Habari za Punde

Uzinduzi wa Bodi ya Chuo cha Kiislam Mazizini Zanzibar.

    
ND. MGENI RASMI WA UZINDUZI WA BODI YA CHUO CHA KIISLAM

Mhe Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali

Nd. Katibu Mkuu – (WEMA)

Nd. Naibu K/Mkuu – (WEMA)

Nd. Kamishna – (WEMA)

Nd. Mkurugenzi Mafunzo ya Ualimu

Wakurugenzi katika vitengo mbali mbali

Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kiislamu

Mkuu wa Chuo Cha Kiislamu

Mwalim Mkuu wa Sekondari ya Kiislamu

Nd. Wajumbe wa Bodi ya Chuo cha Kiislamu

Nd. Wakufunzi na wana chuo wa Chuo cha Kiislamu

Nd. Wageni Waalikwa.



ASSALAMU ALAYKUM WARAHMATULLAH WABARAKATUH

Awali ya yote tunatanguliza shukrani zetu za dhati kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu aliyeepukana na kila upungufu na Mfalme wa ulimwengu wote, kwa kutupa nguvu tukaweza kukutana hapa leo, kwa lengo la kuzindua bodi ya Chuo cha Kiislamu – Mazizini.

Kwa vile sherehe zetu tunazifanya katika eneo la Chuo, itakuwa vizuri sana tuelezee historia fupi ya Chuo cha Kiislamu.


HISTORIA FUPI YA CHUO

Chuo cha Kiislamu Mazizini kimefunguliwa rasmi tarehe Mosi April 1972 na Rais wa kwanza wa Zanzibar, marehemu Abeid Amani Karume. Ufunguzi huu ulitokana na fikra yake mwenyewe ya kuona kuna haja ya wananchi wa Zanzibar kuwa na Chuo chao cha Kiislamu.

Mwaka 1969 marehemu mzee Abeid Amani Karume, alichagua kamati ya wananchi kusimamia ujenzi huo. Alitoa eneo la Mazizini lenye ukubwa wa ekari 80 kwa ajili ya ujenzi.

Wananchi 21 waliochaguliwa kusimamia ujenzi wa chuo kwa niaba ya wenzao bila ya malipo yoyote ni:

1. Bw. Haji wa Haji - Mjini.

2. “ Muhammed Othman - K/Samaki.

3. “ Shaaban Zahran - Maungani.

4. Bw. Fadhil Mzee - Bweleo

5. “ Vuai Khamis - Jendele.

6. “ Fasihi Iddi - Mkokotoni.

7. “ Fasihi Ahmed - Dimani.

8. “ Mahmoud Juma - Kiboje.

9. “ Ali Rijali - Bambi.

10. “ Uzia Mohammed - Uroa.

11. “ Hassan Mwinyi - Kibuteni.

12. “ Abdalla Othman - Kizimkazi.

13. “ Nur Abdulqadir - Tunduni.

14. “ Foum Ame - Kinyasini.

15. Sh. Ameir Tajo (Mkubwa) - Mjini.

16. Bw. Zamani Haji - Donge.

17. “ Umbaya Vuai - Chwaka.

18. Sh. Mussa Makungu - Ndijani.

19. Bw. Yussuf Bira - Mjini.

20. “ Hussein Ramadhan - Mjini.

21. “ Suleiman Ali - Bwejuu.

Mnamo Oktoba 1971 kamati ya wananchi waliiomba Wizara ya Elimu kupitia waziri wake Mhe. Hassan Nassoro Moyo kusimamia mafunzo ya chuo baada ya kukamilika ujenzi wake.

Dhamira kuu ya Mzee Karume ilikuwa kukigeuza chuo hiki hapo baadae, kiwe Chuo Kikuu cha Kiislamu, kitakachojenga maadili mema ya vijana na kupata taaluma ya dini na maendeleo ya kidunia. Ndio maana mbali ya kuwa Chuo cha Kiislamu, lakini pia maabara za kisayansi zimejengwa. Kwa bahati mbaya lengo hilo halikufikiwa baada ya Mzee Karume kufariki dunia baada ya siku sita tu ya ufunguzi wa chuo.,, hapo terehe 7/04/1972.

Mwaka 1982, Rais wa awamu ya pili Mhe. Aboud Jumbe Mwinyi aliunda Taskforce (Kamati maalum) ya wajumbe 14 kwa lengo la kutathmini maendeleo ya Chuo cha Kiislamu na mafunzo ya kiislamu kwa ujumla.

Taskforce, hiyo iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wake Aboud Talib Aboud, iliundwa na wajumbe wafuatao:

1. Mhe. Waziri wa Elimu.

2. Mhe Kadhi Mkuu

3. Sh. Ameir Tajo (mdogo)

4. Sh. Mussa Makungu

5. Sh. Omar Zahran.

6. Sh. Ahmed Abdulrahim.

7. Sh. Ali Khatib Mranzi.

8. Sh. Juma Abdulwadood.

9. Sh. Hamza Ali.

10. Sh. Saleh Omar Kaab.

11. Sh. Abeid Marine.

12. Sh. Khamis Amour.

13. Sh. Faeisal S. Mbamba – ambae alikuwa ndiye Katibu.

Taskforce hiyo ilitoa ripoti ya mapendekezo mwaka 1983, Mapendekezo hayo yameeleza kwamba mfumo wa Chuo cha Kiislamu ubadilishwe na badala yake iundwe, Taasisi ya Mafunzo ya Kiislamu, itakayoundwa kisheria na kupewa uwezo kamili wa kuendesha shughuli zake. Kwa bahati mbaya ripoti ya Taskforce haikuwahi kufanyiwa kazi na Mhe. Rais Aboud Jumbe, kutokana na kuchafuka kwa hali ya kisiasa iliyopelekea Rais ajiuzulu mwaka mmoja baadae (yaani 1984).

Hata hivyo kampeni za Chuo cha Kiislamu kutakiwa kiwe Chuo Kikuu ni mtazamo wa viongozi wengi serikalini, na kwa wananchi kiujumla na ili jamii ya Wazanzibar ambao wengi wao ni waislamu, iweze kunufaika na chuo chao, kielimu kimaadili na kimaendeleo.

Chuo kilipoanzishwa mwaka 1972 kilikuwa na majengo mawili tu. Jengo la kwanza ni afisi ya utawala na staff ya walimu. Jengo la pili lilikuwa ni la Ghorofa moja lenye madarasa manne juu, na maabara mbili za sayansi chini. Lengo lilikuwa kujengwa, majengo mengine manne ya ghorofa baadae, lakini hali ya kifedha haikuruhusu kwa wakati huo.

Mwaka 1990 jengo jipya la madarasa ya diploma lilizinduliwa na mwaka moja baadae, kozi ya diploma ilianzishwa. Mnamo mwaka 1995 jengo lenye maktaba ya chuo lilikamilika na kuzinduliwa rasmi kwa matumizi. Mpaka kufikia hii leo tuna majengo matatu yenye madarasa 15 staff 3 za walimu, chumba cha komputa, maktaba pamoja na maabara mbili. Majengo hayo huwa yanatumika kwa shughuli za chuo pamoja na Sekondari ya mazizini.

Chuo cha kiislamu kinatoa mafunzo ya Ualimu ya ngazi ya Cheti mjumuisho

(Inclusive education), Diploma ya Elimu ya Sekondari (Necta), Diploma ya sekondari ya dini na kiarabu, na Diploma ya msingi . Chuo hivi sasa kina jumla ya wanafunzi 220, na wafanyakazi 75 kati yao wakufunzi 50 na wengine 14 wako masomoni.

Uongozi uliopo sasa unachukua juhudi kubwa ya kulilinda eneo la chuo, baada ya maeneo mengi kuchukuliwa na taasisi za serikali, na za watu binafsi na hata kuanzishwa makaazi ya watu binafsi. Chuo sasa kina ekari 40 tu. Idara ya upimaji tayari imekwisha lipima eneo lote na kuwekwa alama maalum (Becon), shs 650,000/-zimeshalipwa ili chuo kipate hati miliki ya eneo, lakini hadi leo bado haijapatikana na hii ni kwa sababu baadhi ya maeneo yametolewa kwa watu binafsi ambao mpaka hivi sasa yana utata .

Jambo la kufurahisha chuo, kimeshandaa michoro na eneo la ujenzi wa Hall la kimataifa, lenye uwezo wa kubeba watu 2000 litakalobeba juu yake madarsa 7 na chumba kimoja cha komputa, lakini mpaka hivi sasa hatujapata mfadhili wa uhakika katika ujenzi huo, tunaiomba wizara na watendaji wake tuwe pamoja katika kusaidiana na hilo.

Katika kuhakikisha Wakufunzi wanawajibika ipasavyo kwa kutekeleza wajibu na majukumu yao kikamilifu Chuo kimeanzisha Idara tano za mafunzo ya Ualimu (Sayansi/Sayansi Jamii/ Lugha/ Ualimu/ Elimu Mjimuisho).

Pamoja na Idara hizo tano, Chuo pia kimeanzisha Panel za masomo kama vile; Panel nne za Sayansi, Panel tatu za Lugha na Panel Sayansi Jamii.

Vile vile Chuo kimeanzisha Kamati mbali mbali za kusimamia shughuli za Chuo. Kamati hizo ni pamoja na:

1. Kamati ya Utawala na Fedha.

2. Kamati ya Usajili.

3. Kamati ya Taaluma.

4. Kamati ya Mitihani.

5. Serikali ya Wanachuo.

6. Kamati ya Takwimu.

7. Kamati ya Usafi wa Mazingira pamoja na Club ya Mazingira (Mees).

8. Kamati ya Michezo.

9. Kamati ya Ujenzi, Ukarabati na Samani.

10. Kamati ya Sherehe , Tafrija, harusi na Maafa.

11. Kamati ya Matunzo ya Wakati.

12. Kamati ya Usafiri.

13. Kamati ya Ushauri na Nasaha.

14. Kamati ya Vyeti.

15. Kamati ya Chumba cha Computer na ghala.

16. Kamati ya Da’wa.

17. Kamati ya B.T.P.

18. Kamati ya Maktaba.

19. Kamati ya Dakhalia.

UTEKELEZAJI WA MALENGO:

1. Uongozi unafuatilia kwa karibu kuona kuwa kila alopewa dhamana anaitekeleza kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa zaidi.

2. Njia kuu zote za uchumi na mapato zinasimamiwa kwa karibu na Uongozi wa chuo.

3. Uongozi unaagiza kwa watendaji wote kutoa risiti kwa shughuli zote zinazohusu utoaji na upokeaji wa fedha, ili kusudi kukwepa upotevu wa fedha.

4. Chuo kimeandaa Idara mbali mbali za masomo pamoja na Wakuu wa Kozi/Panel kwa lengo la kufanikisha malengo ya Taaluma Chuoni.

5. Chuo kinaendelea na upandaji wa miti ya matunda katika eneo la chuo, kama moja ya njia ya kulinda mazingira.

6. Chuo kimelifanyia ukarabati jengo la ofisi na baadae kinakusudia kufanya hivyo hivyo kwa majengo mengine pale uwezo wa kifedha utakaporuhusu.

HISTORIA YA BODI YA CHUO CHA KIISLAMU

Mhe Waziri wa Elimu, wajumbe wa bodi na wageni waalikwa, jambo kubwa lililotukusanya hapa ni uzinduzi wa bodi ya Chuo chetu, kwa muktadha huu itakuwa ni vizuri ikiwa tutasimulia historia fupi sana, ya Bodi ya Chuo cha Kiislamu.

Kwa mara ya kwanza Bodi ya Chuo ilianzishwa tarehe 19/06/1990. Kipindi hichi Mkuu wa Chuo alikuwa Marehemu Sh. Abdulrazak Othman Juma

(1986-2000).

Bodi hiyo iliundwa na wajumbe wanane.

Nd. Moh’d Kombo Maalim.

Nd. Bwanakheri Omar Hassan.

Mjumbe Jumuiya ya Wazazi Mkoa Mjini/Magharibi.

Mjumbe Jumuiya ya Wanawake Mkoa Mjini/Magharibi.

Mjumbe Jumuiya ya Vijana Mkoa Mjini/Magharibi.

Mjumbe Afisi ya Waziri Kiongozi.

Mjumbe Halmashauri Kuu ya Chama Wilaya M/Magharibi.

Mjumbe Halmashauri Kuu ya Chama Mkoa M/Magharibi.

Wajumbe hao walipatikana kwa mujibu wa sheria ya uanzishaji bodi ya vyuo ya mwaka 1992, na maelekezo ya wizara ya Elimu. Hata hivyo Bodi hiyo haikudumu kiutendaji.

Harakati za kuunda Bodi mpya zilianza mwaka 1994 na mwaka mmoja baadae (1995), Bodi iliundwa ikiwa na wajumbe tisa.

Nd. Hemed Said Al-Bahry – Mwenyekiti.

Nd. Abdulrazak Othman Juma – Katibu

Sh. Habib Al Kombo – CCK

Nd. Asha Mussa Ahmed.

Nd. Fadhil Pandu Pandu – Mwandishi CCK.

Mjumbe Baraza la Manispaa – Khatib Ali Khatib

Mjumbe Kamisheni ya Wakf na Mali ya Amana – Thabit Nouman Jongo.

Sheha wa shehia ya Kiembe samaki – Suleiman Moh’d

Mkuu wa serikali ya wanafunzi ya chuo - Mussa Ussi Sheha, na

nd. Khamis J. Othman – CCK.

Bodi hii iliweza kufuatilia matatizo mbali mbali yaliyokikabili chuo, kama vile tatizo la kufungwa ng’ombe eneo la chuo, ukosefu wa maji na tatizo la usafiri. Bodi ikatoa rai mbali mbali za kutatua matatizo hayo, kama vile kuchimbwa kisima, gari ilyoharibika ilitengenezwa na ng’ombe wanaokula mazao hukumu zao zilichukuliwa na polisi, ikawa ndio dawa tosha la tatizo hilo.

Licha ya mwanzo mzuri wa utendaji kazi wa Bodi hii, lakini hatima yake ilififia na kutoweka.

Hata hivyo, haja ya kuwepo kwa Bodi chuoni lilikuwa ndio lengo kuu kwa wakuu wote waliofuatia baadae. Tunashukuru sana kufikia siku ya leo Jumanne ya tarehe 31 januari 2012, Bodi ya chuo inazinduliwa rasmi baada ya kupita takriban miaka 20.

Tunachukua nafasi hii kukupongeza Mhe. Waziri kwa niaba ya wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kuchukua juhudi kubwa na za maksudi ya kufanikisha kusimama kwa Bodi hii. Aidha, mategemeo yetu ni kwamba pande mbili hizi yaani wizara yetu na Bodi ya chuo zitafanya kazi kwa karibu kufanikisha malengo na maendeleo ya chuo, ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na waasisi wa chuo na wazee wetu kwa ujumla.

Kwa mnasaha huo, chuo kina azma ya kuandaa Tamasha la miaka 40 ya chuo tangu kuanzishwa kwake, ifikapo Mei mwaka huu. Na lengo kuu la sherehe hiyo ni kuzingatia yafuatayo:

1. Kupiga harambee kwa kuomba msaada wa jengo lililotajwa hapo juu (hall la Kimataifa) na majengo mengineo.

2. Kuboresha maendeleo ya chuo kufikia lengo la serikali la kuwa chuo kikuu.

3. Kupatiwa fursa za masomo ya elimu kwa wakufunzi na wanafunzi.

4. Kuendeleza huduma za maktaba na maabara.

5. Kutatua kabisa tatizo la usafiri chuoni kwa kununua mabasi mapya na kuzifanyia matengenezo gari zilizopo.

6. Kuhakikisha kwamba mandhari na mazingira ya chuo yanalindwa, kwa kuzunguushia uzio eneo lote la chuo lililobaki ili kuepushwa kuvamiwa tena, na maeneo yaliyotolewa kwa taasisi nyengine ambayo hayajajengwa kurejeshewa kuwa ni miliki ya chuo kama ilivyokuwa mwanzo.

7. Kuhakikisha kwamba wakufunzi wanapata makaazi ya nyumba zilizo karibu na chuo ili kuleta ufanisi wa utendaji kazi.

8. Kukarabati majengo na kujenga ukumbi wa mitihani, maktaba na mikutano.

9. Kusimamia nidhamu na maadili ya wanachuo kwa lengo la kuleta ufanisi katika tabia, silka na utamaduni wa mzanzibari.

10. Kuhakikisha wanachuo takriban wote wawe wanaishi dakhalia.

11. Kuhakikisha kwamba vifaa muhimu vya ufundishaji na kujifunza vinapatikana chuoni (teaching and learning materials).

12. Kuhakikisha kwamba komputa zinatosheleza kwa ajili ya mafunzo ya wanachuo.

13. Kuzalisha walimu na wataalamu wa mambo ya dini watakaostahiki kufanyakazi katika maeneo mbali mbali, kama vile mahkama ya kazi afisi ya wakfu na mali ya amana na ofisi ya mufti.

14. Kukuza fani za kisayansi na fani nyenginezo za dini na dunia kwa ajili ya maendeleo ya kila nyanja za mwanadamu katika maisha yake.

Tunaomba mashirikiano katika kulifanikisha jambo hili la kheri, na Allah atuwakishe katika utendaji wa mipango hiyo. Amiin.

Mwisho tunatoa shukurani za dhati kwa wizara kuanzia Mkurugenzi wetu hasa katika kufuatilia umoja wa utendaji wa vyuo vya Ualimu CCK Mazizini , Benjamin Mkapa na CCK Kiuyu Pemba kuwa na mashirikiano mazuri ya kufanikisha kupasisha wanafunzi.

Pili shukurani kwa Naibu Katibu Mkuu aliefuatilia kwa kina kupata msaada wa Omani katika majenzi ambao tunamuomba Allah atufanikishie.

Shukurani pia kwa Katibu Mkuu ambae alijitahidi kuhakikisha baadhi ya msaada wetu wa kasma unatufikia na ndio sababu ya kuboresha ukarabati wa majengo yetu.

Mwisho shukurani zije kwako Mhe Waziri, ambae ndie mgeni rasmi, wa uzinduzi wa bodi hii, na ambae umehakikisha kwa nguvu zote uzinduzi huu unafanikiwa kwa siku ya leo, pili kutukubalia kuhudhuria hafla ya uzinduzi huu wewe binafsi na imekuwa ndio fursa ya kwanza kuja kututembelea na kutusikiliza mahitaji yetu, hali ya kwamba una shughuli nyingi za kiwizara na kitaifa.

WABILAHI – TAWFIQ

AHSNTENI KWA KUNISIKILIZA

4 comments:

  1. Mimi ni mmoja wa matunda ya chuo hiki nilikuwepo hapo kati ya 1979 - 1982.

    Kinachonifurahisha ni kuona mafanikio ya chuo hiki kitaaluma kwani kimeweza kutoa Wasomi wengi ambao wapo kwenye medani tofauti za kielimu na utawala wengine kufikia daraja za udaktari.

    Kinachonisikitisha ni kuona jinsi Chuo hiki kilivyotupwa na kutoendelezwa na hata yale Malengo ya muda mrefu ya kuwa Chuo Kikuu cha Kiislamu kutotimizwa mpaka kufikia kufutwa na Wizara husika.

    Katika Ulimwengu wa leo wa utandawazi chuo kina nafasi nzuri sana ya kutafuta njia za kujinasa kutoka katika kutegemea ruzuku ya serikali kujiendeleza na kubuni njia tofauti za kimapato.

    Pia kuwepo na Uongozi uliokuwa na upeo wa kwenda na wakati kwa kuweza kukiunganisha chuo na vyuo yengine tofauti Ulimwenguni ambapo wataweza kubadilishana mambo mengi muhimu kitaaluma na hata Wataalamu na misaada mengine mengi tu kama uongozi utakuwa tayari kuchacharika.

    ReplyDelete
  2. Ndugu yangu unayoyasema ni kweli, lakini hayo, yanataka viongozi wenye kuona mbali, sio sisi.
    Sisi tumeamua kuishi kwa majuto.

    ReplyDelete
  3. kuna haja ya kuazisha program za didni zaidi ili chuo kipate mapato na kiwe na wahitimu wengi zaidi. uongozi uangalie namna ya kuazisha program hizo

    ReplyDelete
  4. Mashallah Allah akikuze chuo cha kiislm u iliwatotowetu wapatefursa yakusoma mabo mengi yakiwemo yadini nadunia natamani kiwechuo kikuu kitoe degree master nahata PHD na ptofesser.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.