Habari za Punde

Waziri aiomba Deutsche Welle kuisaidia Zanzibar kuingia dijitali

Na Mwashamba Juma
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk ameliomba shirika la Utangazaji la Ujerumani Deutsche Welle kuisaidia Zanzibar katika harakati za kuingia kwenye mfumo wa mawasiliano wa dijitali.

Waziri huyo alieleza hayo jana ofisini wake Kikwajuni mjini hapa, alipofanya mazungumzo na ujumbe wa kutoka shirika la Utangazaji la Ujerumani, ambapo alisema msaada wa nchi hiyo kwa Zanzibar utaharakisha kuingia kwenye mfumo huo mpya.

Alisema kuwa matumizi ya mfumo wa analojia yatakwisha mwishoni mwa mwaka huu, ambapo Zanzibar imeanza kwa kasi matumizi ya dijitali hivyo itakuwa vizuri sana endapo shirika hilo litaisaidia Zanzibar ili iweze kuingia kwenye mageuzi hayo haraka iwezekanavyo ili isiachwe nyuma na dunia.

Waziri Mbarouk aliuomba ujumbe huo kulisaidia wataalamu shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), katika kubadilisha vipindi vyake ambavyo viko katika mfumo wa zamani wa analogi na kupeleka katika mfumo wa dijitali.

Aliomba kuendelezwa kwa ushirikiano uliopo baina ya Zanzibar na Ujerumani hasa katika vyombo vya habari na kutaka usiishie kwenye vyombo hivyo tu bali pia uangalie maeneo mengine yenye maslahi kwa nchi hizo.

Alisema uangaliwe uwezekano kwa Deutsche Welle, iwapatie mafunzo ya vitendo wafanyakazi wa vyombo vya habari vya Zanzibar, hali ambayo itawawezesha kufanya kazi zao kwa umakini zaidi.

Kwa upande wa ujumbe huo wa Deutsche Welle uliokuwa na maofisa wawili, Charles Achaye na Glido Loct, walisema shirika hilo litaendelea kuleta walimu zaidi watakaotoa mafunzo kwa ajili ya uendeshaji wa vyombo vya habari.

Walisema kwa muda wa miezi mitatu waliyokuwa visiwani hapa wakitoa taaluma juu ya uendeshaji wa vyombo vya habari walipata kila aina ya ushirikiano huku wakiwasisitiza wafanyakazi waliopata mafunzo hayo kuyatumia kwa ajili ya kuleta mabadiliko katika vyombo vya habari.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.