Habari za Punde

Ukata Wakwamisha Kombe la Mapinduzi Skwashi

Timu za Bara zarejea kwao  
Yasubiri kupangiwa tarehe mpya

Na Mwandishi Wetu

MICHUANO ya mpira wa ukutani (Squash) ya kutafuta mshindi wa miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar iIiyokuwa ianze Januari 13, 2012 kwenye ukumbi wa Polisi Ziwani, imeahirishwa hadi itakapotangazwa tena.

Katibu wa Chama cha Skwashi Zanzibar (ZSRA) Haji Uzia Vuai, amesema hatua hiyo imetokana na ukata wa fedha unaokikabili chama hicho, na Baraza la Michezo la Zanzibar kushindwa kutoa fedha za kuendeshea
michuano hiyo kama ilivyopangwa hapo kabla.


Vuai amesema baadhi ya washiriki kutoka Tanzania Bara walishaanza kuwasili Zanzibar tayari kwa mashindano hayo ambayo sasa yanasubiri kupangiwa tarehe nyengine, baada ya kupatikana kwa ruzuku hiyo
isiyozidi shingili milioni mbili.

Hata hivyo, Vuai ametoa wito kwa serikali na wadau wa michezo wenye uwezo kukisaidia chama chake ili kiweze kufanikisha michuano hiyo ambayo ipo kwenye ratiba ya sherehe za miaka 48 ya Mapinduzi ya
Zanzibar.

Awali Vuai alisema michuano hiyo ambayo imekuwa ikifanyika kila mwaka wakati wa sherehe za Mapinduzi, endapo ingefanyika kama ilivyokuwa imepangwa, ilitarajiwa kumalizika leo kwenye ukumbi wa hoteli ya
Bwawani mjini Zanzibar.

Alieleza kuwa, mshindi wa kwanza wa michuano hiyo ilipangwa apate shilingi laki mbili, wa pili 150,000 na shilingi 100,000 kwa mshindi wa tatu zawadi ambazo ziliahidiwa kutolewa na baraza la michezo la
Zanzibar.

Alipoulizwa, Katibu wa BTMZ Hassan Khairallah Tawakal, alikiri kupokea ombi la chama hicho la shlingi 1,400,000, lakini kutokana na upungufu wa fedha, baraza lake lilikubali kutoa shilingi milioni moja.

Hata hivyo, alisema viongozi wa Chama cha Skwashi walieleza kuwa, watachukua jukumu la kutafuta mkopo ili kukamilisha kiasi kinachohitajiwa, na kwamba ofisi yake inasubiri iijulishe tarehe watakayoamua kuanza mashindano hayo ili iwakabidhi fedha hizo.

Aidha alifafanyia kuwa, ombi hilo walilipata katika wakati mgumu, ambapo viongozi wa BTMZ walichelewa kukaa na kulifanyia upembuzi yakinifu ombi la chama hicho, kwa kuwa muda mwingi waliutumia
kushughulikia mashindano ya Kombe la Mapinduzi kwa mchezo wa soka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.