Habari za Punde

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Amefanya Mazungumzo na Waziri Mkuu wa Japan. *Asema Japan itaendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Tanzania *Aagiza tathmini ya barabara za Kibiti-Lindi na Morogoro-Dodoma

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri Mkuu wa Japan Ishiba Shigeru kwenye mazungumzo rasmi yaliyolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na uchumi kati ya nchi hizo mbili. Mazungumzo hayo yalifanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tokyo nchini Japan, Mei 29, 2025.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri Mkuu wa Japan Ishiba Shigeru kabla ya mazungumzo rasmi yaliyolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na uchumi kati ya nchi hizo mbili. Mazungumzo hayo yalifanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tokyo nchini Japan, Mei 29, 2025. 
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekutana na Waziri Mkuu wa Japan, Ishiba  Shigeru ambaye amemuhakikishia kuwa nchi hiyo itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania jambo ambalo linalenga kuchochea ukuaji wa uchumi kutokana na fursa zitakazoendelea kupatikana kupitia mahusiano hayo.

Amekutana na kiongozi huyo leo (Alhamisi, Mei 29, 2025) katika ofisi ya Waziri Mkuu Tokyo, Japan, ambapo Mheshimiwa Majaliwa amesema ahadi hiyo inazidi kutoa fursa ya wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan pamoja na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kumueleza Waziri Mkuu huyo kuwa  pamoja na miradi mingine wanayotekeleza nchini, Japan kupitia JICA iangalie uwezekano wa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuzifanyia ukarabati mkubwa barabara za Morogoro-Dodoma na barabara ya Kibiti-Lindi ambayo imeharibika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini.

Amesema Waziri Mkuu wa Japan baada ya kupata maelezo hayo ameuelekeza uongozi wa JICA pamoja na Balozi wa Japan nchini Tanzania Youichi Mikami kwenda kutembelea barabara hizo na kuzifanyia tathmini ya uharibifu na kisha kuwasilisha taarifa ili Serikali ya Japan ione namna itakavyoshirikiana na Tanzania katika utekelezaji wake.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan amepongeza kuendelea kuimarika kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Japan na kwamba ameahidi kuhakikisha makampuni mbalimbali ya Japan yataendelea kufanyakazi na Tanzania ili kuisaidia katika kukuza uchumi, kuendelea masuala ya kijamii na teknolojia kwani wanatambua idadi ya watu nchini inaendelea kuongezeka.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amekutana na Rais na Mtendaji Mkuu wa Japan Tobacco Inc (JTI) Masamichi Terabatake pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni hiyo, Mutsuo Iwai ambapo pamoja na mambo mengine ameishawishi ijenge kiwanda cha kuongeza thamani ya zao la tumbaku mkoani Tabora.

Waziri Mkuu amesema kampuni hiyo ambayo ni miongoni mwa wanunuzi wakubwa wa tumbaku nchini na ndiyo inayoendesha kiwanda cha sigara kichopo Dar es Salaam kuwa ni vizuri wakapanua uwekezaji kwa kujenga kiwanda Tabora ili kurahisisha usafirishaji wa malighafi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema Tanzania ni nchi ya pili kwa uzalishaji wa tumbaku Barani Afrika na kwamba kampuni ya JTI inaongoza kwa kununua asilimia 25 ya tumbaku yote inayozalishwa nchini.

Naye, Rais na Mtendaji Mkuu wa Japan Tobacco Inc (JTI) Masamichi Terabatake ameahidi kuendelea kununua tumbaku nchini ambapo kwa mwaka huu wanatarajia kununua kilo milioni 33 zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 190, ambapo mwaka 2024 walinunua kilo milioni 30 zilizokuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 165.

Pia amesema katika kipindi cha miaka mitatu ijayo kuanzia mwaka 2026 hadi 2028 wanatarajia kutumia takribani Dola za Marekani milioni 1.5 kwa ajili ya kushirikiana na Serikali katika uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo afya, maji, elimu uwezeshaji wananchi kiuchumi pamoja na kusaidia watu wenye mahitaji maalumu.

 (mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,                    

ALHAMISI, MEI 29, 2025



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.