Habari za Punde

Boti za Doria za Polisi Kuzinduliwa

Na Ramadhan Makame

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha anatarajiwa kuzindua rasmi boti mbili zitakazotumiwa na jeshi la polisi kwa ajili ya doria baharini.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Kamishna wa polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema hafla hiyo itafanyika leo katika Bandari ya Malindi mjini Zanzibar.

Alisema jeshi hilo limepatiwa msaada wa boti hizo za kisasa kutoka Marekani ambapo alisema zitaongeza ulinzi wa baharini pamoja na kupunguza uhalifu.

“Hizi ni boti za kisasa, zilizokamilika kuwa na vifaa kama rada vitakavyosaidia kwenye ulinzi baharini”,alisema Kamishna Mussa.


Aidha alisema msaada wa boti hizo umekuja wakati muafaka hasa ikizingatiwa bahari imekuwa ikitumiwa kwa masula mbali ya kiuhalifu.

Kamishna huyo alisema miongoni mwa changamoto ambazo zinaweza kupatiwa ufumbuzi kutokana na uwepo wa boti hizo ni pamoja na suala zima la uharamia baharini ambapo mara kadhaa kumekuwa na tishio hilo.

Aidha alisema kuwa tatizo jengine ambalo linaweza kupatiwa ufumbuzi ni pamoja na magendo ya mafuta hasa diseli, karafuu, uvuvi haramu, pamoja na majambazi wa mahoteli.

“Ni nafasi ya wananchi kutupatia taarifa za wahalifu wanaotumia bahari ili kujiandaa kukabiliana nao”,alisema Kamishna huyo.

Katika hafla ya uzinduzi wa boti hizo ziendazo kasi, pia Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspekta Jenerali Said Mwema na Balozi wa Marekani nchini Tanzani watahudhuria.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.