Habari za Punde

Shehia 13 Kunufaika na Mradi wa UKIMWI

Na Masanja Mabula, Pemba

JUMLA ya shehiya 13 katika Mkoa wa Kaskazini Pemba zitanufaika na mradi wa mapambano dhidi ya UKIMWI unaoendeshwa na Shirika la Engender Health kupitia mradi wa Champion unofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Misaada la Watu wa Marekani .

Shehiya hizo ni zile zilizopitiwa na mradi wa ujenzi wa barabara tano za mkoa huo zinazojengwa na Mfuko wa Changamoto ya Millenium Tanzania ,MCAT .


Akizindua mradi huo Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Dadi Faki Dadi aliwataka watendaji wa mradi huo kuondoa muhali wakati wa utekelezaji wake, na kulizungumzia tatizo la Ukimwi kama lilivyo .

“Ondoeni muhali wakati wa utekelezaji wa mradi huu , lizungumzieni tatizo la Ukimwi na athari zake kwa taifa kama lilivyo , huu sio wakati wa kuoneana haya kwani hili ni janga la kitaifa”, alisema Dadi .

Alisema kuwa katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kila mwananchi anapaswa kushiriki kikamilifu kwa kutoa misaada na michango ya hali na mali ili kuzuia maambukizi mapya kwa jamii .

Alisema tatizo la Ukimwi limekuwa likiathiri sekta mbali mbali za maendeleo , hivyo kupitia mradi huo wananchi waliowengi hasa wa vijijini watapata elimu ya kujikinga na maambukizi mapya na kufanya Taifa kuwa na watu wenye afya njema .

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa alisisitiza haja kwa jamii kuwa na utaratibu wa kupima mara kwa mara ili kujua afya zao jambo ambalo litawafanya waendeshe shughuli za maendeleo huku wakijua usalama wa afya zao .

Naye ofisa Mipango wa Mradi wa Champion Dk. Andrew William alisema kuwa lengo la kuanziasha Mradi huo ni kusaidia upatikanaji wa elimu ya kujikinga na maambukizi ya VVU kwa wananchi wa shehiya 13 katika Wilaya ya Wete na Micheweni.

Alisema kuwa uamuzi huo umekuja kufuatia kuwepo na mwingiliano wa watu kutoka sehemu mbali mbali ambao wanafanya kazi za ujenzi wa barabara hizo , na kwamba endapo elimu ya Ukimwi itawafikia na mapema wataweza kujikinga na maambukizi mapya .

Aidha alifahamisha kuwa mbali na kuwanufaisha wananchi wa shehiya 13 , pia mradi huo utakuwa na uwezo wa kutoa elimu ya Ukimwi kwa wananchi ambao sio wakaazi wa shehiya hizo kwani tatizo la ukimwi linamgusa kila mmoja .

Katika uzinduzi wa mradi huo uliwashirikisha wajumbe wa kamati za Ukimwi za Wilaya ya Wete na Micheweni pamoja na wadau wengine wa mapambano ya Ukimwi wakiwemo wajumbe kutoka Tume ya Ukimwi ZAC Kisiwani Pemba ..

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.