Habari za Punde

Balozi Seif Mgeni Rasmi Maulid ya Madrasatul Jabal Hira Wete, Pemba

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikabidhi mchango wa Shilingi 1,000,000/- kwa Mwalimu wa Madrasatul Jabal Hira ya Utaani Wete Ustaadhi Khamis Hamad Faki kwa ajili ya kusadia uendelezaji wa Madrasa hiyo.
Waumini mbali mbali wa Dini ya Kiislamu wakimsalia Mtume Muhammad { SAW } katika hafla ya Maulidi ya Uzawa wa Kiongozi huyo iliyoandaliwa na Madrasatul Jabal Hira iliyopo Mtaa WA Utaani Wete Pemba ambapo Mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Baadhi ya Viongozi wa Madrasatul Jabal Hira ya Utaani Wete Pemba ambapo alikuwa Mgeni rasmi katika Maulidi ya Chuo hicho kutukuza Uzawa wa Mtume Muhammad { SAW }.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddiamesema huu ni wakati muwafaka kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu kujitathmini kutokana na matendo yao iwapo yanaendaje na mwenendo mzima wa Kiongozi wao Mtume Muhammad {SAW} katika kumcha vyema Mwenyezi Muungu.

Balozi Seif ametoa kauli hiyo wakati wa sherehe za Maulidi ya Uzawa wa Mtume Muhammad { SAW } yaliyoandaliwa na Al Madrasat Jabal Hira iliyopo Mtaa wa Utaani Wete Pemba.


Alisema Imani na Nafsi miongoni mwa Waumini hivi sasa zinaonekana kubadilika kabisa nah ii ni kwenda kinyume na mwenendo wa Kiongozi wa Dini hii Mtume Muhammad { SAW }.

Balozi Seif aliitahadharisha Jamii kujikita zaidi katika matumizi bora ya ulimi ambao kwa kiasi kikubwa ndio chanzo kinachopelekea kusambaa kwa migogoro ndani ya Familia na Jamii kwa jumla..

Alisisitiza suala la Waislamu kuendelea kusaidia miongoni mwao kwa lengo la kuongeza mapenzi kati yao na Jamii inayowazunguuka.

“Tuko wangapi wenye tabia ya kusaidia wenzetu wakati wanapopatwa na matatizo na pale wanapofaulu tukafurahi nao pamoja”. Alihoji Balozi Seif.

Akizungumzia suala la malezi bora kwa watoto makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Jamii hivi sasa imekuwa na Mapenzi makubwa kwa Watoto wao na kupelekea upungufu wa Maadili.

Alisema tabia hiyo imeza Watoto wengi wasiokuwa na Heshima na matokeo yake nidhamu imeanza kupotea jambo ambalo ni janga katika siku chache zijazo.

Kuhusu Mchakato wa Katiba Mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Seif aliwaasa Baadhi ya Watu hasa Waumini wa Dini ya Kiislamu kuwepuka kutumia Misikiti katika kupotosha Watu kwenye suala hilo zito.

Aliwashauri Waumini wote wayakatae mawazo hayo ambayo yana nia ya kutaka kuutendanisha umma ambao tayari umeshachanganya kizazi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alichangia Jumla ya Shilingi Milioni Moja {1,000,000/- } kwa ajili ya kuendeleza Madrasa hiyo na kusisitiza kwamba ataangalia zaidi kuona njia ya kusaidia kutanzua matatizo yanayoikabili Madrasa hiyo ya Jabal Hira.

Katika Risala yao Wanafunzi hao wamesema pamoja na jitihada wanazochukuwa lakini bado wamekuwa wakipambana na changamoto kadhaa ikiwemo uhaba wa Misahafu, Vitabu pamoja na baadhi ya vifaa unaopelekea kupunguza harakati zao za kielimu Chuoni hapo.

Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Dadi Faki Dadi akimkaribisha Balozi Seif alikumbusha umuhimu wa kuendelezwa uvumilivu miongoni mwa Waumini ambao ndio utakaoleta kufaulu vyema katika matendo yao.

Mh. Dadi alisema kibri, dharau na hata majigambo yanazoweza kufanywa na baadhi ya Watu hasa Viongozi husababisha ukosefu wa amani na Utulivu matokeo yake kuleta mtafaruki katika Jamii.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.