BUNGE limesema muswada wa marekebisho ya katiba uliopitishwa na wabunge sio muswada wa kubadilisha katiba kwa kuwa katiba ya sasa haitabadilishwa bali itaandikwa upya na serikali iliyopo madarakani na bunge.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Ushirikiano wa Kimataifa Ofisi ya Bunge,suala hilo limekuwa likipotoshwa na baadhi ya wadau aidha kwa makusudi au kwa kutojua tofauti ya katiba na sheria ya kawaida.
Aidha, taarifa hiyo ilisema muswada huo ambao unasubiri kutiwa saini na Rais Kikwete kuwa sheria, ni kama mwingine wowote uliowahi kupitishwa na Bunge, na ni wa kawaida unaoweka utaratibu wa kuwafikia wananchi, kuwasikiliza, kupata utashi wao juu ya mapendekezo ya kuandika katiba mpya ili kila Mtanzania aweze kushirikishwa kwa wakati husika moja kwa moja.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa mswada huo utaendelea kusimamiwa na kutekelezwa kama sheria nyingine yoyote ambayo utekelezwaji wake unaweza kusababisha mtizamo tofauti na hivyo kupelekea kufanyiwa marekebisho endapo itaonekana kuwa ipo sababu ya kufanya hivyo.
“Muswada huo ulilenga katika kuweka chombo ambacho kitafanya kazi ya kuchukua maoni ya wananchi ili kuyapeleka katika Bunge la Katiba, ambalo, nalo litakuwa na nafasi ya uwakilishi wa kila mtu katika jamii kwa utaratibu wa uwakilishi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Ufafanuzi huu umetolewa huku kukiwa na mgongano wa mawazo kuhusu msamiati “Muswada wa Sheria ya mabadiliko ya katiba mwaka 2011” uliotumika kwenye muswada huo.
Kuna wanaosema kuwa muswada huo ni wa mabadiliko ya katiba huku wengine wakisema ni muswada wa kuanzisha tume ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu katiba mpya.
No comments:
Post a Comment