Na Raya Hamad (OMKR)                                                 
Wazazi na walezi wametakiwa kutoyafumbia macho matatizo mbali mbali yanayowapata watoto wenye ulemavu wa akili na badala yake waende katika vyombo vya sheria au Jumuia zinazotetea masuala ya Watu wenye ulemavu.
Wito huo umetolewa na Bi Mwanamgeni Ali wakati alipokuwa akielezea mkasa uliomkuta mwanae  Msim Idrissa Mwinyi mwenye ulemavu wa akili ambae amebakwa na mtu wakaribu na familia yao nahatimae kupelekea kupata ujauzito .
Bi Mwanamgeni amesema kuwa muwazi katika kuelezea matatizo ya mwanawe kwenye taasisi husika ikiwemo ZAFELA  na Umoja wa Watu Wenye Ulemavu  kumepelekea kupata mafanikiao hadi kufikia mwanawe kujifungua salama ingawa kwa njia ya upasuaji .
Msimu Idrisa Mwinyi  mwenye umri wa miaka 16  mkaazi wa Kisakasaka Wilaya ya Magharibi alibakwa na mtu wa karibu jina linahifadhiwa na hatimae kupata ujauzito anao uwezo wa kujielezea na kufahamisha sehemu alikokuwa akipelekwa. 
Akitowa ufafanuzi juu ya suala hilo Afisa msimamizi na ufatiliaji wa masuala ya watu wenye ulemavu kutoka Umoja wa Watu wenye Ulemavu  Bi Njuma Ali amesema kukosekana kwa ushahidi kwa watu wenye ulemavu wa akili isiwe sababu ya kutotiwa hatiani kwa wale washukiwa wa vitendo vya ubakaji ambavyo vimekuwa vikishamiri siku hadi siku .
“Imekuwa ni kawaida tunapokwenda Polisi kuambiwa hakuna ushahidi mpaka ajifungue kisha kipatikane kipimo cha DNA kitakachogharimu shilingi laki tano lakini ni ushahidi gani tena unaotakiwa wakati Msimu akiulizwa anasema nani kakupa mimba, anataja Juma baba ake Salama kanipeleka pwani kwenye mikoko akanifanyia uchimvi isitoshe wazazi wenyewe hali zao tunazifahamu  Msimu na mwanawe wanahitaji huduma ” alisisitiza Njuma.
Aidha Bi Njuma amesisitiza kuwa masuala ya sheria yawe wazi na hasa ukizingatia  pamoja na ulemavu wake wa akili na sura mfanano lakini Msimu bado ni mtoto  mdogo ambae hajafikia umri wa miaka 18 hivyo anahitaji kutendewa haki na mamlaka husika   
Msimu amejifungua mtoto wa kike anaitwa Amina jina ambalo amemuita mwenyewe anahitaji  kupata huduma yeye na mtoto wake ikiwemo maziwa kila siku jambo ambalo wazazi wake litawawia ugumu kutokana na hali zao pamoja na mahitaji mengine muhimu hivyo wameomba wasamaria wema kuweza kumsaidia Msimu.

No comments:
Post a Comment