Habari za Punde

WAWAKILISHI KUWAENDEA WABUNGE NUNGWI

Na Mwajuma Juma

KATIKA kujiandaa kwa ajili ya pambano la soka dhidi ya timu ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, timu ya Baraza la Wawakilishi inapanga kupiga kambi katika kijiji cha Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Wawakilishi hao wataivaa timu hiyo ya bunge ukiwa mchezo wa kirafiki maalumu kwa ajili ya sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara ambao umepangwa kufanyika kwenye uwanja wa Uhuru.


Akizungumza wakati wa mazoezi ya timu hiyo kwenye uwanja wa Mao Dzedong, Msaidizi Meneja wa watunga sheria hao Nassor Salim Ali 'Jazeera', amesema kambi hiyo itaanza Novemba 28, ikitarajiwa kuchukua siku kumi.

Pamoja na kuelekeza utayari wa kikosi chake, Ali alizishukuru taasisi mbalimbali zilizojitokeza kuichangia timu hiyo kwa misaada mbalimbali ikiwemo vifaa.

"Tuko katika mazoezi makali, na inaonesha wazi wachezaji wetu wameshajenga uwezo wa kushinda mchezo huo, kwani wanafuata vyema maelekezo ya mwalimu", alijigamba.

Naye nahodha wa timu hiyo Ali Abdallah Ali, alisema pamoja na kufahamu kuwa pambano hiko litakuwa gumu, lakini kikosi chake kiko imara kuwavaa watoto wa Anna Makinda, ambao kwa sasa wako nchini Burundi kushiriki mashindano ya mabunge ya Afrika Mashariki

Kwa upande wake, kocha wa timu hiyo Juma Sumbu, alieleza kuridhishwa na uwezo wa wachezaji wake, na kueleza kuwa, timu hiyo itakuwa kamili baada ya kuungana na wawakilishi wenzao walioko Pemba kwenda kufanya kazi ya kuwafunga wabunge katika mchezo huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.