Khamis Ali Suleiman
HOTUBA YA MKURUGENZI ZANZIBAR KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI TAREHE 23 MACHI 2012
Katibu Mkuu, Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano (SMZ)
Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar
Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka kutoka Zanzibar
Meneja – uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zanzibar
Meneja –TCAA Zanzibar
Meneja mstaafu wa TMA
Walimu na wanafunzi wa skuli mbali mbali mlohudhuria
Wageni Waalikwa
Wafanyakazi wenzangu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Zanzibar
Mabibi na Mabwana,
Assalam alaikum,
Mheshimiwa Mgeni rasmi,
Napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru Mheshimiwa Waziri kwa kukubali na kupata muda wa kuja kwenye hafla hii pamoja na shughuli nyingi ulizonazo za kitaifa na kimataifa. Sisi tumefarijika sana kwa kuja kwako na tuna imani kubwa kuwa tutakayoyapata kutoka kwako yatatupa nafasi nzuri ya mtazamo wetu katika utendaji wetu wa kazi zetu za kila siku pamoja na kwenye maeneo mengine yanayotugusa kwa njia moja au nyengine.
Aidha, kwa niaba ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya Zanzibar napenda kuwashukuru sana sana wageni wetu wote waalikwa waliokuja hapa kushirikiana nasi katika maadhimisho haya ya SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI, nasema karibuni sana.
Mheshimiwa Mgeni rasmi, wageni waalikwa,
Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), ambalo leo hii tunaadhimisha kuasisiwa kwake, lilianzishwa mwaka 1950 na kuwa mojawapo ya jumuiya kuu za Umoja wa Mataifa ili kusimamia, kuratibu, kuweka viwango vya vifaa vya kupimia na jinsi ya kupima hali ya hewa. Kadiri ya miaka ilivyoenda Shirika hilo lilipanua shuhuli zake na kuanza kushuhulikia pia masuala ya maji na mazingira. Hapa nchini, kuanzia mwaka 1999 huduma hizi zinatolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania chini ya Wizara ya Usafirishaji ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyochukua majukumu ya iliyokuwa Idara ya Hali ya Hewa.
Mheshimiwa Waziri na wageni waalikwa,
Naomba pia nichukue fursa hii angalau kidogo nielezee majukumu ya Mamlaka yetu ya Hali ya Hewa ikiwa moja ya vichocheo vya kuleta maendeleo nchini. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa ujumla ina jukumu kubwa la kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa Taifa letu ikiwa ni pamoja na kutoa huduma kwa sekta mbali mbali za uchumi na jamii zikiwemo mipango ya maendeleo, kilimo, uvuvi na mifugo, usafiri wa anga, majini na nchi kavu, majanga ya asilia, afya, nishati, maji, ujenzi na maeneo mengine mengi. Katika kufanikisha kutoa huduma katika maeneo haya na mengine Mheshimiwa Waziri, Mamlaka inapaswa kufanya kati ya mengi kama ifuatavyo:
• Kuviendesha na kuviendeleza vituo vya hali ya hewa nchini;
. Kupima, kukusanya, kuchambua na kuzihifadhi takwimu za hali ya hewa pamoja na kuzifanyia kazi;
• Kutoa huduma za hali ya hewa kwa wananchi kwa usalama wao na mali zao ikiwa ni pamoja na shughuli kadhaa za maendeleo;
• Kutoa ushauri na tahadhari kuhusu majanga ya asili yanayohusiana na hali mbaya ya hewa yanayoweza kutokea;
• Kubadilishana takwimu za hali ya hewa katika mfumo wa kimataifa wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO);
• Kushirikiana na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), nchi za kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika kwa ujumla (AU) katika nyanja za hali ya hewa; na
• Kushiriki katika shughuli za Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).
Wageni waalikwa, mabibi na mabwana,
Imekuwa ni kawaida kila mwaka kuwa na ujumbe mahususi wa kusherehekea siku hii na mwaka huu wa 2012 ujumbe , au kauli mbiu ni HALI YA HEWA KWA MUSTAKBALI WETU (Powering our future with weather, climate and water). Ujumbe huu ni muafaka hasa ukizingatia kuwa mataifa yote ulimwenguni yanajitahidi kufikia malengo ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo ya Millenium hususan ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi kwa afya, chakula, maji salama , kuondoa umasikini na kuhamasisha jamii jinsi ya kuzuia na kujikinga na majanga ya asili ambayo kwa asilimia 90 husababishwa na hali mbaya ya hewa.Watafiti wa sayansi wakishirikiana na wataalaam wa masuala ya afya wamegundua kwamba kuna uhusiano mkubwa kati ya mabadiliko ya hali ya hewa, tabia nchi na afya ya binadamu na viumbe vyote viishivyo juu ya uso wa dunia.
Mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi ni changamoto kubwa kwa kizazi chetu cha sasa na baadae . Kuongezeka kwa gesi joto katika anga la dunia, mabadiliko ya halijoto, kuongezeka kwa matukio ya ukame na mafuriko ya mara kwa mara kutaleta athari kubwa kwa jamii. Hayo ni majaribio makubwa katika kupima uwezo na ubunifu wetu katika kukabiliana na majanga. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania itaendelea na juhudi zake za kuwasilisha taarifa kwa wakati kwa wadau mbalimbali wanao husika na matumizi ya taarifa hizi. Aidha, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ambayo imepewa majukumu haya itashirikiana na taasisi zinazotumia taarifa hizi.
Huduma za hali ya hewa zinapotolewa kwa wakati na kukidhi mahitaji ya taasisi husika ni faida kubwa kwa wadau wote pamoja na wafanya biashara, watu wa mipango, na wakulima pamoja na wengine wengi. n.k. Malengo ya huduma hizo za hali yahewa ni kuonyesha umoja katika dunia kutafsiri elimu ya sayansi kwa jamii kwa kuzingatia mahitaji ya nchi.
Wageni waalikwa, mabibi na mabwana,
Tumekwisha ona mara nyingi jinsi watu wanvyopoteza maisha, na waathirika wakiwa mamilioni kutokana na hali mbaya ya hewa. Matukio haya yanatokea mara kwa mara na yaneandela kuathiri watu zaidi. Kutoa huduma za hali ya hewa kwa waathirika wa mara kwa mara na kwa kiwango kikubwa huwawezesha kuchukua hatua ya kupunguza athari kwa maisha na mali zao.
Asili mia themanini ya watu wanaendesha maisha yao kwa kutumia kilimo na ni njia pekee ya kuboresha afya zao. Kwa ujumla katika miongo mitano ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la uzalishaji wa mazao ya kilimo, tunashukuru kwa matumizi mazuri ya mbinu bora za kilimo kama vile matumizi ya mbolea, umwagiliaji n.k, ikiwa pamoja na sera nzuri za Taifa.
Utafiti uliofanyika hivi karibuni katika bara la Afrika, umeonesha kuwa ni kilimo pekee chanye nafasi ya kuwezesha kuongeza mapato katika siku za hivi karibuni.
Ukame ni moja ya majanga asilia ambayo huyakumba maeneo mbalimbali katika vipindi vya msimu hadi karne.Taarifa ya utafiti ya mwaka 2011 iliyotolewa na jopo la kimataifa la wanasayansi linalohusika na mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi ‘Intergovernmental Panel on Climate Change’ (IPCC), linatabiri kuongezeka kwa majanga hayo. Mataifa mengi yanakosa sera zitakazo wezesha kukabiliana na majanga hayo kitaifa na kikanda.
Mfumo wa kukabiliana na athari za mafuriko ni pamoja na kuweka mikakati ya kupunguza madhara kabla hayajatokea.
Mafuriko, tufani, ukame, maporomoko ya ardhi pamoja na majanga mengine yatokanayo na hali ya hewa ni matukio yanayotokea mara kwa mara nchini Tanzania. Ili kuzuia maafa yatokanayo na majanga asili , ushauri wa wataalamu hauna budi kuzingatiwa. Utaalamu na uwezo wa Mamlaka ya Hali ya Hewa unahitajika zaidi katika kufanikisha adhma hii. Sambamba na mabadiliko ya Hali ya hewa na tabia nchi, matukio ya majanga yanatarajiwa kuongezeka. Utabiri na tahadhari zinazohusu hali ya hewa na maji pamoja na mejejimenti ya maafa zimefanikisha kuokoa maisha ya watu wengi. Hata hivyo, ongezeko kubwa la watu pamoja na hali ya umaskini vinachangia watu kuishi katika maeneo hatarishi zaidi. Hii ni pamoja na nyumba kujengwa katika mikondo ya mafuriko, maporomoko ya ardhi, na kilimo katika maeneo yenye ukame.
Mfumo wa kutoa tahadhari ni muhimu katika kujikinga na hatari za kiafya zitokanazo na hali ya hewa, madhalani, tahadhari kuhusu ongezeko la mbu ni wa thamani. Sera na mipango ya kijamii inayohusu hali ya hewa na maji ni muhimu katika kuhakikisha afya ya jamii hususan upatikanaji wa maji, udhibiti wa magonjwa ya mlipuko, hewa safi, nyumba bora pamoja na kuwepo kwa mfumo bora katika menejimenti ya maafa. Matokeo mazuri ya hatua hizi yanategemea jamii iliyojiandaa vyema kukabiliana na changamoto hizo.
Ndugu Mgeni rasmi,
Hudama za hali ya hewa ni muhimu katika sekta ya usafirishaji majini, angani na nchi kavu kwa namna mbalimbali; usalama na kuongeza ufanisi wa sekta ya usafrishaji katika mazingira ya mabadiliko ya hali ya hewa na bahari. Mkataba wa SOLAS (Safety of Life at Sea Convention) umeweka mahitaji mahususi ya hali ya hewa ambapo Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini inawajibu wa kutoa huduma zitakazowezesha usafiri salama majini.
Usafiri wa anga unatoa fursa za safari za masafa marefu hususani kwa usafirishaji wa bidhaa zinazoharibika mapema. Sekta hii inategemea sana takwimu na utabiri wa hali wa hewa unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Shughuli za mashirika ya ndege zinahitaji taarifa za nguvu ya upepo na mwelekeo wake, mawingu, theluji na maeneo yenye mawingu ya radi katika viwanja vya ndege. Mashirika hayo pia hutumia taarifa hizo kupanga njia na umbali wa mruko wa ndege wenye gharama nafuu. Huduma hizi zinatoa manufaa mengi ikiwamo kuepuka maeneo hatarishi, kupunguza matumizi ya nishati ya mafuta na gharama, na kuhakikisha safari za ndege zinakamilika kwa wakati uliopangwa. Ni jambo linalokubalika na wengi kuwa, sekta ya nishati hususani nishati ya mafuta inachangia katika mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.
Mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi yanaongeza umuhimu wa kuhusisha huduma za hali ya hewa na maji katika shughuli za mipango miji na uhandisi, ujenzi wa miundombinu na usimamizi wa fukwe kukabiliana na chanagmoto zijazo. Mipango ya usafirishaji jijini pamoja na uzalishaji na usambazaji wa umeme havina budi kuhusisha sio tu hali ya hewa ya sasa bali na mabadiliko yake.. Miji inahitaji taarifa za klaimatolojia za muda mrefu, takwimu na utabiri kusaidia utoaji wa maamuzi mbalimbali.
Ili kufanikisha malengo ya millennium ya mwaka 2015, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania itaendelea kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo endelevu yanayotumainiwa na watanzania. Hali ya hewa, maji na mazingira imeendelea kuwezesha mustakbali wa maendeleo yetu na itaendelea kuwa hivyo kwa siku za baadae.
Mheshimiwa Waziri,
Kwa upande wa Zanzibar Mamlaka ina changamoto kadhaa katika kufanikisha majukumu haya zikiwa ni pamoja na:
• Upungufu wa vituo na vifaa vya kupimia hali ya hewa;
• Gharama kubwa za kununua na kuendesha mitambo ya hali ya hewa wakati bajeti ya Mamlaka ni finyu;
• Ongezeko la mahitaji ya taarifa maalum za hali ya hewa kwa wadau wa sekta mbali mbali kwa shughuli zao za kila siku;
• Kuongezeka kwa matukio ya majanga ya hali mbaya ya hewa;
• Ukosefu wa ofisi ya Mamlaka kwenye bandari ya Zanzibar kwa ajili ya kutoa huduma kwa vyombo vya baharini;
• Mabadiliko ya hali ya hewa duniani jambo linalofanya utabiri wa hali ya hewa kuhitaji nguvu ya ziada ili kupata usahihi unaohitajika;
• Upungufu wa wataalam wa hali ya hewa kutokana na baadhi yao kufikia umri wa kustaafu;
• Ufinyu wa bajeti; • Upungufu wa ofisi kwenye uwanja wa ndege, Pemba.
Baada ya kutoa taarifa hii fupi nawatakia siku njema ya kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani 2012.
No comments:
Post a Comment