Ni baada ya kukishtaki chama hicho mahakamani
Na Masanja Mabula, Pemba
CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA) Wilaya ya Micheweni Pemba, kimeifuta uwanachama klabu ya Small Manta kufuatia hatua yake ya kupeleka mahakamani shauri linalohusiana na michezo, jambo ambalo kwa mujibu wa ZFA, ni kinyume cha kanuni.
Barua ya chama hicho yenye namba ya kumbukumbu ZFA//WM/VOL.1/32/2012 iliyosainiwa na Katibu wa ZFA Wilaya hiyo Ahmed Khamis Mohamed kwenda kwa klabu hiyo na Zanzibar leo kupata nakala yake , imesema kuwa mwanachama yeyote wa ZFA haruhusiki kupeleka shauri la mchezo mahakamani.
Imezidi kufafanua kuwa, kwa mujibu wa katiba ya chama hicho ya mwaka 2006 Ibara ya 100, hatua ya mwisho ya ukataji wa rufaa kutokana na mchezo katika ngazi yoyote, ni Kamati ya Rufaa na Usuluhishi ya ZFA Taifa.
"Ibara ya 100 (1) imeweka bayana kwamba mwanachama yeyote hataruhusiwa kupeleka mahakamani shauri linalohusiana na matokeo ya mchezo katika mahakama na ZFA Wilaya imetumia kifungu hicho kuifukuza uanachama klabu hiyo", ilieleza sehemu ya barua hiyo.
Wakati ikichukua hatua ya kuitimua timu hiyo, ZFA Wilaya ilikwishapokea barua kutoka kwa msajili wa mahakama Wete, inayoagiza kusimamisha ligi daraja la pili na mchezo kati ya timu ya Makangale Stars na Scud Boys uliokuwa uchezwe tarehe 16 Februari, mwaka huu, lakini chama hicho kilidai kuwa kilistahamili ili kutoa nafasi kwa klabu hiyo kufuta shauri mahakamanai lakini haikufanya hivyo.
Barua hiyo imefafanua kuwa, Small Manta ilifikia uamuzi huo, baada ya ZFA Taifa kupinga hatua ya ZFA Wilaya, iliyotaka kutorejewa kwa mchezo kati ya Makangale na Scud Boys, na kwamba ZFA Wilaya iliitisha kikao terehe 12 Februari, mwaka huu, kwa ajili ya kubadilisha mfumo kutoka nne bora hadi sita bora, ambapo uongozi wa Small Manta ulipinga na kuahidi kwenda mahakamani .
Pamoja na ZFA kuifukuza uanachama klabu hiyo, bado kitendawili cha kitendawili cha kumpata bingwa na makamu wake katika ligi hiyo hakijapatiwa ufumbuzi kutokana na mahakama kuizuia isiendelee.
Hata hivyo mmoja wa viongozi wa ZFA wilayani humo amelidokeza gazeti hili kuwa, ligi hiyo yawezekana ikaendelea ndani ya wiki ijayo, baada ya kutekeleza agizo la kuifukuza klabu ya Small Manta, na kufahamisha kuwa huenda ikachezwa kwa mtindo wa mtoano ili kuwahi kalenda ya ZFA Taifa.
No comments:
Post a Comment