Serikali imetoa onyo
kali kwa watu na kampuni zinazoendelea kuzalisha bidhaa za mifuko ya plastiki iliyopigwa
marufuku na kuingiza katika matumizi kwa njia za panya.
Imesema itaendelea
kufanya doria za kushtukiza katika viwanda, viwanda bubu na masoko ili
kuwabaini na kuwachukulia hatua wahusika wote wanaojihusisha na biashara hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni
amesema hayo leo Mei 27, 2025 jijini Dodoma wakati akitoa tamko la Serikali kuelekea
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kilele chake kitakuwa jijini
Dodoma na mgeni rasmi anatarajia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hatua hiyo inakuja
kutokana na kujitokeza kwa changamoto ya matumizi ya vifungashio vya plastiki
aina ya tubings kutumika kama vibebeo
na vifungashio ambavyo havina sifa na kutokukidhi matakwa yaliyowekwa na
Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Kufuatia hatua, Mhandisi
Masauni amelielekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira
(NEMC), Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mamlaka nyingine za umma kuendelea
kufuatilia na kuwabaini wahusika wote wanaokiuka sheria na kuzalisha bidhaa za
plastiki zilizopigwa marufuku kuzalishwa na kutumika nchini.
“Niwakumbushe Watanzania
wenzangu kuzingatia maelekezo ya Serikali kuachana na mifuko ya plastiki na
kutumia mifuko mbadala ambayo kwa sasa inapatikana nchini kote kwa gharama nafuu”
amesisitiza Mhandisi Masauni.
Aidha, alisema kuwa
pamoja na changamoto hiyo, kwa kiasi kikubwa Tanzania imepiga hatua katika
kudhibiti taka za plastiki baada ya kupiga marufuku uzalishaji, uingizaji,
usambazaji na matumizi ya mifuko ya plastiki kuanzia Juni, 2019, hatua
iliyosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Ili kuhakikisha
wananchi wanapata uelewa kuhusu kutambua mifuko na vifungashio vya plastiki
vilivyoruhusiwa, Mhe. Masauni alisema kuwa Serikali imeendelea kutoa elimu kwa
umma sambamba na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uzalishaji wa mifuko
mbadala ambazo ni rafiki kwa mazingira.
Akizungumzia maadhimisho
hayo, Waziri Masauni alisema yatachagizwa na maonesho ya Wadau ya Bidhaa, Huduma
na Ubunifu kuhusu Hifadhi ya Mazingira yakayoanza Juni mosi hadi 5, 2025 jijini
Dodoma.
Pia, alisema Kutakuwa na Kongamano
la Vijana litakalowatanisha vijana mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa vyuo,
wajasiriamali na mabalozi wa mazingira litakalofanyika jijini Dar es Salaam tarehe
3 Juni, 2025.
Kwa mujibu wa
Mhandisi Masauni, Kaulimbiu ya madhimisho ya mwaka huu ni ‘Tanzania Ijayo
Tuwajibike Sasa, Dhibiti Matumizi ya Plastiki’ inayolenga kuikumbusha jamii kuwa
mazingira na rasilimali zake ni msingi wa uhai na maisha pamoja na ukuaji wa Uchumi,
hivyo utunzaji na uhifadhi wa mazingira na rasilimali zake ni jambo muhimu.
MWISHO
No comments:
Post a Comment