Habari za Punde

Mazingira Mazuri Ajira Wanaomaliza Elimu ya Juu

Na Mwashamba Juma

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema serikali imejidhatiti kuweka mazingira mazuri ya nafasi za ajira kwa vijana wake wanaomaliza masomo ya elimu ya juu.

Aliyasema hayo wakati akiwatunuku Shahada ya kwanza wahitimu 219 katika mahafali ya 11 ya Chuo kikuu kishiriki cha elimu Zanzibar kilichopo Chukwani waliomaliza vitivo mbalimbali.


Balozi Seif alisema elimu ni moja ya rasilimali ya maendeleo ya nchi katika kukuza uchumi wake, hivyo aliwataka wahitimu kukabiliana na changamoto zinazoikumba dunia ikiwa ni pamoja na kutumia vizuri taaluma na ujuzi walioupata wakiwa chuoni hapo.

Akizungumzia matatizo na mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira pamoja na matumizi mabaya ya dawa za kulevya, Balozi Seif alisema ni changamoto zilizozikumba nchi nyingi ikiwemo Zanzibar.

Hivyo, aliwataka wahitimu wa kitivo cha sayansi na kitivo cha elimu jamii kuwa mabalozi wazuri kwa jamii katika kufikisha elimu ya kulinda na kuhifadhi maliasili za taifa kwani elimu ni zana muhimu ya kuzuia uharibifu wa mazingira.

Aidha aliwataka wahitimu wa kitivo cha mafunzo ya dini kwa jitihada na nguvu zao zote wazielekeze kwa kutekeleza daawa, pamoja na kutoa taaluma ya maadili ili kukabiliana na kuzuia wimbi la matumizi ya dawa za kulevya, kwani serikali inatumia pesa nyingi kwa kutumia dawa za hospitali kuwatibu vijana walioathirika na dawa hizo.

Balozi Seif alisema serikali kwa kushirikiana na mamlaka husika imesikia kilio cha tatizo la maji linalokikabili chuo hicho na italitafutia ufumbuzi wa kuliondoa.

Nae Makamu Mwenyekiti wa Afican Muslim Agency Zanzibar Dk. Abdulrahman Al-Muhailan, alisema chuo kimeweka mahusiano ya historia baina ya Zanzibar na nchi ya Kuwait.

Katika kufikia malengo ya Dira ya maendeleo 2020 pamoja na malengo ya MKUZA, Dk. Al-Muhailan alisema elimu inayotolewa na chuo hicho itachangia kwa kiasi kikubwa uwezo wa elimu kwa kizazi cha sasa kushindana na soko la dunia pamoja na kukabiliana na kipindi kipya cha utandawazi.

Aidha, alisema wamejiandaa na kutoa mafunzo yatakayoendana na matakwa ya ukuwaji wa sayansi na teknolojia pamoja na matumizi ya ICT.

Sambamba na kutoa mafunzo yatakayoendana na mahitaji ya soko la ajira la ndani na nje ya Zanzibar.

Chuo kikuu kishiriki cha elimu Zanzibar, kilianzishwa mwaka 1998 ambapo kilianza na wanafunzi 25 kwa wakati huo, kinatoa mafunzo ya dini ya kiislamu, mafunzo ya lugha ya kiarabu, mafunzo ya sayansi pamoja na elimu jamii.

Kwa sasa chuo kimesajili wanafunzi 1207 ambapo miaka 10 iliyopita, Chuo kilihitimisha zaidi ya wanafunzi 1000 hali iliyosababishwa na ukuwaji wa sekta ya elimu nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.