Habari za Punde

TAKUKURU TANGA YABORESHA MFUMO WA HUDUMA ZA UDHIBITI TAKA NGUMU JIJINI TANGA



Na Oscar Assenga, TANGA
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Tanga (Takukuru) imesema kwamba moja ya mafanikio ya utendaji wake kazi katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi 2025 uboreshaji mfumo wa huduma za udhibiti Taka Ngumu Jijini Tanga.
Hayo yalisemwa leo na Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga Mariam Mayaya wakati akitoa taarifa kwa umma juu ya mafanikio ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2025.
Alisema kwa upande wa uchambuzi wa mifumo katika kipindi hicho taasisi hiyo imefanikiwa kutekeleza matakwa ya sheria na kanuni za udhibiti taka ngumu nchini Tanzania kwa kutumia mfumo wa Punguza,Tumia Tena na Rejeleza taka (PTR) au Reduce,Re-use and Reycle (3R),
Aidha alisema katika mkoa wa Tanga mfumo huo ulianza katika kata ya Central,Chumbageni na Ngamiani Kati pamoja na utekelezaji wa sheria ya udhibiti wa taka ngumu,uchambuzi uliofanywa na Takukuru umesaidia mikakati na maazimio ya kulipwa kwa madeni ya wazabuni hivyo kufanya kazi ya uzoaji taka kuanza kutekelezwa kwa ufanisi.

Mariam alisema kwamba kwa ujumla zimefanyika chambuzi za mifumo 20 katika sekta za udhibiti take na usafi wa Mazingira,Afya,Kilimo na mapato ambapo wamefanikiwa kubaini mapungufu na kuwasilisha ripoti za chambuzi husika kwa wadau ambazo zimejadiliwa na maazimio yaliyofikiwa yametekelezwa na mengine yanaendelea kutekelezwa kwa ufanisi.
Akizungumzia ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo,Mariam alisema kwamba katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025 walifanya kazi ya ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma katika miradi 54 yenye thamani ya Bilioni 240,264,703,118.09.
Alisema katika ufuatiliaji wa miradi hiyo iliyopo katika sekta za Maji,Elimu na Afya ambapo miradi 12 yenye thamani ya Sh.Bilioni 5,468,760,058 ilibainika kuwa na mapungufu ambapo ushauri wa marekebisho yalitolewa na hatua za marekebisho ya mapungufu hayo zimechukuliwa na miradi ipo katika hali inayokidhi ubora kulingana na thamani ya fedha zilizowekezwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.