Habari za Punde

Jamii Yaaswa isiwatenge wagonjwa wa ukoma

Na Salum Vuai, Maelezo

JAMII nchini imeaswa kutowatenga watu walioathirika na ugonjwa wa ukoma, na badala yake iwasaidie pamoja na kuwahimiza kwenda hospitali ili kupata tiba sahihi.

Ushauri huo umetolewa jana na Naibu Waziri wa Afya Dk. Sira Ubwa Mamboya katika ukumbi wa wizara hiyo alipozungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Waziri wa Afya Juma Duni Haji, katika maadhimisho ya Siku ya Ukoma Duniani.


Alisema ugonjwa wa ukoma ni wa kuambukiza, ni vyema watu walio salama wawahimize wenzao walioathirika ili kupata tiba, kwani kinyume na hivyo, kutawaweka wengine katika hatari ya kuambukizwa.

Aidha alitanabahisha kwa kusema, jamii inapaswa kutambua kuwa mgonjwa aliyeanza tiba, siyo rahisi kuambukiza mtu mwengine na hivyo, hakuna sababu ya kumtenga, kwani anaweza kuendelea na shughuli zake za kawaida za maisha.

Alitoa rai kwa wananchi wote hasa katika maeneo ambayo yanaendelea kutolewa taarifa za kuwepo wagonjwa wengi wa ukoma, kutambua mapema dalili za ugonjwa huo na kuwahi matibabu.

Aliyataja maeneo ambayo utafiti umeonesha kuwepo kwa wagonjwa wengi hapa nchini tangu zamani, kuwa ni Mkoa wa Kusini Unguja katika vijiji vya Kizimkazi Mkunguni na Dimbani, Kibuteni pamoja na Makunduchi.

"Takwimu za mwaka 2011 zinaonesha kwamba Zanzibar waligunduliwa wagonjwa wa ukoma 81 ambapo kati yao 13, sawa na asilimia 16, walibainika tayari wakiwa walemavu", alifahamisha.

Dk. Mamboya alizitaja dalili za ukoma kuwa ni mabaka kwenye ngozi yasiyokuwa na uwezo wa kuhisi, yanayokosa hisia ya joto, mguso au maumivu, ambayo kwa kawaida hayawashi wala hayaumi.

Dalili nyengine, alisema, ni pamoja na vijinundu vyenye rangi iliyo sawa na ya ngozi, na kusisitiza kuwa endapo mtu ataona dalili hizo, afanye haraka kwenda kituo cha tiba kilicho karibu naye kwa uchunguzi.

Alisema kufanya hivyo, kutawawezesha wataalamu wa afya kuchunguza na kubainisha kama mgonjwa ana ukoma katika hatua za awali ili apate tiba mapema.

Alifahamisha kuwa, maadhimisho ya siku ya ukoma duniani, yanatoa fursa ya kutathmini mwelekeo wa jitihada za kitaifa na kimataifa katika kupambana na ugonjwa huo, akisema kila mmoja ni mdau katika mapambano hayo.

Kwa upande wa serikali, alisema itaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya na wilaya zote kupitia kamati za afya, kutekeleza kikamilifu mikakati mizuri inayopangwa ili kuutokomeza na kuufuta ukoma katika orodha ya maradhi ya kuambukiza yanayoisibu jamii.

Akihitimisha, alilishukuru Shirika la Kijerumani la GLRA, kwa kushirikiana na wizara yake katika uendeshaji wa kitengo cha kifua kikuu na ukoma, sambamba na Chama cha Ukoma Tanzania (TLA), ambacho kimewaweka pamoja walemavu wa ukoma na kutekeleza miradi mbalimbali inayobuniwa kuwawezesha kuiuchumi.

Aidha alieleza kuwa dunia imepiga hatua kubwa katika kutokomeza ugonjwa huo, na ndio sababu kambi zote zilizokuwa zikiwahifadhi wagonjwa kwa ajili ya matibabu zimevunjwa na sasa wachache wanaotokezea hupata huduma za moja wa moja katika hospitali na vituo vya afya.

Siku ya ukoma duniani huadhimishwa kimataifa kila ifikapo Jumapili ya mwisho wa Januari, ambapo mwaka huu imeangukia jana Januari, 29, na ujumbe wake ni 'Dumisha huduma bora kwa watu walioathirika na ukoma'.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.