Habari za Punde

Jengo la SUZA Tunguu Kukabidhiwa Julai

Dk. Shein asisitiza umuhimu masomo ya sayansi

Na Rajab Mkasaba, IKULU
MKANADARASI anayejenga Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), anatarajiwa kukabidhi majengo hao yaliyopo Tunguu mwezi Julai mwaka huu.

Taarifa ya wizara hiyo ilieleza jana Ikulu mjini Zanzibar wakati uongozi wa wizara ulipokutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Mkutano wa viongozi wa wizara hiyo na Dk. Shein ulilenga kuangalia utekelezaji majukumu ya wizara kwa kuangalia robo tatu ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2011-2012.

Wizara hiyo ilimueleza Dk. Shein kuwa kazi za ujenzi wa Chuo hicho huko Tunguu imekamilika kwa asilimia 90 na kwamba ikifika Julai mwaka huu, Mkandarasi atakabidhi majengo ya Chuo hicho.

Uongozi wa wizara ulisema kazi zinazoendelea hivi sasa ni kupaka rangi na uchongaji wa madirisha, milango, makabati pamoja na kutengeneza bustani.

Aidha ripoti ya uongozi wa wizara hiyo, ilielezea tatizo la udanganyifu wa mitihani kwa wanafunzi, ambapo wizara hiyo inakusudia kuimarisha usimamzi wakati wa ufanyaji wa mitihani, kuimarisha ukaguzi na kuwapa mafunzo ya uongozi kwa waalimu wakuu na mafunzo kazini kwa walimu.

Aidha wizara hiyo inakusudia kuanzisha mitihani ya pamoja ya majaribio kwa wanafunzi wa darasa la saba, kidato cha pili, kidato cha nne na kidato cha tano, ambapo wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na mchepuo watafanya mitihani ya kidato cha pili na watakaoshindwa watarudia masomo ya kidato cha pili sawa na wale wa kidato cha tano.

Kuhusu tatizo la walimu wa sayansi na hisabati kwa skuli za sekondari, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kimeanzisha darasa la kidato cha tano kwa masomo ya sayansi ili wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita wajiunge na ualimu kwa ngazi ya shahada ya kwanza.

Aidha waziri wa wizara hiyo Ali Juma Shamuhuna alisema Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia, ina mpango wa kuanzisha kozi maalum kwa ajili ya kuwashajiisha vijana kupenda masomo ya sayansi.

Waziri huyo alisema wizara imejipanga kuendelea kujenga vyumba vya maabara na kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara kwa skuli za sekondari na msingi, hiyo ni kutokana na skuli nyingi hushindwa kufanya mazoezi ya vitendo kutokana na kutokuwa na maabara na vifaa vya kutosha.

Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa unakusudia kuimarisha vyuo vya Kiislamu nchini, Mradi ambao utaendelea na ujenzi na ukarabati wa Chuo cha Kiislamu, Kiuyu, Pemba.

Wizara hiyo ilieleza kuwa, kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013, inakusudia kuendeleza na utekelezaji wa MKUZA II na utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu (ZEDP) na Sera ya Elimu ya mwaka 2006 ambapo Wizara itahakikisha kuwa malengo ya Milenia na Elimu kwa wote yanafikiwa ifikapo mwaka 2015.

Kwa upande wake Dk. Shein alisema wakati umefika kwa wizara hiyo kuongeza juhudi katika masomo ya sayansi ili waweze kupatikana wataalamu watakaosaidia maendeleo ya nchi.

Dk. Shein aliutaka uongozi huo wa wizara ya Elimu kuwahamasisha zaidi kusoma masomo ya sayansi watoto pamoja na kuwahimiza wazee kuwashajiisha watoto wao kuyapenda masomo ya sayansi.

Dk. Shein aliagiza kuwekwa mazingira ya daghalia za hapa ili ziweze kutoa huduma kwa wanafunzi kama ilivyokuwa siku za nyuma na kuweza kusoma kwa ufanisi zaidi.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.