Habari za Punde

Sheria Mfuko wa Baraza la Wawakilishi Yaandaliwa

 Balozi Sef asema italiepusha Baraza kuwa omba omba

Othman Khamis, OMPR

RASIMU ya mswada wa sheria ya Mfuko wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ni hatua muhimu katika kuweka taratibu zitakazoliwezesha Baraza hilo kutekeleza kazi zake kwa ufanisi mkubwa kwa mujibu wa matakwa ya Katiba ya Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi, Seif Ali Iddi alieleza hayo katika semina ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuhusu rasimu ya mswada wa sheria ya mfuko wa Baraza la Wawakilishi pamoja na ile ya Sensa ya Watu na Makaazi ya Mwaka 2012 iliyofanyika hapo Zanzibar Beach Resort Mazizini Mjini Zanzibar.


Balozi Seif alisema sheria ya mfuko wa Baraza endapo utaanzishwa utaliwezesha Baraza la Wawakilishi kuwa huru katika utendaji wake na kuliondolea utaratibu wa kuomba omba pale linapohitaji fedha kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake.

Balozi Seif alisema kutokana na majukumu hayo ni dhahiri panahitajika kuwepo kwa utaratibu mzuri utakaoliwezesha Baraza hilo kufanya kazi zake ambao ni kuwa na uhuru kifedha.

“Kidemokrasia Baraza la kutunga Sheria halitakiwi kuwa omba omba pale linapohitaji fedha kwa ajili ya kuyetekeleza majukumu yake kikatiba, vyenginevyo linaweza kuwa Baraza butu lisilokuwa na makali yoyote”. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema mkutano wa Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola uliofanyika Zanzibar mnamo mwaka 2005 ulijadili nanma ya kuyajengea uwezo wa uhuru wa mambo ya kifedha Mabunge Wanachama ikiwemo Tanzania.

Alisema baadhi ya Mabunge yameanza kutekeleza maazimio ya mkutano huo ikiwemo Tanzania na Baraza la Wawakilishi Zanzibar liko katika hatua ya kutekeleza maazimio ya mkutano huo.

Akizungumzia kuhusu sensa ya Watu na Makazi, Balozi Seif aliwaomba Wawakilishi kuwa Mabalozi wa kufikisha taaluma kwa wananchi kuhusu umuhimu wa zoezi ya kuhesabiwa wakati utakapowadia.

Alisema kwa upande wa maandalizi ya kutenga maeneo ya kuhesabu watu ili kurahisisha kazi za kuhesabu watu Zanzibar imeshamaliza kwa wilaya zote 10 za Zanzibar.

Wakichangia mada ya rasimu ya mswada wa Mfuko wa Baraza la Wawakilishi baadhi ya Wawakilishi waliwashauri watendaji wa serikali kujenga utamaduni wa kuheshimu mihimili mitatu inayoendesha nchi.

Walisema rasimu hiyo haijakidhi hata kidogo matakwa yaliyokusudiwa na kueleza kuwa baadhi ya vipengele vya rasimu hiyo vinaashiria muelekeo wa mgongano kati ya Baraza la Wawakilshi na serikali.

Wawakilishi hao waliomba rasimu hiyo irejeshwe serikalini kwa maarekebisho zaidi ya msingi na si vibaya ukachelewa kupelekwa Barazani ili kupata wasaa wa marekebisho hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.