Habari za Punde

DK SHEIN AUFUNGUA MSIKITI WA AL HARAMAIN DONGE MUWANDA LEO

Na Rajab Mkasaba

Ataka Waislamu kuipa umuhimu elimu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein amewakumbusha waumini wa dini ya Kiislamu juu ya umuhimu wa elimu hasa kwa watoto na kusisitiza kuwa Uislamu haujaweka mipaka ya elimu hasa katika mambo anayoridhia MwenyeziMungu.

Alhaj Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Donge Muwanda, Mkoa wa Kaskazini Unguja wakati wa ufunguzi wa msikiti wa Ijumaa wa Donge Muwanda (Masjid Al-Haramain).



Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa miongobni mwa jambo ambalo MwenyeziMungu amelipa nguvu kwa Waislamu ni suala la kutafuta elimu kwani hiyo ni amri kwa Waislamu wote kujibidisha juu ya jambo hilo.

Kutokana na hali hiyo Alhaj Dk. Shein aliwaeleza wazazi kuwa wana wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wote wenye umri wa kwenda skuli wanapata fursa hiyo.

Alhaj Dk. Shein alitoa nasaha zake kwa wazazi kutilia mkazo suala la elimu kwa vijana ili iwe taa kwa maisha yao ya hapa duniani na akhera na kuwasisitiza wafanyabiashara wa vifaa vya skuli wawe na huruma kwa kutoa bei watakazozimudu wazazi ambazo hazitowavunja moyo katika kipindi hichi cha maandalizi.

Aidha, Dk. Shein aliwataka wazazi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao vyuoni au madrasa ili waijue dini yao na kupata maadili mema na kusisitiza kuwa MwenyeziMungu ameshasema kuwa kamwe hawawezi kuwa sawa mwenye elimu na asie na elimu.

Alhaj Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kuwasihi wananchi waliojaaliwa uwezo wa kusaidia kujenga misikiti na madrasa ambazo ndio chimbuko la elimu na malezi ya Kiislamu kwa watoto wajenge kwani kuna ujira mkubwa mbele ya Allah.

Pamoja na hayo Dk. Shein aliwataka Waislamu kuwa wamoja na kuepuka mambo yote yatawatenganisha na kuwasisitiza kuelekeza jitihada zao katika kumtakasa MwenyeziMungu na kuzishukuru neema zake.

Alieleza kuwa kwa bahati mbaya sana kuna baadhi ya misikiti hukumbwa na misuko suko ya mizozo baina ya waumini ikiwemo kugombania vyeo na uongozi wa misikiti, jambo ambalo linawashusha hadhi waumini hao mbele ya macho ya watu wengine.

Kutokana na maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa hali hiyo pia, ni kinyume cha maamrisho ya MwenyeziMungu huku akisisitiza wajibu wa kuitunza misikiti.

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwapongeza wananchi wa Donge kwa mchango wao mkubwa katika shughuli za kilimo cha chakula na biashara kwa mazao ya chakula hasa viazi na karafuu.

Alhaj Dk. Shein alitoa wito wa kuongeza jitihada katika kilimo na kuwanasihi wananchi wa Donge kuongeza juhudi katika kupanda mikarafuu mipya na kuendelea kushirikiana na serikali katika kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Pia,alisisitiza kuwa azma ya Serikali ni kurejesha hadi ya karafuu ili zitoe mchango unaostahili katika kuendeleza uchumi.

Nao wananchi wa Donge Muwanda katika risala yao walitoa shukurani kwa Mfadhili aliojenga msikiti huo Sheikh Adil bin Othman, na kueleza kuwa kabla ya hapo msikiti waliokuwa wakisalia ulikuwa mdogo na haukidhi haja.

Mapema Viongozi wa Dini na Masheik katika hutuba zao ikiwemo hutba ya Ijumaa,walieleza fadhila za watu wanaojenga misikiti na jinsi gani MwenyeziMungu alivyowatayarishia nyumba nzuri huko Peponi.

Nae Waziri wa Ardhi, Makaazi, Nishati na Maji Mhe. Ali Juma Shamuhuna ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Donge akitoa neno la shukurani kwa niaba ya wananchi wa Muwanda, alimshukuru Dk. Shein pamoja na viongozi wengine wa dini, vyama vya siasa na serikali kwa kushiriki katika hafla hiyo na kueleza jinsi Donge ilivyojidhatiti katika kilimo cha biashara na chakula.

Viongozi mbali mbali wa vyama, serikali pamoja na dini ya Kiislamu kutoka Zanzibar na Tanzania Bara walihudhuria katika sherehe za ufunguzi huo viongozi waliohudhuria ni pamoja na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Idd, Rais Mstaafu Alhaj Dk. Amani Karume na wengineo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.