Na Mwandishi wetu
KAMPUNI ya usafiri wa baharini, Seagull, imejitokeza kuinusuru Ligi Kuu ya soka Zanzibar msimu wa mwaka 2011/2012, kwa kuidhamini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Meneja Masoko wa Kampuni ya Seagull, Rehema Yussuf, amesema udhamini huo utagharimu shilingi milioni 41. 5 katika kipindi cha mwaka mmoja.
"Seagull itabeba gharama za usafiri kwenda katika vituo Unguja na Pemba, lakini pia tutaizawadia timu itakayotwaa ubingwa shilingi milioni 10", alisema Meneja huyo.
"Lakini pia tutampatia mshindi wa pili zawadi ya shilingi milioni 5 huku kila timu ikipewa jezi seti mbili zitazokuwa zikitumika katika ligi hiyo", alieleza.
Alisema, Seagull imeamua kudhamini ligi hiyo, ikiamini michezo ni miongoni mwa sekta zenye mchango mkubwa wa maendeleo ya taifa na watu wake.
"Ni imani yetu kwamba udhamini huu, ambao siyo mkubwa sana kwa kiasi fulani utazisaidia timu zetu kupunguza gharama za kujiendesha, lakini pia utachangia kuongeza msisimko wa ligi yenyewe", alisema, Rehema.
Aidha, Meneja huyo alielezea matarajio ya Kampuni ya Seagull kuongeza udhamini huo katika miaka ijayo kulingana na hali itakavyoruhusu na hali nzima ya udhamini huo.
"Hapa tumeanzia, ni matumaini yetu kwenda mbele zaidi ya hapa, kutegemea na hali itakavyokuwa", alisema.
Naye Katibu Msaidizi wa ZFA, Masoud Attai, aliishukuru kampuni hiyo kwa kujitokeza kudhamini ligi hiyo itakayokuwa na timu 12 ambapo bingwa wake ataiwakilisha Zanzibar katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Kagame Afrika Mashariki na Kati, huku mshindi wa pili akicheza Kombe la Shirikisho.
"Ni hatua moja kubwa iliyofikiwa na ZFA, bado tunaendelea na jitihada za kutafuta wadhamini wengine watakaoweza kudhamini mambo mengine yaliyobakia", alisema.
"ZFA imejipanga vizuri kuhakikisha ligi hiyo inakuwa na msisimko na ushindani zaidi, kwa kutafuta wadhamini wengine", alisema, Attai.
Katika hatua nyengine, Attai, alisema, Ligi Kuu ya Zanzibar inatarajiwa kuanza Novemba 1 ambapo mzunguko wa kwanza utakamilika Disemba 27.
Ligi hiyo itajulikana Ligi Kuu ya Seagull na kuchezwa katika viwanja vya Amaan na Mao Dzedong kwa Unguja na Gombani, Pemba.
Timu zitakazoshiriki ngarambe hizi, ni Miembeni United, Miembeni FC, Polisi, KMKM, Mafunzo, Kikwajuni, Jamhuri, Super Falcon, Chipukizi, Zimamoto, Mundu na Chuoni.
Kampuni ya Simu ya Zantel ilijitokeza kudhamini Ligi Kuu ya Zanzibar mwaka 2008 kabla ya kujitoa katika msimu wa 2010.
Chini ya udhamini huo, bingwa wa Zanzibar alizawadia fedha taslimu shilingi milioni 5 na mfungaji bora akatunukiwa kiatu cha dhahabu na Kampuni ya Multi Color.
Haya tena w'znz. kama SEAGULL wameyashinda makampuni makubwa kama Z'TEL na PBZ, ndio muone kuwa 'kutoa ni moyo si utajiri' na muwape 'tafu' wadau, hao inaonyesha wanataka kutumia sehemu ya faida ndogo waliyoipata ktk biashara,huku wakiamini na nyinyi mtaendelea kuwapa ushirikiano...nipe nikupe ndio mtindo wa kisasa'
ReplyDelete