Habari za Punde

Tunalazimishwa Kuchukua Sheria Mkononi

Salim Said Salim

UTAWALA bora si tu kuwa na katiba na sheria nzuri kwenye vitabu, bali kwa kila mmoja, raia na mgeni, mkubwa na mdogo, tajiri na maskini kuziheshimu.

Pale ambapo panatokea kundi la watu kutokana na nguvu zao za misuli, fedha au madaraka waliyonayo katika serikali kuzipuuza na kutojali sheria za nchi basi matokeo yake huwa balaa kubwa.

Hali kama hiyo inapochomoza wananchi wengi hupoteza matumaini na hukata tamaa na wengine kuanza kujiuliza masuali ambayo majawabu yake hawayapati .


Kinachofutia ni kwa wananchi kuamua kuchukua sheria mikononi kwani huona vyombo vya dola vinavyotarajiwa kufanya hivyo, vimeshindwa kazi.

Vitendo vyao vinaweza hata kusababisha watu wengine kujeruhiwa na hata kupoteza maisha.

Kwa vyovyote vile, hata pakiwepo uvunjaji wa sheria na wanaofanya hivyo kutoguswa na sheria za nchi bado hakuna mwenye haki au anayeweza kutumia kisingizio chochote kile kinachoweza kuhalalisha kuchukua sheria mikononi mwake. Mwenye malalamiko anatakiwa aende mahakamani, hata kama hana imani na mahakama.

Lakini sote tunaelewa jinsi hasira zinavyoweza kuwasukuma watu kufanya mambo ambayo baadaye hujutia na kujilaumu kwa nini walifanya hivyo. Jibu huwa ni hasira…hasara.

Hivi karibuni zimesikika habari za wana vijiji wa Selem, karibu kilomita 15 nje ya mji wa Zanzibar, wameanza kugawana viwanja vya kujenga nyumba baada ya maombi yao waliyopeleka serikalini kwa muda mrefu kupuuzwa na wakati huo huo kuona wakubwa wanamegewa mapande makubwa ya ardhi kujenga nyumba za kifahari huku wao wakiangalia kwa unyonge.

Sehemu kubwa ya Selem ni shamba la serikali na liliendelezwa kwa upandaji wa minazi mifupi kwa msaada wa zaidi ya miaka 10 uliotolewa na serikali ya Finalnd. Lakini mara baaada ya mradi wa minazi kumalizika muda wake, shamba lilianza kukatwa mapande mapande, huyu kachukua ekari tano, yule sita na wengine zaidi ya 10. Wanyonge wakibaki wanaangalia.

Wengi wa wakubwa waliojimegea shamba la Selem ni viongozi wa juu, watendaji waaandamizi katika serikali ya awamu ya nne na ya tano. Hii si haki hata kidogo na kwa kweli ni dhambi.

Lakini uvamizi wa ardhi na hasa mashamba ya serikali unashuhudiwa si kwa shamba la Selem tu. Katika kisiwa cha Pemba wana familia wa aliyekuwa kiongozi mmoja wa serikali anasemekana kuchukua sehemu kubwa ya shamba la serikali lililopo Micheweni, Kaskazini Pemba.

Eneo kubwa la Micheweni, ambapo ndipo penye umaskini uliokithiri zaidi katika visiwa vya Unguja na Pemba, ni la mawe na halina rutuba. Lakini shamba hili la serikali ambalo ni kituo cha mafunzo ya kilimo bora lipo katika sehemu yenye rutuba.

Wananchi wa eneo hilo wamepiga kelele na kutaka wapatiwe ardhi kwa ajili ya kilimo ili kujikwamua na umasikini, lakini maombi yao yamezibwa masikio.

Miaka mitatu iliyopita zilisikika kelele za kudaiwa viongozi na watendaji waandamizi wa serikali, hasa katika Wizara ya Ujenzi na Ardhi, wamechukua sehemu kubwa ya viwanja vilivyopimwa katika eneo la Tunguu, nje ya mji wa Zanzibar na baadhi yao wamepatiwa viwanja vitatu hadi vinne.

Hatimaye iliundwa tume kuchunguza na ripoti yake ambayo inasadikiwa kuficha mengi kwa vile baadhi ya wafanyakazi wa wizara hiyo ndio waliokuwa wajumbe wa tume. Hata hivyo, ripoti ilieleza kuwepo watu ambao baada ya kuchukua viwanja kwa majina yao, wake au waume zao, pia waliwapatia viwanja wajukuu zao, wengine wakiwa ndiyo kwanza wanatambaa.

Kinachoshangaza hapa ni kwamba yalitolewa tu maelezo ya uchunguzi na si ripoti yenyewe na majina ya watu waliokufa, kufichwa.

Katika utawala bora, ungelitegemea wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria au kinadhamu, kama kuyaanika majina yao hadharani ili angalau waone aibu na wengine watakaotaka kufanya hivyo, wafikiri mara mbili au tatu kabla.

Hapa unaona wazi mwenendo wa ule usemi maarufu wa Kiswahili wa mshitakiwa ni Msomali, mwendesha mashitaka ni Msomali na hakimu ni Msomali. Katika hali kama hii huwezi kutarajia haki kupatikana. Wazungu nao wanao msemo unaeleza : “Scratch my back and I scratch yours.” ( Nikune mgongo wangu na mimi nitaukuna wako).

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Maliasili, Afaan Othman Maalim, amesema serikali haijawahi kutoa eneo la ardhi sehemu hiyo kwa wananchi wala viongozi na kama wapo watu ambao wamechukua ardhi na kujenga nyumba basi wamefanya hivyo kinyume cha sheria.

Hii ina maana wizara yake haijui kinachoendelea Selem au yale majengo ni ya mashetani na kwamba ina miujiza ya kutoweza kuonekana na maofisa wa serikali?

Je, hapa tunataka kuambiwa maofisa kilimo wanaoranda kila siku na magari makubwa na mapikipiki yanayotolewa kama msaada na washirika wetu wa maendeleo wamebana kimya na hawajawahi kutoa taarifa juu ya sehemu kubwa ya Selem kuchukuliwa na wakubwa kwa ujenzi wa majumba?

Jamani, kama hatuna ubavu wa kusema ukweli tuache kujidanganya na kudanganya wengine. Watu wanaona na mwenye macho haambiwi tazama. Hizi ni zama za ukweli na uwazi na waliopora ardhi kama hawataki kuwekwa hadharani basi wasingechukua hayo maeneo.

Tatizo la kinyang’anyiro kinachoonekana katika Kijiji cha Selem linafaa kushughulikiwa haraka kwa sababu malalamiko ya uporaji ardhi yamekuwa makubwa kila pembe ya visiwa vya Unguja na Pemba na hatari ninayoiona ni uwezekano wa wanavijiji wa maeneo mengine ya Visiwani kuiga kinachofanywa na wanavijiji wa Selem, yaani kuchukuwa sheria mikononi mwao.

Matokeo yake hapo baadaye tunaweza kuwepo na vurugu ya aina yake Visiwani na tutapokuja kuamua kuanza kukamatana mashati tutakuta hayo mashati yenyewe yameshachoka na kuraruka na kunyauka na hakuna sehemu ya shati unayoweza kuikamata.

Kama kweli Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliopo Zanzibar imepania kweli kutandika utawala wa haki na sheria basi suala la Selem lichunguzwe na majina ya watu wote waliojenga majumba au mabanda ya mifugo na kuku katika sehemu hiyo kwa kutumia nguvu zao za misuli, fedha au madaraka yatangazwe.

Vile vile matatizo ya uporaji wa ardhi na mashamba ya watu katika sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba ni lazima yakomeshwe haraka na kutafutiwa dawa na wote wanaohusika wachukuliwe hatua za kisheria. Vinginevyo tutakuwa tunakaribisha balaa kubwa.

Zanzibar imepita katika wakati mgumu na mrefu wa balaa za kisiasa hata amani na utulivu uliopo sasa ukapatikana.

Ni vema, ni jambo la busara na itakuwa matumizi ya hekima kama kila Mzanzibari awe ana nguvu za misuli, fedha au madaraka, atafanya kila juhudi za kulinda amani iliyopo na kujizuia kufanya mambo ambayo yanaweza kuwarudisha watu wa Visiwani walipotoka.

Sheria ni msumeno na uachiwe kufanya kazi yake kwani msumeno huwa na maana kama utapasua mbao na si kutundikwa ukutani kama pambo la nyumba.

Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.