Habari za Punde

RC Ataka Wadaiwa Sugu Nyumba za Serikali Wachukuliwe Hatua

Na Masanja Mabula, Pemba

MKUU wa mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi ameiagiza Idara ya Nyumba na Makaazi mkoani humo kufuatilia madeni ya wapangaji wa nyumba za serikali na kuwachukulia hatua wadaiwa sugu.

Akizungumza na watendaji wa Idara hiyo wakiongozwa na Ofisa Mdhamini Wizara ya Ardhi, Makaazi , Maji na Nishati Pemba Hemed Salim, uongozi wa Baraza la Mji na wapangaji wa nyumba hizo, aliitaka Idara hiyo kufanyakazi zake kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.


Alisema serikali ya mkoa imebaini kuwepo na wapangaji ambao wameshindwa kulipa kodi za nyumba kwa kipindi kirefu huku baadhi ya nyumba za wapangaji wamepangishana (sublet), jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa sheria.

Kufuatia kuwepo na vitendo hivyo, mkuu huyo alitoa muda wa miezi mitatu kwa Idara ya Nyumba na Makaazi kuwafukuza katika nyumba za serikali wananchi wanaoishi katika nyumba hizo bila ya kuwa na mikataba halali ili kutoa fursa kwa wananchi wengine kuweza kukodishwa.

Aidha alieleza kuwa baadhi ya nyumba hizo, wapangaji wameshahama na kuwarithisha nyumba jamaa zao, na kwamba aliiagiza Idara kuzifuatilia nyumba hizo na kisha kuzifunga wakati mipango ya kuwakodisha watu wengine ikifanywa.

“Zipo nyumba ambazo wapangaji walio na mkataba wameshahama na kuhamia sehemu nyingine, naiomba Idara izifunge mara moja wakati mipango ya kuwapatia watu wengine inafanywa”, alisema Dadi.

Kwa upande wake Ofisa Mdhamini wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Pemba, Hemed Salim alisema wizara imejipanga kufanya ukaguzi wa nyumba zake ili kujua wapangaji halali pamoja na wadaiwa sugu.

“Tumeandaa utaratibu wa kufanya ukaguzi kila mwezi ili kuja wapangaji wenye mikataba halali, jambo hilo litatuwezesha kuwabaini wananchi wanaoishi kwenye nyumba bila ya kuwa na mikataba”, alisema.

Alisema zoezi hilo limeanza katika nyumba za serikali zilizoko Kengeja na kwamba kwa sasa wanajiandaa kufanya ukaguzi kwenye nyumba zilizoko wilaya ya Wete, Micheweni na Chake Chake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.