WIZARA ya Kilimo na Maliasili imeeleza kuwa ‘Mapinduzi ya Kilimo’ ndio mwelekeo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya Awamu ya saba yenye nia ya kutekeleza kwa vitendo dhamira ya kuwakomboa wakulima wa Zanzibar kutokana kilimo duni kisichokuwa na tija na kuweka mazingira na fursa endelevu.
Uongozi wa Wizara ya Kilimo na Maliasili chini ya Kaimu Waziri wake, Ramadhan Abdalla Shaaban ambaye pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, ulieleza hayo wakati ulipokutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Muhamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.
Mkutano huo ni muendelezo wa Dk.Shein kukutana na Wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuangalia Mpango Kazi wa utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2011/2012 kwa kipindi cha robo ya kwanza na ya pili ya mwaka.
Uongozi wa Wizara hiyo ulieleza kuwa hali hiyo itawezesha wakulima kuongeza tija na uzalishaji katika kilimo kwa lengo la kuinua kipato na kuwa na uhakika wa chakula na lishe bora. Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa mwendelezo huo unaendana na Mpango wa Mageuzi ya sekta ya Kilimo (ATI).
Uongozi huo ulieleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2011/2012, Wizara ya Kilimo na Maliasili inatekeleza dhamira ya Mapinduzi ya Kilimo yatakayopelekea kutoa mchango zaidi katika kukuza uchumi wa taifa sambamba na kupunguza umasikini.
Aidha, Wizara hiyo ilieleza mafanikio ya mbegu ya mpunga wa NERICA na kueleza utafiti wa mbegu mpya ya mpunga aina ya chotara kutoka China kuwa unaendelea pamoja na kuendelea kufanya utafiti kwa mazao ya mizizi.
Pamoja na hayo, uongozi huo ulieleza hatua zinazoendelea katika mashamba yanayovamiwa na maji ya chumvi hasa katika maeneo ya bonde la Mziwanda na Wapape ambapo tayari upimaji, uchoraji na usanifu umeshafanyika.
Nae Dk. Shein alipongeza hatua zinazochukuliwa na Wizara katika kuimarisha sekta ya kilimo na Maliasili sanjari na kazi nzuri ya utayarishaji wa Taarifa hiyo ya utekelezaji wa
Mapango Kazi wa mwaka 2011/2012
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya Waziri wake, Said Ali Mbarouk ambaye katika utangulizi wa ripoti ya utekelezaji wa Maendeleo kwa robo ya kwanza na ya pili ya mwaka wa fedha 2011/2012 alitoa pongezi kwa Dk. Shein kutokana na juhudi zake za uongozi nchini.
Alieleza kuwa katika kipindi kifupi cha miezi sita nchi imepiga hatua kubwa za maendelo kutokana na utekelezaji wa malengo yake kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wa Wizara hiyo, Waziri huyo alieleza kuwa katika kipindi hicho cha mienzi sita imeweza kutekeleza shughuli mbali mbali za maendeleo kupitia miongozo na maelekezo anayoyatoa Rais.
Uongozi huo ulieleza kuwa utaratibu huo wa kukutana na Wizara za Serikali kutaka kufahamu hatua za utekelezaji wa mipango ya bajeti za serikali ni njia sahihi ya ufuatiliaji wa shughuli za kila siku za Taasisi za serikali.
Aidha Wizara hiyo ilieleza kuwa kwa mashirikiano na Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika zimewasaidia wanavijiji wa Kiuyu Mbuyuni,Kangani na Mwambe wanaoharibu mazingira kwa kuchimba matofali, kuibua miradi mbadala ya ufugaji wa mifugo bora ili iwasaide kukimu maisha yao ambapo vikundi 16 vimeibuliwa.
Aidha uongozi huo ulieleza kuwa mbali ya vikundi hivyo vinane kati ya hivyo vimetengewa shilingi milioni 80 na mradi wa TASAF/MACEMP ambapo pia imeshaanzisha mpango wa kuwaelimisha wananchi juu ya unywaji wa maziwa kwa kuanzisha Kampeni ya unywaji wa maziwa inayotarajiwa kufanywa mwishoni mwa mwezi wa Februari, 2012.
Pamoja na hayo uongozi huo wa Wizara ulieleza kuwa umeshirikiana na Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko na Wizara Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika kutengeneza waraka wa mapendekezo ya bei ya mwani ambao unatarajiwa kuwasilishwa serikalini hivi karibuni.
Pia, ulieleza juhudi ilizochukua kwa kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wa mwani juu ya mbinu za kusarifu mwani puia, imeandaa miradi ya usarifu mwani. Aidha ilieleza kuwa tayari Sera ya Mifugo ambayo inazingatia masuala ya kuingiza mazao ya mifugo kutoka nje imeshakamilika na imeshapitishwa katika Baraza la Wawakilishi.
Nae Dk. Shein akizungumza na uongozi wa Wizara hiyo alieleza kufarajika na hatua na juhudi zinazochukuliwa na Wizara hiyo katika kuimarisha sekta ya Mifugo na Uvuvi.
Alieleza kuwa malengo pamoja na mikakati iliyowekwa na Wizara hiyo itaisaidia serikali katika kutekeleza kazi zake na wajibu wake kwa wananchi wa Zanzibar.

No comments:
Post a Comment