HOTUBA YA MHESHIMIWA KAIMU WAZIRI WA USTAWI WA JAMII MAENDELEO YA VIJANA WANAWAKE NA WATOTO MHESHIMIWA ALI JUMA SHAMUHUNA KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI 2012
NDUGU WANANCHI,
Assalaam Alaykum Warahmatullahi Taala Wabarakatuh.
Kwanza kabisa nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu (SW) kwa kutujaalia afya njema na kuweza kuwepo hapa leo tukiwa katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani.
Kama inavyoeleweka kwamba tarehe 8 Machi ya kila mwaka ni siku ya wanawake Duniani, ambapo takriban Mataifa yote ulimwenguni huadhimisha siku
hii kwa kufanya shughuli mbali mbali. Huu ni mwaka wa 37 tokea siku hii kuasisiwa na Umoja wa Mataifa kuwa ni siku ya kimataifa ya Wanawake. Kwa hapa kwetu Zanzibar siku hii imeanza kuadhimishwa tokea mwaka 1991 ikiwa ni mwaka wa 21 sasa.
NDUGU WANANCHI
Chimbuko la siku hii ya kimataifa limetokana na harakati za wafanyakazi wa viwanda katika karne ya 19 huko Amerika ya kaskazini na Ulaya ambapo mwaka 1908 wafanyakazi wanawake waliandamana huko Marekani kupinga uonevu waliokuwa wakifanyiwa na waajiri wao. Hii ilifuatiwa na migomo na maandamano ya wanawake yaliofanyika katika nchi mbalimbali duniani kwa
lengo la kudai haki zao za msingi. Ambapo mnamo mwaka 1977 umoja wa mataifa ilitangaza rasmi siku ya tarehe 8 march ya kila mwaka kua ni siku ya wke duniani.
NDUGU WANANCHI
Lengo la maadhimisho ya siku hii ni kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kubaini changamoto katika kufikia haki na maendeleo ya wanawake katika Nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa, ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya kuimarisha hali na ustawi wa wanawake na jamii kwa ujumla.
NDUGU WANANCHI
Ujumbe wa mwaka huu 2012 wa Siku ya Wanawake Duniani ni: ONDOA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE TANZANIA. Ujumbe huu umekuja
wakati muwafaka ambapo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia taasisi husika imekuwa ikichukuwa juhudi za makusudi katika kuondoa vitendo vya udhalilishaji na ukatili dhidi ya wanawake.
NDUGU WANANCHI
Tunapozungumzia ukatili dhidi ya wanawake tuna maana kwamba ni vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa wanawake katika nyanja zote za maisha yaani kiuchumi, kijamii, kisiasa na kifamilia ambapo wanawake wamekuwa wakitelekezwa,kudharauliwa, wakidhulumiwa mali zao, kubakwa kwa watoto wa kike na kupigwa bila ya hatia. Kwa mujibu wa taarifa zilizopokelewa na Wizara ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto kwa mwaka 2010/2011 imepokea jumla ya malalamiko 144. Malalamiko 114
kwa upande wa Unguja na malalamiko 30 kwa upande wa Pemba. Malalamiko hayo yanayohusiana na udhalilishaji wa wanawake yamechukuliwa hatua zinazofaa kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya sheria.
NDUGU WANANCHI
Vitendo vvya ukatili dhidi ya wanawake vinapelekea athari za kimwili, kiakili na kisaikologia,.
Miongoni mwa athari za vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake ni maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa wanawake. Wakati kiwango cha Ukimwi katika jamii ni asilimia 0.6 ikiwa na maana kwamba takriban watu 7,200 wanaishi na VVU Zanzibar. Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi miongoni mwa wanawake ni
asilimia 0.7 na miongoni mwa wanaume ni asilimia 0.5. Kwa ujumla kwa kila mwanamme mmoja aliyepata maambukizo kuna wanawake watatu zaidi waliombukizwa. Hali hii inaonesha kwamba bado kuna mienendo na tabia ndani ya jamii zinazomfanya mwanamke kuwa katika hatari zaidi ya maambukizo kuliko mwanaume.
NDUGU WANANCHI
Vitendo hivi ni kinyume na haki za kibinaadamu na sheria zetu za nchi, hivyo
Katika kuhakikisha kwamba vitendo vya udhalilishaji na ukatili dhidi ya wanawake vinapungua na kuondoka kabisa. Wizara ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto
imekuwa ikichukua hatua mbalimbali . Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na: –
• Kuweka Sera, Sheria na Miongozo:
Kwanza kabisa Wizara ilifanya tafiti mbali mbali zilizotathmini hali ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, kuchambua na kubaini mapungufu Katika sheria zilizopo nchini, pamoja na mapungufu ya kiuwezo kwa taasisi zinazotoa huduma dhidi ya vitendo vya udhalilishaji visiwani.
Kufuatia tafiti hizi Wizara ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto imetayarisha Mpango wa Utekelezaji dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, ambao utekelezaji wake unahusisha wadau wote. Lengo la
mpango huu ni kuongoza na kuunganisha jitihada za kupiga vita vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.
Pia Serikali kwa kutambua athari ya vitendo vya udhalilishaji wa Wanawake na Watoto katika kufikia malengo ya Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA), mikakati madhubuti imewekwa katika mpango huo ili kudhibiti vitendo vya udhalilishaji.
Aidha, Mnamo mwezi March 2011 Sheria ya mtoto ilipitishwa ambayo ilizingatia upatikanaji wa Haki, Fursa na Ulinzi wa Watoto wakiwemo watoto wa Kike kupitia taasisi husika na jamii kwa jumla.
Katika kuhakikisha kwamba zipo sheria madhubuti dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa jinsia, Wizara
kwa kushirikiana na wadau wengine imo katika hatua za kuzifanyia marekebisho sheria mbali mbali za nchi ambazo zilibainika kuwa na mapungufu ikiwemo Sheria ya Mahakama ya Kadhi ya 1985.
Kuweka miundo na kuzijengea uwezo tasisi zinazoshughulikia na kupiga vita vitendo vya Udhalilishaji:
Wizara ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto ilisimamia uanzishaji wa kamati ya kitaifa ya kuratibu shughuli dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ambayo imezinduliwa mwezi wa Oktoba 2011. Kamati hii inajumuisha wajumbe kutoka Wizara ya Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto, Wizara ya Afya, Mahkama, Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu, na Wizara inayoshughulikia masuala ya Katiba.
Pia katika ngazi za Mikoa , Wilaya na Shehia kamati maalim zimeanzishwa za kushughulikia vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia. Kamati hizi zimepewa mafunzo ya kuziwezesha kufanya shughuli zake kwa ufanisi.
Hatua nyengine muhimu ni Kuanzishwa kwa kituo cha mkono kwa mkono (one stop center) hapo Hospitali ya mnazimmoja tarehe 26/5/ 2011, kituo hiki kinahudumia waathirika wa udhalilishwaji wa kijinsia na kuhakikisha kwamba haki inatendeka kwa waathirika wa vitendo hivyo na wahusika wa vitendo hivyo kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria. Aidha taratibu zinafanywa kuanzishwa kwa kituo kama hiki huko Kiswani Pemba. Ili kuhakikisha kuawaathirika wa vitendo vya udhalilishaji wanapata huduma iliyo bora katika vituo bali mbali, hivi sasa Wizara ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana Wanawakle na Watoto imo katika hatua ya kukamilisha muongozo wa watoa huduma katika vituo hivyo.
• Kuelimisha na kuhamasisha jamii:
Katika kupiga vita vitendo vya udhalilishaji, Wizara ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto inaendelea kuchukua hatua ya kuielimisha jamii juu ya athari za vitendo vya udhalilishaji, sheria na taratibu zilizopo pamoja na kuihamasisha jamii ili waweze kushiriki katika vita
dhidi ya vitendo hivyo. Hatua hii imechangia kuwepo kwa muamko pamoja uanzishwaji wa kamati za Shehia zinazoshughulikia vitendo vya udhalilishaji.
NDUGU WANANCHI
Pamoja na juhudi hizi bado tunachangamoto kubwa ya kuhakikisha watuhumiwa wanatiwa hatiani hususan wa vitendo vya ubakaji. Hivyo napenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa taasisi za Serikali na zisizokuwa za Serikali zinazoshughulikia masuala ya wanawake, Watoto na jamii kwa ujumla kuufanyia kazi ujumbe huu kivitendo na kuhakikisha kwamba masuala ya udhalilishaji wa wanawake yanaondoka kabisa Visiwani hapa na Tanzania kwa jumla.
NDUGU WANANCHI
Kwa kumalizia ninawaomba sote kwa pamoja tushirikiane katika kupambana na tatizo hili la unyanyasaji wa wanawake ili kujenga jamii yenye usawa na kuheshimu Haki ya kila mmoja wetu.
Sote kwa pamoja kuanzia sasa tuseme kuwa vitendo vya udhalilishaji wa wanawake sasa basi.
AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA
No comments:
Post a Comment