Na Mwashamba Juma
WAZIRI wa Afya, Juma Duni Haji amesema zaidi ya wananchi 10,000 hapa Zanzibar wanakabiliwa na matatizo ya macho yanayosababishwa na mtoto wa jicho pamoja na ugonjwa wa glaucoma.
Waziri huyo alieleza hayo jana katika hospitali ya Bububu, kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa kambi ya matibabu ya macho ambapo matakatari wa JWTZ watashirikiana na wale wa Marekani.
Waziri Duni alisema magonjwa ya macho yamekuwa yakiongezea katika jamii hali inayoongeza idadi ya wananchi wengi kuwa vipofu.
Alisema kupigwa kwa kambi hiyo kutasaidia kwa kiasi kukibwa wananchi wa Zanzibar kuepukana na matatizo ya macho hasa ikizingatiwa kuwa kitengo cha macho katika hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja hakijitoshelezi kutokana na wingi wa watu.
Waziri huyo alisema hivi sasa wananchi wa mijini na vijijini wamekuwa na mahitaji makubwa ya kupatiwa huduma za macho kutokana na kuongezea kwa magonjwa yanayosababishwa na sababu mbali mbali.
Katika kambi hiyo zaidi ya watu 1636 wanatarajiwa kupatiwa matibabu ya macho huko kwenye kambi ya matibabu ya macho katika hospitali ya jeshi Bububu ambapo jumla ya watu 102 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji na watu 982 wanategemewa kupatiwa miwani.
Aidha waziri huyo aliushukusru Ubalozi wa Marekani kwa kukubali kwao na kujitolea kutuma wataalamu na madaktari bingwa pamoja na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa Zanzibar, jambo ambalo linaimarisha na kudumisha udugu uliopo baina ya Zanzibar na Marekani.
Wakati huohuo aliushukuru uongozi wa hospitali ya jeshi ya Bububu kwa kukubali kwao kuwekwa kambi hiyo hospitalini hapo.
Nae Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso Lenhardt alisema ufunguzi wa kambi ya matibabu ya macho umefanikisha mashirikiano baina ya watu wa Marekani, wizara Afya ya Zanzibar pamoja na Jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania, katika kudhibiti magonjwa sugu ya macho.
Awali mkuu wa hospitali hiyo Bregedia Jenerali, Adam Mwabulanga alisema zoezi hilo limewashirikisha ufadhili wa Marekani, wakiwemo jeshi la Marekani kupitia AFRICOM, Jeshi la Tanzania katika huduma za afya ambao ni wenyeji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya.
Bregedia Mwabulanga alisema zoezi hilo ambalo limewashirikisha wataalamu 20 kutoka Marekani wakiwemo madaktari bingwa sita wa upasuaji wa mtoto wa jicho, wauguzi watano, nesi watano pamoja na utawala wanne.

No comments:
Post a Comment