HOTUBA YA MGENI RASMI WAZIRI WA MIUNDOMBINU NA MAWASILIANO (SMZ) MHE. HAMAD MASOUD
KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA HALI
YA HEWA DUNIANI
TAREHE 23 MACHI 2012
Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Zanzibar
Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kutoka Zanzibar
Mkurugenzi – Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya Zanzibar
Meneja – Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar
Meneja – TCAA ZANZIBAR
Walimu na wanafunzi wote mlioalikwa
Wageni waalikwa
Mabibi na Mabwana,
ASALAAM ALAIKUM
Awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake kwa kutujaalia uhai na uzima na kutuwezesha kukutana hapa leo kusherehekea Siku ya Hali ya Hewa Duniani.
Aidha, napenda nichukue fursa hii kwa niaba yangu na kwa niaba ya Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwashukuru watendaji wakuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya Zanzibar kwa kunialika katika hafla hii kuwa Mgeni Rasmi. Siku hii ni adhimu kwetu sote na ndio maana tumeadhimia kuisherehekea hii leo.
Wageni waalikwa, mabibi na mabwana,
Kila mwaka, ifikapo tarehe 23 Machi, Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Jumuia ya Kimataifa ya Hali ya Hewa huunganisha juhudi zao kusherehekea SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI, ili kuadhimisha kuasisiwa kwa shirika hilo katika mwaka 1950 kufuatia makubaliano ambayo Shirika la Hali ya Hewa Duniani lilichukua majukumu ya kabla ya Shirika la Kimataifa la Hali ya Hewa (IMO) lililoanzishwa mwaka 1873 ili kuendeleza mshikamano katika masuala ya hali ya hewa kwa ajili ya kulinda maisha ya binadamu na mali zao.
Wakati Shirika la Kimataifa la Hali ya Hewa halikua na makubaliano yoyote ya kimataifa, Shirika la Hali ya Hewa Duniani lilikuwa Taasisi maalum ya mfumo wa kimataifa mapema mwaka 1951 na ilipofika mwaka 1972 lilipanua majukumu yake katika Hali ya Hewa na Klaimatolojia na kujumuisha yale ya Maji na mengine mengi ya Mazingira.
Wageni waalikwa, mabibi na mabwana,
Sherehe za Siku ya Hali ya Hewa Duniani kila mwaka kiutamaduni zimekua zikilenga mada maalum iliyokuwa ikichaguliwa. Kauli mbiu iliyochaguliwa na Halmashauri Kuu ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka huu wa 2012 ni ‘HALI YA HEWA NA MAJI KWA MUSTAKBALI WETU’ (“Powering our future with weather, climate and water”) iliyochaguliwa makhsusi kwa ajili ya kufafanua manufaa endelevu yapatikanayo kwa matumizi ya taarifa za hali ya hewa, klimatolojia na maji kwa sekta mbali mbali za kijamii na kiuchumi kwa ajili yetu na kizazi kijacho.
Mifano ya manufaa hayo ni mingi mno. Kwa mfano, upatikanaji wa chakula chetu na shughuli za kilimo ni lazima ziendane na hali ya hewa ya sehemu husika pamoja na upatikanaji wa maji. Shughuli za viwanda zinahitaji maji mengi pamoja na nishati. Miji inahitaji hewa safi na kulindwa kutokana na dhoruba na mafuriko.
Biashara za kimataifa na utalii vyote vinahitaji usafiri wa salama na wenye ufanisi, nakadhalika nakadhalika.
Kwa kweli tunategemea mpaka dakika ya mwisho utabiri wa hali ya hewa wa kuaminika kwa kila kitu kuanzia shughuli za kijamii mpaka katika kufanya maamuzi ya miradi ya mamilioni ya madola. Inaaminika kwamba katika moja ya tafiti zilizofanyika hivi karibuni nchini Marekani, uchumi wake hubadilika mpaka kwa US $ 485 bilioni kwa mwaka kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa nchini humo.
Uchaguzi wa kauli mbiu hii kwa mwaka huu imeonekana ni muwafaka hasa pale ilipokubalika kwa pamoja katika mkutano mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani mwaka 2011 kwamba mwaka huu wa 2012 uzinduliwe mfumo wa kimataifa wa huduma za hali ya hewa (Global Framework for Climate Services – GFCS).
Kama mnavyoelewa kwamba, jopo la kimataifa linaloshughulikia mabadiliko ya hali ya hewa ( Intergovernmental Panel on Climate Change – IPCC ), ambalo liliundwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani na ambalo limekuwa likifadhili kwa pamoja na Mpango wa umoja wa mataifa wa mazingira (UNEP) tokea mwaka 1988, na ambalo mwisho wa mwaka 2007 lilipata tuzo ya juu ya amani, lilifafanua kinaganaga kwamba baadhi ya shughuli za binaadamu zinachangia katika kuongeza joto la mfumo mzima wa hali ya hewa na lina athari kwa mazingira yetu kama vile ongezeko la wastni wa joto la hewa na bahari, kuyeyuka kwa theluji na barafu na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari. Hili ni suala ambalo Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa aliliainisha kuwa ni Changamoto ya hizi enzi zetu. Kwa hivyo itakuwa ni muhimu sana kwetu tuhakikishe kwamba katika juhudi zetu zote za kutekeleza mfumo wa Kimataifa wa huduma za hali ya hewa, na hasa katika kuchangia maendeleo endelevu, basi tuzingatie haja ya kupunguza uzalishaji wa gesi mkaa ( greenhouse gases ) kadri inavyowezekana.
Aidha, katika mkutano mkuu wa 16 wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani ( Sixteenth WMO Congress) katika mwaka 2011, ilikubalika kwamba vipaumbele vine vya mwanzo vya mfumo wa kimataifa wa huduma za hali ya hewa vitakuwa katika upunguzaji wa athari za majanga, maji, afya na usalama wa chakula. Kipaumbele hichi cha mwanzo, yaani upunguzaji wa athari za majanga, kimekuwa kipaumbele cha juu cha Shirika la Hali ya Hewa Duniani kwa muda mrefu, na kinaendelea kuwa hivyo, kutokana na kwamba jamii zinazodhurika na majanga katika dunia nzima zimekuwa zikiongeza juhudi zao katika kudhibiti majanga asilia kwa karibu asilimia 90 ambayo katika miaka 50 iliyopita yalihusishwa na majanga yanayosababishwa na hali ya hewa, klimatologia na maji na suala hili limo katika majukumu ya WMO. Kuongezeka kwa jamii zinazodhurika na majanga asilia katika dunia kumechangiwa sana katika muongo uliopita kutokana na kupanuka kwa miji, kuhama kwa watu na kuhamia katika sehemu zilizo hatarishi zaidi kama vile sehemu za mwambao, mabondeni, sehemu za ukame na zilizo tambarare ambazo kwa kawaida hupata mafuriko.
Aidha suala hili pia huchangiwa zaidi na kuongezeka kwa matokeo na kasi ya majanga yaliyotegemewa katika naripoti ya nne ya tathmini ya jopo la Kimataifa la mabadiliko ya hali ya hewa ( IPCC Fourth Assessment Report ). Kwa kawaida watendaji na wapangaji wakuu wataendelea kuhitaji zaidi huduma bora za hali ya hewa na taarifa za maji ili kuweka vizuri mipango yao ya dharura. Utoaji wa taarifa zinazohusu hali ya hewa, klimatolojia na maji unahitajika pia katika kukimu shughuli mbali mbali muhimu za kijamii na kiuchumi kama vile kilimo, afya, usafiri,uzalishaji wa nishati na udhibiti wa raslimali ya maji, shughuli ambazo huleta maendeleo makubwa katika uekezaji.
Katika mkutano wake wa 17 wa hivi karibuni wa mfumo wa Kimataifa wa makubaliano juu ya mabadiliko ya hali ya hewa ( UNFCCC COP 17 session ) uliofanyika huko Durban, Afrika Kusini, Shirika la Hali ya Hewa Duniani liliendelea kusisitiza zaidi kwamba utafiti, uchunguzi, utabiri na kujenga uwezo wa maendeleo katika haya ni vitu vya msingi sana katika kukinga maisha na mali za watu katika nchi zenye sehemu hatarishi ambazo nyingi tayari zina matatizo mengi katika kuzidumisha huduma za hali ya hewa na maji pamoja na mitandao ya mawasiliano na kwa hivyo zitahitaji kuwezeshwa kuziba mapengo haya yaliyosababishwa na maendeleo ya kisayansi na teknolojia ya dunia inayoendelea.
Aidha, Shirika la Hali ya Hewa Duniani liliendelea kusisitiza kwamba nchi zinazoendelea, visiwa vidogovidogo vinavoendelea na nchi nyengine zilizoendelea ambazo hudhurika na majanga ziendelee kuwezeshwa kutumia mifumo ya tahadhari ( early warning systems ) kwa ajili ya kulinda maendeleo yao pamoja na mazingira na hali ya hewa ya dunia kwa ajili kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa hivyo Kauli mbiu ya mwaka huu 2012 ni muwafaka kwa vile inatoa fursa kwa wajumbe wote wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani kuelezea faida inayoweza kupatikana kutokana na kutumia taarifa za hali ya hewa, klaimatolojia na maji pamoja na taarifa za mwelekeo wake. Manufaa yanayopatikana yatakuwa ni muhimu katika nyanja zote za raslimali na kwa viwango vyote.
Wageni waalikwa, mabibi na mabwana,
Kabla ya kumalizia hotuba yangu hii ningependa kukumbushia hapa kidogo juu ya kauli iliyotolewa hivi karibuni na Shirika la Hali ya Hewa Duniani ( WMO ) juu ya hali ya hewa ilivyo, ilibainisha kwamba hali ya hewa yetu inaendelea kubadilika. Kwamba miaka 13 ya joto kali zaidi yote imetokea kuanzia mwaka 1997 na kwamba hali ya joto katika dunia katika mwaka 2011 lilikuwa kubwa zaidi kuliko miaka ya nyuma iliyokuwa na La-Nina, tukio ambalo kwa kawaida huwa linapoza hali ya hewa. Mkusanyiko wa hewa mkaa ( greenhouse gases ) angani umekuwa ukiongezeka kwa kasi ile ile na kufikia kiwango kikubwa mwaka 2011.
Kutokana na hayo niliyoyaeleza kabla na kwa kuzingatia kuwa hali ya hewa haina mipaka ya kisiasa, Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikishirikiana na Wizara ya Uchukuzi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa itaendelea kuunga mkono utekelezaji wa mfumo wa kubadilishana taarifa na takwimu za hali ya hewa, hali ya hewa ya muda mrefu (klimatolojia), maji na huduma nyinginezo ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili nchi yetu, zinazoikabili Mamlaka kama zilivyoelezwa kabla na Mkurugenzi na zile zinazoikabili dunia kwa ujumla.
Wito kwa wananchi wasidharau taarifa zitolewazo – hasa wenye vyombo vya majini (manahodha), abiria wenyewe, na kwamba wananchi waache kujenga kwenye mabanda ya mpunga na kando kando ya madimbwi ya maji yaliyozagaa.
Wageni waalikwa, mabibi na mabwana,
Baada ya kusema hayo machache, nachukua fursa hii kuwatakieni sherehe nzuri za maadhimisho haya ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani. Nawashukuru kwa kunisikiliza, na nasema ahsanteni sana.
No comments:
Post a Comment