Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Ujumbe uliofuatana na Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Alfonso Lenherts,walipofika Ikulu Mjini Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Alfonso Lenherts,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar
Picha na Ramadhan Othman, Ikulu
Habari na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amepongeza juhudi za Serikali ya Marekani kupitia Mashirika yake ya Misaada kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha Miradi ya maendeleo hapa nchini.
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mhe, Alfonso Lenhardt akiwa na ujumbe wake alipofika Ikulu mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar inathamini sana mashirikiano inayopata kutoka kwa Serikali ya Marekani ambayo yameweza kuunga mkono juhudi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuimarisha miradi yake ya maendeleo.
Alieleza kuwa miongoni mwa ushirikiano huo ni pamoja na kuendelea kuunga mkono miradi ya afya, elimu, nishati, miundombinu ya barabara, kuimarisha hali za maisha ya wananchi kiuchumi, kupunguza vifo vya wazazi na watoto na kuendeleza huduma za kijamii sanjari na kuimarisha Utawala Bora na mengineyo.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Marekani imeweza kutoa mchango wake mkubwa katika mafanikio yaliopatikana juu ya kupiga vita Malaria na kuwa nchi ya kwanza katika bara la Afrika kufanikiwa katika mradi huo uliosimamiwa na nchi hiyo kwa mashirikiano na serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Mbali ya hayo, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Marekani imekuwa mstari wa mbele kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi yake ya maendeleo kwa muda mrefu hatua ambayo imeweza kuleta manufaa kwa kiasi kikubwa hasa kupitia Mashirika yake ya Misaada ya USAID, MCC, PMI, PEPFAR na mengineyo.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa kutokana na juhudi za serikali katika kuwaongezea uwezo wa elimu watumishi wake bado Zanzibar inahitaji uungwaji mkono na Marekani ili watumishi hao waendelee kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi wa kitaalamu.
Dk. Shein alimuhakikishia Balozi huyo kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliyopo tokea miaka ya 1800 iliyopita ambapo nchi hizo mbili zilianza uhusiano.
Nae Balozi wa Marekani Mhe. Alfonso , alimueleza Dk. Shein kuwa Marekani inafarajika kwa kiasi kikubwa na mashirikiano mazuri inayoyapata kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huku akipongeza juhudi za uongozi wa Dk. Shein na serikali yake tokea kuingia madarakani.
Balozi huyo wa Marekani aliahidi kuwa Serikali ya Marekani itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha miradi yote inayoisimamia inaimarika na kuweza kuleta manufaa kwa Zanzibar na wananchi wake.
Katika kuendelea kuiunga mkono sekta ya afya hapa Zanzibar, Balozi huyo wa Marekani alieleza kuwa Serikali ya Marekani kwa kushirikiana na madaktari wazalendo wamo katika kutoa huduma ya magonjwa ya macho huko katika Hospitali ya Bububu mjini Unguja.
Alieleza kuwa zoezi hilo linaloendelea huko katika hospitali ya Bububu limewashirikisha wataalamu hao 20 kutoka Marekani wakiwemo madaktari bingwa sita wa upasuaji wa mtoto wa jicho, wauguzi watano, nesi watano pamoja na wafanyakazi ya utawala wanne.
Balozi huyo pia, alimueleza Dk. Shein kuwa serikali ya Marekani imetoa msaada wa boti mbili kwa ajili ya kusaidia suala zima la ulinzi wa baharini hapa Zanzibar, ambapo boti hizo zilikabidhiwa kwa uongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani.
Aidha, Balozi huyo alieleza kuwa miradi mengine ambayo Marekani imo katika mchakato ni pamoja na mradi mkubwa wa waya wa pili wa umeme wa chini ya bahari kutoka Ras Kiromoni Dar-es-Salaam hadi Ras Fumba Zanzibar chini ya Shirika la MCC pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara huko kisiwani Pemba
Nao wajumbe aliofuatana nao balozi huyo walieleza jinsi Mashirikika ya misaada ya Marekani yalivyodhamiria kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya, kwa kuendeleza programu mbali mbali pamoja na kupanga mikakati juu ya mapambano ya VVU.
Aidha, wajumbe hao walieleza juhudi za pamoja jinsi zilivyozaa matunda katika kupambana na Malaria hapa Zanzibar na kuweza kujijengea sifa kimataifa huku ukieleza mipango yake ya kuendelea kuwajengea uwezo wa kimafunzo madaktari wa Zanzibar.
Pia, ujumbe huo ulieleza azma ya nchi hiyo kuunga mkono changamoto zilizopo katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto, kuendeleza mradi wa lishe kwa wadau wa kilimo kwa kuweza kutoa mafunzo juu ya mazao ya viungo na namna ya kuyasafirisha sanjari na kusaidia Benki za kijamii vijijini (Vikoba).
Kwa upande wa sekta ya elimu kwa kuweza kuimarisha elimu ya msingi kwa kuinua kiwango cha kusoma, kuimarisha somo la hesabati na sayansi sanjari na kutoa elimu ya kompyuta na kuwapa mafunzo waalimu wa skuli za msingi.
Pamoja na hayo, Shirika la USAID limeweza kutoa msukumo mkubwa na kuweza kupata mafanikio katika suala zima la uzazi wa mpango kwa kuweza kuwashirika wadau mbali mbali wakiwemo viongozi wa dini na jamii kwa ujumla pamoja na kuendeleza na kuimarisha programu juu ya uzazi wa mpango.
No comments:
Post a Comment