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya
Maendeleo.

Aidha alieleza kuwa mradi huo wa uvuvi salama katika Jimbo la Ziwani, utalenga zaidi Shehia za ukanda wa baharini ikiwemo Ndagoni, Michungwani, Kwale na Ziwani ndizo ambazo zenye wavuvi na zilizo hatarini kwa uchafuzi wa mazingira kutokana na kukosa maelekezo ya
uvuvi salama pamoja na uharibifu wa mazingira ya baharini.

“Mradi wetu mpya umelenga kutoa elimu ya uvuvi salama ili kuyafanya mazingira yawe rafiki yaani mwanadamu afaidike na mazingira yake na mazingira yapate hifadhi kutoka kwa mwaadamu” alieleza Khamis.

Mapema akizindua mradi huo, afisa mipango ofisi ya Mkuu wa wilaya Chake Chake, Kassim Ali Omar, kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Mwanajuma Majid, ameitaka jumuiya hiyo kufanya jitihada za haraka kuweza kuyarudisha mazingira ya bahari yaliyoharibiwa na mwanadamu kwa kupanda mikoko.

Alisema ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia na kuweza kutumia soko la kisasa, wavuvi lazima wabadilike kwa kutumia vyombo vya kisasa na kuachana na matumizi mabaya ya utumiaji wa nyavu zenye macho madogo pamoja na uharibifu wa mazalio ya samaki.

Alifahamisha kuwa, mazalio ya samaki mengi hivi sasa yameharibika, na hata kuangamizwa kutokana na uvuvi mbaya, unaofanyika na kupelekea hata samaki wengi kupungua kutokana na uharibifu wa mazingira unaofanywa na wavuvi.

Aidha alisema kuwa, serekali ya wilaya iko pamoja na jumuiya hiyo,katika hatua za kutoa elimu na kuhusisha wavuvi juu ya sera na sheria ya uvuvi na kuipongeza jumuiya hiyo kwa hauta waliyoichukua ya kuwapatia elimu wavuvi.

“Ni jambo zuri na la kuigwa na jumuiya nyengine juu ya kuwaelimisha wavuvi katika utumiaji wa sera na sheria na kuacha kuharibu mazingira ya bahari juu ya uvuvi mbaya unaofanywa na wavuvi” alifahamisha Afisa Mipango huyo.

Jumuiya ya maendeleo ya Jimbo la Ziwani, ilianzishwa mwaka 2007 kupatiwa usajili Oktoba 10 mwaka 2008 chini ya sheria Namba 6 ya mwaka 1995 ya jumuiya za kijamii Zanzibar na kupewa hati ya usajili Namba 660, ambapo ilianza ikiwa na wanachama 20 wanaume 12 na wanawake 8 ikiwa hadi sasa inahitaji wanachama wapya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.