Habari za Punde

ZFA YAKALIA RIPOTI YA FUTURE CENTURY

Baada ya kufafanuliwa mapato, matumizi yaunda kamati kuchunguza

Na Salum Vuai, Maelezo

BAADA ya kikao cha Kamati Tendaji ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) na uongozi wa kampuni ya Future Century Limited, ZFA imeshindwa kutoa taarifa kuhusiana na fedha zilizokusanywa kwa kuisaidia timu ya taifa ya soka Zanzibar Heroes.

Kamati Tendaji ya chama hicho, ililazimika kukutana na uongozi wa Future Century, kufuatia agizo la Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), baada ya kuwepo malalamiko kwamba Zanzibar Heroes ilishiriki
kinyonge michuano ya Chalenji iliyofanyika Dar es Salaam hivi karibuni.

Msemaji wa ZFA Hafidh Ali Tahir, ameliambia gazeti hili kuwa, baada ya Future Century ambao ni wakala wa kuitafutia udhamini Zanzibar Heroes kutoa maelezo mbele ya kamati hiyo, ZFA imeamua kuunda kamati mbili ili kutathmini na kuyapitia kwa kina kabla kutoa taarifa kwa umma.


“Tumewasikiliza watendaji wa Future Century, wamesema ya kwao, nasi tumekubaliana tuyafanyie tathmini kwa kuunda kamati mbili, moja ya ligi na nyengine kuangalia mikataba kama hii na ule wa Sea gull, baada
ya hapo tutawajuvya wananchi kupitia vyombo vya habari”, alifafanua Tahir.

Hata hivyo, uchunguzi wa Zanzibar Leo kutoka ndani ya Kamati Tendaji ya ZFA, umegundua kuwa hakuna mkataba wowote unaotambulika kwa sasa kati ya ZFA na Future Century.

Chanzo chetu cha uhakika kimefahamisha kuwa, kwa mujibu wa maelezo ya Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni hiyo, mkataba wa kwanza ambao ulikuwa wa ubia wa kampuni mbili na ZFA, ulikufa baada ya kampuni moja kujiondoa.

Baada ya kujitoa kwa kampuni hiyo iitwayo Global Scouting Bureau, ZFA ilipaswa kuomba kusaini mkataba mwengine lakini haikufanya hivyo, na kuifanya Future Century iitumikie Heroes bila makubaliano maalumu.

Aidha alifahamisha kuwa, kampuni hiyo iliwaambia kwamba ilimudu kukusanya si zaidi ya shilingi milioni 50, na kwamba kampuni na taasisi kadhaa zilizoahidi kuchangia, hadi sasa hazijawasilisha michango yao.

Bila kutaja kiasi cha fedha, mjumbe huyo wa Kamati Tendaji, alisema pamoja na Future Century kukusanya fedha hizo, lakini imeainisha matumizi yanayopindukia kiasi kilichopatikana kuonesha kuwa ilitumia
fedha nyingi kuihudumia Heroes katika mambo mbalimbali, ambapo bajeti ilipangwa na kutolewa na ZFA kwao.

“Kwa hali hii, imeonekana kuwa Future Century inatudai sisi, lakini mimi naona kuunda kamati kuchunguza kadhia hii ni kupoteza wakati kwa sababu hakuna mkataba unaoweza kuifunga kampuni hiyo”, aliweka wazi.

Future Century iliandaa hafla ya chakula cha usiku Machi 26, mwaka huu kwenye hoteli ya Zanzibar Beach Resort ikiwa harambee ya kuichangia Zanzibar Heroes ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.