ZAIDI ya shilingi milioni 300 zimetengwa na mradi wa HIMA kwa ajili ya usimamizi wa biashara ya Hewa ukaa kwa madhumuni ya kupunguza uharibifu wa misitu nchini.
Fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya kujaribu biashara ya Hewa Ukaa ,mradi ambao unatarajiwa kuanza mwezi wa Machi mwaka huu baaada ya kupatikana chombo au taasisi itakayoweza kusimamia kazi.
Akizungumza katika warsha ya kujadili usimamizi wa biashara ya Hewa ukaa ofisa wa shirika la Care Tanzania, Soud Mohammed Juma alisema hatua hiyo imekuja kufuatia mkutano wa umoja wa mataifa uliofanyika Denmark uliojadili biashara ya hewa ukaa uliopitisha mpango wa kupunguza uharibifu wa misitu (REDD).
Alisema fedha hizo zitagaiwa kwa vikundi 40 vya uhifadhi ya misitu ya jamii vya Unguja na Pemba, ambapo mgao huo utategemea ukubwa na uzuri wa msitu pamoja na juhudi za wanajamii katika kijiji husika.
Alisema biashara hiyo ni ya wanajamii, hivyo ni vyema ikatafutwa taasisi itakayoweza kuviunganisha vikundi hivyo pamoja ili kuisimamia biashara hiyo ambayo ina gharama kubwa na kikudi kimoja kimoja hakitoweza kufanikiwa endapo kitafanya kazi hiyo peke yake kutokana na gharama hizo.
Alisema kutokana na utafiti uliofanywa na wataalamu mbali mbali unaonesha kuwa biashara hii itagharimu si chini ya dolla 10,000 kutafuta soko, hivyo kikundi kimoja pekee hakitoweza kumudu gharama hizo kutokana na hali za maisha zilivyokuwa ngumu.
Mapema Mkurugenzi wa idara ya Misitu na mali asili zisizorejesheka, Sheha Idrissa Hamdan aliwataka washiriki wa warsha hiyo kutoa mawazo yao kwa uwazi ili kupata chombo bora kitakachosimamia biashara ya hewa Ukaa kwa ajili ya kupunguza uharibifu wa misitu.
Alisema wakati dunia ikiwa mbioni kupunguza ongezeko la hewa chafu duniani zinazopelekea kuongezeka kwa joto, Zanzibar chini ya mradi wa HIMA imefanya warsha hiyo ili kujadili chombo kitakachosimamia biashara ya hewa ukaa ili kuunga mkono juhudi hizo.
Pia walikubaliana kuwashirikisha wanajamii wanaohusika na uhifadhi wa misitu na wao kujadili na kutowa mawazo yao juu ya upatikanaji wa taasisi hiyo.

No comments:
Post a Comment