Habari za Punde

Waziri Shaaban: Wakandarasi ‘Uchwara’ Wanyimwe Zabuni


Na Haji Nassor, PEMBA

WAZIRI wa Ardhi Makaazi Maji na Nishati, Ramadhan Abdallah Shaaban, amezitaka taasisi za umma na za watu binfasi, kuzinyima zabuni kampuni za wakandarasi waliokuwa hawajasajiliwa na Bodi ya usajili wa wakandarasi Zanzibar (ZCRB).

Alisema wakandarasi wasiosajiliwa wanasababisha kuporomoka kwa majengo na kuharibika kwa miundombinu kabla ya wamiliki kuanza kuitumia, hali ambayo imetokana na kukosa sifa stahiki za ujenzi.

Waziri Shaaban alieleza hayo jana huko Wesha Chake Chake, alipokuwa akifungua mkutano wa siku moja wa kuitambulisha Bodi ya Usajili wa Wakandarasi Zanzibar (ZCRB), kwa wadau wa ujenzi kisiwani Pemba.

Alieleza kuwa Bodi hiyo ipo kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi, hivyo haitakuwa sahihi kuwakabidhi kazi za ujenzi wakandarasi ambao hawajajisajili kwenye bodi hiyo.

Aidha waziri huyo, alisema wakandarasi waliosajiliwa ni vyema wakajitahidi kufanyakazi zao kwa ufanisi na uhakika ili majengo na miundombinu wanayo wananayoijenga iweze kudumu.

“Suala la usajili kwa wakandarasi ni la lazima, kwa vile sheria imeshabainisha juu ya hilo, ni kosa kwa taasisi yeyote kuwapa tenda wakandarasi uchwara”, alisema waziri Shaaban.

Waziri Shaaban aliwataka wakandarasi wazalendo kwenda sambamba na wale wa kigeni na kuwataka wazingatie muda wa kumalizia kazi, wawe wabunifu hali itakayowafanya kwenda na wakati.

Alisema wapo baadhi ya wakandarasi wazalendo wamekuwa wakipuuza muda uliokubaliwa kukabidhi mradi na kusababaisha kuzorota kwa baadhi ya mejengo na miundombinu mengine.

Mapema akitoa salamu za Wakandarasi, Mkandarasi kutoka kampuni ya Quality Shaibu Ali, aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwapa miradi ya ujenzi wakandarasi wazalendo pale wanapowasilisha maombi ya zabuni.

Alisema iwapo kazi atapewa mkandarasi wa nje, hakuna faida kubwa inayopata serikali badala ya jengo husika alilojenga ambapo kwa upande wa mzalendo ni kuendelea kuwepo nchini.

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi Zanzibar (ZCRB) Rama Kessi, alisema kama kuna wakandarasi ni wazito kufuata taratibu za nchi, ni vyema wakandarasi wa aina hiyo wakanyima tenda.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa, hadi kufikia mwaka 2012 Bodi imeshasajili wakandarasi 22 wazalendo wakiwemo wenye fani mbali mbali kama vile wa majengo (building), wakandarasi maalum (specialist), majenzi (civil works).

Bodi ya Usajili wa Wakandarasi Zanzibar, imeanzishwa mwaka 2008, na kuanza kazi zake mwaka 2009, ambapo miongoni mwa majukumu yake ni pamoja na kuwasajili wakandarasi wote wanaofanyakazi za ujenzi Zanzibar.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.