Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema itafungua Akaunti Maalum za Michango ya Fedha zitakazotumika kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa Mafuriko ambayo yamesababisha vifo na uharibifu mkubwa katika maeneo ya Tanzania Bara.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohammed Aboud Mohammed wakati alipokuwa akitowa taarifa kuhusu tahadhari juu ya mwelekeo wa mvua za vuli zinaziendelea kunyesha Nchini kwa sasa.
Amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itahakikisha kuwa inashirikiana vyema na Seriakali ya Muungano katika kukabiliana na maafa hayo kwa kutoa michango ya hali na mali kwa ajili ya wahanga wa Mafuriko.
Waziri Aboud amesema katika kupata fedha hizo Serikali imeandaa utaratibu maalum wa kuwashajihisha wananchi, wafanyabishara, taasisi za Serikali na zisizokuwa za kiserikali kutoa michango yao ili kufanikisha lengo hilo
Aidha amesema Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ndiyo itakayoratibu misaada yote na baadaye kuwasilishwa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kuwafikia Wahanga wa maafa hayo.
Amesema kwa wale wote waliokuwa Mikoani Ofisi za mikoa Unguja na Pemba zitapokea misaada hiyo na baadaye kuwasilishwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ili kuwasilishwa kwa wahusika.
Wakati huo huo Waziri Aboud ameziagiza Ofisi za Wakuu wa Mikoa kupitia Kamati za Maafa za Mikoa kuainisha maeneo maalum yatakayoweza kutumika kwa makaazi ya dharura iwapo baadhi ya wananchi katika maeneo yao watakumbwa na mafuriko
Amezitaka taasisi husika na Wizara ya Afya,Miundo mbinu ,Baraza la Manispaa na Idara ya Uvuvi kuendelea kuwapa wananchi taarifa za sekta zao kila inapohitajika ili kuhakikisha wananchi wanakuwa katika hali ya usalama na utulivu.
Kwa upande wa viongozi wa Dini Waziri Aboud amewaomba viongozi hao nchini kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu kwa imani zao ili alete Mvua za kheri na Baraka na kuepusha madhara yote yanoyoweza kutokea.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya Zanzibar iliwahi kutoa mwelekeo juu ya hali ya Mvua mwaka huu na kusema kuwa Mvua za Vuli zitakuwa kubwa kuliko kiwango cha kawaida katika baadhi ya maeneo
Mafuriko ambayo yameikumba mikoa mbali mbali ya Tanzania Bara ikiwemo Dar es Salaam, Iringa Pwani na Mbeya yamesababisha kupelekea upotevu wa maisha, mali, kubomoka kwa nyumba za makazi na majengo ya kibiashara pamoja na miundo mbinu.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR 23/12/2011

No comments:
Post a Comment