Habari za Punde

SHAMUHUNA ATAKA WANAHABARI KUJIELIMISHA ZAIDI

Haji Nassor, Na Nassra Khatib-MUM

WAZIRI wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Ali Juma Shamuhuna amewataka wahitimu wa chuo cha uandishi wa habari Zanzibar (ZJMMC) kutotosheka na kiwango cha elimu katika ngazi ya Cheti na Stashahada na badala yake kujiendeleza zaidi kielimu ili kuwa waandishi waliobobea katika
fani hiyo.

Waziri Shamuhuna alisema hayo katika mahafali ya tatu ya chuo hicho yaliyofanyika viwanja vya Wizara ya Habari,Utamaduni,Utalii,na Michezo Kikwanjuni mjinu Unguja mara baada ya kutunuku vyeti na stashahada
hizo kwa wahitmu 69.


Alisema kiwango cha elimu walichokipata ni cha kuanzia, hivyo safari iliopo mbele yao ni kuhakikisha wanajiendeleza katika vyuo mbali mbali ili kuhakikisha Zanzibar inakuwa na madaktari katika ngazi ya fani ya
uandishi wa habari.

“Katika hatua ya ngazi ya awali ni mwanzo mzuri walioupta lakini wasichoke kujiendeleza katika vyuo mbali mbali maana elimu kwa sasa imetanuka,”, alisisitiza Shamhuna.

Waziri Shamhuna alisema wahitimu hao ni kizazi kipya kwenye tasnia ya habari, hivyo wachukue juhudi katika kujiendeleza ili wafikie katika daraja za juu za uandishi na huo uwe mtazamo wao wa baadae .

Aidha alisisitiza kwa waandishi wa habari kujituma na kuzifanyia utafiti taarifa wanazoziandika au kuzitangaza ili kuhakikisha wanapata dondoo za kutosha kutoka katika vyanzo vya habari ili wasomaji wapate taarifa sahihi .

Nao wahitimu katika risala yao iliyosomwa na Omar Ahmed Mcheju walisema kuwa watazitumia kalamu zao kuelimisha katika mambo yenye manufaa pamoja na kufuata maadili yalioko katika jamii na hawatozitumia kalamu zao kwa kazi zinazokwenda kinyume na maadili kwani wanatambua kalamu ilivyo na ncha kali kuliko risasi.

Walisema licha ya kuwa wao wamehitimu lakini katika chuo hicho kuna changamoto nyingi ambazo zinakikabili chuo hicho ikiwemo upungufu wa vifaa vya kufundishi kama Komputer ,Camera ,vitabu pamoja na chuo kutokuwa na majengo ya kutosha, hivyo wameiomba serikali kuyatafutia ufumbuzi matatizo hayo ili wanafunzi wengine wajifunze kwa vitendo kwani taaluma ya habari inahitaji vitendo zaidi..

Katika hafla hiyo jumla ya wahitimu 69 walitunukiwa vyeti na stashahada ya uandishi ambapo arubaini na tano kati ya hao walitunukiwa vyeti na ishirini na nne stashahada

Pia katika hafla hiyo Salma Ameir alitunukiwa zawadi kwa kuwa mwanafunzi bora katika somo la Public Relation, Haji Nassor mwanafunzi mwenye nidhamu, Nafda Hindi mwanafunzi bora katika somo la
utangazaji, Juma Abdallah katika somo la uandishi wa habari za magazeti, na mwanafunzi Shaaban Juma Mnyika katika ngazi ya cheti amekuwa ni mwanafunzi bora wa jumla chuoni hapo kwa mwaka uliopita.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.