Wadau washauri nafasi itangazwe isitolewe kwa mahaba
Na Salum Vuai, Maelezo
WIKI kadhaa baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Mzee Zam Ali kuanza likizo ya kustaafu, baadhi ya wadau wa michezo wametoa rai juu ya njia ya kumpata katibu mpya wa chama hicho pamoja na vyama vyengine vya michezo.
Zam ameanza likizo hiyo tangu Januari 1, 2012, na hivyo kiti cha ukatibu wa ZFA kubaki wazi hadi sasa.
Baadhi ya wadau waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tafauti katika uwanja wa Amaan wakati wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi, wameshauri nafasi zote za ukatibu wa vyama vya michezo zitangazwe kwa ajili ya kuombwa kama inavyofanywa kwenye ajira nyengine.
Mkufunzi wa makocha Suleiman Mahmoud Jabir, amesema wakati umefika sasa wa kuacha utaratibu wa kuteua makatibu wa vyama vya michezo, na badala yake wizara husika itoe matangazo katika vyombo vya habari juu ya kuwepo nafasi hizo, ili watu wenye sifa waziombe.
Alisema uongozi wa vyama vya michezo si nafasi za kisiasa ambazo viongozi wake huteuliwa na serikali na kuwajibika kwazo, hivyo ni vyema kama zinatokezea nafasi zilizo wazi, zitangazwe ili kupata watendaji wenye sifa kielimu na uzoefu.
"Huu si wakati tena wa kupeana vyeo kama sadaka, hivyo ni vyema serikali iajiri kwa mfumo wa kutangaza nafasi na baadae waombaji wafanyiwe usaili, hii itasaidia kupata waombaji wenye sifa zinazokubalika na kuleta ushindani", alisisitiza Jabir aliyewahi kufundisha klabu kadhaa pamoja na timu ya taifa 'Zanzibar Heroes'.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu katika klabu ya Jamhuri ya Pemba Masanja Mabula, amesema kutumika kwa mfumo huo, kutawafanya wanaoajiriwa watimize majukumu yao bila ubabaishaji kwani watalazimika kufanya kazi kwa kuheshimu mikataba waliyosaini.
Naye Hashim Salum, Katibu wa klabu ya Miembeni United, amesema kwa kuwa ukatibu ni kazi inayohitaji taaluma, ni vyema itangaziwe kwani katika kuteua, mara nyingi mamlaka huangalia mapenzi na usahibu ilionao kwa wanaopewa nafasi hizo, jambo alilosema husababisha muhali pale muajiriwa anapokiuka miiko na maadili ya kazi zake.
No comments:
Post a Comment