Habari za Punde

Kampuni ya Simu ya Mkononi ya Zantel Yaipiga Jeki Polisi Zanzibar.

Meneja Biashara wa Zantel kanda ya Zanzibar Mohammed Mussa. akitowa maelezo ya Kampuni yake wakati wa kukabidhi Pikipiki kwa Jeshi la Polisi Zanzibar, hafla iliofanyika viwanja vya Bamani.
Kamishna Msaidizi Kenneth Kaseke alisema msaada huo ni faraja kubwa kwao, hasa katika kipindi hichi ambapo jeshi hilo lina kazi kubwa ya kuihamasisha jamii kuliunga mkono katika ulinzi wa taifa.

Wakiwa katika picha ya pamoja na Polisi Shirikishi, baada ya  kumalizika kwa makabidhiano ya Pikipiki hizo kwa ajili ya kuimarisha Ulinzi kwa Taifa na Mali zao Zanzibar. 


Na Salum Vuai, Maelezo

JUMLA ya pikipiki kumi zenye thamani ya shilingi milioni 15, zimekabidhiwa kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuliongezea nguvu ya kupambana na vitendo vya uhalifu nchini.

Msaada huo umetolewa na kampuni ya simu Zantel, na makabidhiano hayo kufanyika kwa sherehe kubwa kwenye uwanja wa Polisi Ziwani mjini Zanzibar.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi Khamis aliyekuwa mgeni rasmi, aliisifu kampuni ya Zantel kwa moyo wa uzalendo ilionao ambapo mara kwa mara imekuwa ikisaidia huduma mbalimbali za jamii.

Mwinyi alisema, ni dhahiri uongozi wa kampuni hiyo unaumwa na uzanzibari, na hivyo hauridhiki kuona jamii inakabiliwa na changamoto mbalimbali, nayo isiingize mkono mfukoni kutoa msaada wake.

Aidha alisema miongoni mwa changamoto kubwa zilizopo nchini hivi sasa, ni mazingira hatarishi kwa sekta ya utalii ambapo watu wasiokuwa na nia njema, wamekuwa wakiwasumbua watalii wanaofika nchini pamoja na kuwapora mali zao.

Naye Meneja Biashara wa Zantel kanda ya Zanzibar Mohammed Mussa, alisema kampuni yake inafarijika kutumia faida inayopata kutokana na wateja wake katika kusaidia mbalimbali kwa jamii, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono mpango wa polisi jamii ili kuwalinda wananchi, wageni pamoja na mali zao.

Akitoa shukurani kwa niaba ya jeshi lake,
Kamishna Msaidizi Kenneth Kaseke alisema msaada huo ni faraja kubwa kwao, hasa katika kipindi hichi ambapo jeshi hilo lina kazi kubwa ya kuihamasisha jamii kuliunga mkono katika ulinzi wa taifa.

Alihakikisha kuwa, pikipiki hizo zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, na kuwaomba wale watakaopewa kufanyia kazi, kuzitunza na kufanikisha jukumu la ulinzi na polisi jamii.

Hafla hiyo ilipambwa kwa matukio mbalimbali ya burudani, ikiwemo igizo, utenzi na maonesho ya kikosi cha mbwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.