Habari za Punde

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Amekutana na Kuzungumza na Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Usafafiri na Utalii wa Japan

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Ardhi,  Miundombinu, Usafirishaji na Utalii wa Japan,  Mheshimiwa Hiromasa Nakano  kwenye Makao Mkuu ya Wizara hiyo   Tokyo Japan, Mei 27, 2025.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza  na Waziri wa Ardhi,  Miundombinu, Usafirishaji, na Utalii wa Japan,  Mheshimiwa Hiromasa Nakano  kwenye Makao Mkuu ya Wizara hiyo   Tokyo Japan, Mei 27, 2025
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Ujumbe wake wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wizara ya Miundombinu, Usafirishaji na Utalii   ya  Japan pamoja na Rais wa Shirikisho la Wawekezaji katika Sekta ya Miundombinu la Japan (JAIDA)  baada ya mazungumzo kwenye makao makuu  ya Wizara hiyo, Tokyo Japan, Mei 27, 2025.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao  na  Naibu Waziri wa Miundombinu, Usafirishaji na Utalii   wa  Japan, Kenichi Ogasakawara pamoja na Rais wa Shirikisho la Wawekezaji katika Sekta ya Miundombinu Japan (JAIDA) kwenye makao makuu  ya Wizara hiyo, Tokyo Japan, Mei 27, 2025.



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Ujumbe wake wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wizara ya Miundombinu, Usafirishaji na Utalii   ya  Japan pamoja na Rais wa Shirikisho la Wawekezaji katika Sekta ya Miundombinu la Japan (JAIDA)  baada ya mazungumzo kwenye makao makuu  ya Wizara hiyo, Tokyo Japan, Mei 27, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)



WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameendelea kuwashawishi wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa wa Japan kuja kuwekeza kwenye sekta za kilimo, afya, uchumi wa buluu, nishati, miundombinu, ufugaji na TEHAMA kwani Serikali imeshaboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji.

Ameyasema hayo leo (Jumatano, Mei 28, 2025) alipokutana kwa nyakati tofauti na viongozi wa Shirikisho la Wawekezaji katika Sekta za Miundombinu, Shirikisho la Wawekezaji na Wafanyabiashara nchini Japan (KEIDANREN) na Jumuiya ya Wamiliki, Marais na Watendaji Wakuu wa Mashirika na Makampuni wa Japan (KEIZA DOYUKAI).Waziri Mkuu yuko Tokyo nchini Japan kwa ziara ya kikazi.

 “Tunakaribisha makampuni ya Japan kuchangamkia fursa nyingi za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania, zikiungwa mkono na mazingira tulivu ya biashara, mageuzi ya sera, na juhudi zinazoendelea za kupunguza urasimu.”

Jana, Mei 27, 2025, Mheshimiwa Majaliwa alikutana na Naibu Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Usafirishaji na Utalii wa Japan (MLIT), Kenichi Ogasawara pamoja na Rais wa Shirikisho la Wawekezaji katika Sekta za Miundombinu Japan na Afrika (JAIDA) Miyamoto Yaichi

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye ofisi za MLIT na kuhudhuriwa na Marais wa makampuni makubwa ya uwekezaji ya Japan, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji hao nchini kuwekeza kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za nishati, miundombinu, utalii, kilimo na biashara.

Aidha, Waziri Mkuu alisema kuwa Tanzania imejiimarisha katika kujenga uwezo wa rasilimali watu, hivyo aliwakaribisha katika kutoa mafunzo na programu za kubadilishana maarifa zitakazowezesha wahandisi wa Kitanzania, wapangaji miji, na wataalamu wa miundombinu kunufaika na utaalamu na ubunifu mkubwa wa Japan.

Alisema Japan imeendelea kuwa mmoja wa washirika wakubwa wa maendeleo wa Tanzania na kwa kipindi cha miaka mingi, nchi hizo mbili zimejenga uhusiano thabiti, hasa katika eneo la miundombinu. “Tunathamini sana uhusiano huu na mchango mkubwa wa makampuni ya Kijapani katika maendeleo ya Taifa letu.”

Alisema Serikali inaamini kuwa miundombinu bora ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi, kuboresha maisha ya watu, kuwezesha biashara, na kuimarisha ushirikiano wa kikanda. “Lengo la Tanzania kuendelea kuboresha mtandao wa barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege”.

“Haya ni maeneo muhimu ya kuimarisha muunganiko wa ndani ya nchi na maeneo ya kikanda. Miradi mikubwa kama Reli ya Kisasa (SGR) na upanuzi wa bandari za Dar es Salaam na Mtwara ni mifano thabiti ya dhamira yetu ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji wa kikanda.”

Kwa Upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Stanslaus Nyongo amesema kuwa ametumia vikao kuwaeleza wawekezaji na wafanyabaishara hao kuhusu mipango na mikakati ya Serikali katika kuhakikisha inavutia zaidi uwekezaji katika sekta mbalimbali.

Aidha, Mheshimiwa Nyongo amesema kuwa Serikali inaendelea na mchakato wa kuwa na dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ambayo itaeleza kwa kiasi kikubwa itasaidia kubainisha maeneo muhimu ya uwekezaji ili yanayolenga kukuza uchumi wa nchi.

Naye, Muwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania (UNDP) Shigeki Komatsubara amesema kuwa Tanzania itaendelea kunufaika na utaalam na teknolojia kutoka Japan katika sekta mbalimbali zikiwemo za Miundombinu na Rasilimali watu.

 (mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,                    

JUMATANO, MEI 28, 2025

One attachment • Scanne









 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.