Kwanza tunapenda kutoa Shukrani zetu zinazotoka ndani ya moyo kwa wahusika wote waliobahatika kututembelea katika Blog yetu ya Zanzinews kwa mwaka 2011.
Kutembelea kwenu pamoja na kusoma na kutoa maoni katika habari, picha na matukio ni moja katika kichocheo na msukumo unaotufanya tuendeleze harakati hizi za kublog japo katika mazingira magumu.
Pia tunapenda kuwashukuru wote wanaotutumia habari, picha, matukio kwa kuonesha moyo wa ushirikiano na kuwa na thiqqa na Zanzinews kama ni chombo muwafaka cha kuweza kufikisha ujumbe wao ili kuifikia jamii popote pale ilipo katika ulimwengu huu wa Arrahmaan.
Pia wanahabari wenzangu katika gazeti la ZanzibarLeo hasa waandishi kwa kuweza kuwa pamoja katika kuwafikishia habari wadu kwa ujumla. Mchango wenu ni muhimu sana kuweza kuendeleza. Shukurani pekee zimwendee Abou Shatry wa swahilivillablog ambaye alitoa msaada mkubwa wa kiufundi kuikarabati blog na kuwa katika mwonekano ulio hivi sasa. Pia Ndugu zangu Ramadhan Othman (Ikulu), Rajab Mkasaba (Ikulu), Othman Khamis Ame, Hassan hamad (OMKR), Idara ya habari (Maelezo) na wengineo. Kutoka nje ni Dk Yussuf S Salim, Narendra Gajjar, Da Subi na Urban Pulse. Pia Wanaphotojournalist wenzangu kina Martin Kabemba, Ali Othman, Salmin Said, Abdalla Masangu na wengineo
Kwa upande wa wenye kutoa maoni (comments), shukurani za dhati kwa Adhubany ambae amekuwa mstari wa mbele katika kucomment na pia kwa wale wote waliopendelea kuwa anonymous wakati wa kutoa maoni yao.
Zanzinews blog imeweza kupiga hatua kwa kuweza kuongeza idadi ya wanaotutembelea kutoka wastani wa Elfu 15 kwa mwezi 2010 hadi Elfu 25 mwaka 2011 na kila siku idadi hii inaongezeka kuthibitisha kwamba kazi hii inazidi kukubalika. Tunawashukuru sana wadau kutoka Uingereza ambao ndio watembeleaji wakubwa wa blog wakifuatiwa na Tanzania na Marekani. Hii pia inaweza kutupa picha kwamba Wazanzibari wengi walio Diaspora basi wapo Uingereza.
Mwaka 2011 pia tulibadilisha jina la Blog ili liendane sambamba na maudhui ya blog yenyewe kwa kujikita zaidi katika kuwapasha habari jamii ya kizanzibari popote ilipo ulimwenguni.
Zanzinews imejitahidi kulenga katika eneo maalum kufikisha ujumbe na pia kujiepusha kwa kiasi kikubwa na kuwa na utamaduni wa kuchukua habari kutoka blog nyengine, vyanzo vyengine vya habari mpaka habari iwe na uzito na umuhimu mkubwa kupaswa kuwepo kwenye ZanziNews blog kwa maslahi ya Wazanzibari. Na mara nyingi habari tunazoziweka hutumiwa na wahusika kupitia anuani yetu othmanmaulid@gmail.com
Changamoto pia zipo nazo ni kukosa zana za kuendeleza hii kazi kwani hadi hivi sasa bado tunategemea Kompyuta za kazini au Internet cafe. Pia kupata muda wa kuweza kuwaletea habari motomoto na up to date kwani wakati mwengine kuwepo mbali na Kompyuta na pia Kompyuta zikileta taabu kidogo tu basi mchezo inabidi uwekwe kiporo.
Pia kwa kuwa kazi hii ni ya ujenzi wa taifa (kujitolea) inakuwa vigumu kuweza kupata msaada inapohitajika. Hata hivyo ninapenda kumshukuru mwanahabari mwenzangu na mwandishi wa ITV Farouk Karim kwa kuweza kunipa sapoti na msaada kila anaponafasika.
Pia bado kuna habari na taarifa nyingi ndani na nje ya Zanzibar ambazo hazitolewi na hivyo kukosa nafasi ya kujuzwa jamii yanayojiri nyumbani na nje.
Ila tukio la kuzama kwa MV Spice katika mwezi wa Septemba 2011 ni tukio moja ambalo hatuna budi kuliweka katika kumbukumbu za mwaka 2011 kwa jinsi lilivyoshitua Wazanzibari na ulimwengu kwa ujumla hasa kwa kuweza kupata janga la msiba ambalo lilichukuwa maisha ya wanyonge, wadhaifu, wasio na uwezo ambao idadi yao ni MwenyeziMungu pekee ndio anaeijua na katika historia ya visiwa hivyi halijawahi kutokea huku likiwaacha wengine yatima, vizuka na kadhalika. Mwenyezi Mungu awalaze mahala pema wote waliofariki na awape subira jamaa, ndugu wa waathirika wote.
Habari ndiyo chachu ya kuleta maendeleo katika jamii kwani hupatikana taarifa, maendeleo, maoni, ushauri,kukosolewa na kurekebishwa na pia miongozo na kadhalika.
Tunawatakia wadau wote heri ya mwaka 2012 na InshaAllah tunawaahidi kuiendeleza ZanziNews blog na tuwe pamoja si katika kuja na kusoma tu habari na taarifa bali nanyi mna nafasi ya kuonesha mambo ambayo mnajifunza huko mlipo kwa faida ya visiwa vyetu na maendeleo yetu ambayo yanawategemea wanadiaspora katika kuharakiza gurudumu hili la maendeleo. Pia kwa wenyeji wa nyumbani mnakaribishwa kuleta habari zenu, picha na matukio yoyote ambayo hayawezi kuwa habari mpaka yatangazwe na hayawezi kuwa taarifa mpaka yataarifiwe.
Shukran
Tuandikie othmanmaulid@gmail.com
ZanziNews Admin
tupo pamoja mkuu inshalah
ReplyDeleteAhsante sana kwa kutuwekea habari za nyumbani hapa.
Zanzinews is the best Blog Ever.
HAPPY NEW YEAR 2012
Hongera sana kwa kuweza kutupa taarifa na matukio kadhaa toka nyumbani (Visiwani).Kwa kweli inapendeza kuwepo watu kama nyinyi ambao mko tayari kutumika kwa maslahi ya umma kwa hakika tunatarajia makubwa zaidi kwa mwaka 2012 ishallah.
ReplyDeleteNakutakia kazi na maisha mema na yenye mafanikio kwa mwaka ujao. AHSANTE.
Kaka kila la kheri, kazi njema!
ReplyDelete