Habari za Punde

Vitambulisho Vipya vya JAB Vyarejesha Heshima ya Taaluma ya Habari


Na Mwandishi Wetu, JAB

Vitambulisho vipya vya kidijitali vinavyoendelea kutolewa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) vimepokelewa kwa furaha na matumaini makubwa na waandishi wa habari nchini. Hatua hii imeelezwa kuwa ni mwanzo wa mwelekeo mpya wa tasnia ya habari nchini Tanzania.

Waandishi wengi wa habari wamepongeza hatua hiyo, wakieleza kuwa utoaji wa vitambulisho hivyo unarejesha heshima ya taaluma na kuongeza thamani ya elimu pamoja na juhudi walizowekeza ili kufikia viwango vya elimu vinavyohitajika kisheria.
Mhariri wa Gazeti Mwananchi Lilian Timbuka amesema kuwa hatua hiyo inaleta matumaini mapya katika tasnia ya habari.

“Tunayo matumaini kwamba sasa tasnia yetu itaonekana kwa jicho jipya. Heshima itakuwepo, maslahi yataongezeka, na jamii itaona thamani ya kazi tunayoifanya,” amesema Lilian.

Amefafanua kuwa kwa miaka ya nyuma, kazi ya uandishi wa habari ilizoeleka kufanywa na watu waliokuwa wamemaliza elimu ya sekondari bila ufaulu mzuri, au wale wenye vipaji vya kuzungumza na kupanga maneno, bila kujali vigezo vya kitaaluma.

Hata hivyo, ujio wa Bodi ya Ithibati umeweka mwelekeo mpya ambapo mtu atakayefanya kazi za kihabari na utangazaji ni yule mwenye kiwango cha elimu kisichopungua Stashahada (Diploma) katika fani ya Uandishi wa Habari au Mawasiliano kwa Umma.
Absalom Kibanda ni miongoni mwa waandishi wa habari wakongwe wanaounga mkono matakwa ya kisheria yanayomtaka mwandishi wa habari kuwa na kiwango cha elimu kisichopungua Stashahada (Diploma), ili kuipa taaluma hiyo heshima na hadhi inayostahili.

Wakili Patrick Kipangula, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Wanahabari (JAB), amesema kuwa wakati Sheria ya Huduma za Habari ilipotungwa mwaka 2016, Waziri mwenye dhamana alitoa kipindi cha mpito cha miaka mitano kwa wale waliokuwa na elimu chini ya Stashahada, au ambao hawakuwa na elimu rasmi ya uandishi, kurudi shuleni na kusomea taaluma hiyo.

Baada ya kipindi hicho, mwaka mmoja wa ziada uliongezwa ili kutoa fursa zaidi kwa wahusika kukamilisha masomo yao na sasa ni miaka mitatu zaidi ikifanya jumla ya miaka 9.

“Katika kipindi hicho, wapo waliotumia nafasi hiyo vizuri, kuna walioanzia ngazi ya cheti (Astashahada) wakaendelea hadi Stashahada, wengine wakaenda hadi Shahada na hata ngazi ya Shahada ya Uzamivu.
Hata hivyo, wapo ambao walibaki wakitazama wenzao wakijiendeleza na sasa utekelezaji wa sheria unapoanza rasmi, wameanza kulalamika na kuomba huruma. Ni wakati muafaka kwao kurudi vyuoni, kipaji pekee hakitoshi,” amesema Kipangula.

Furaha hii imeonekana pia miongoni mwa waandishi wenye Shahada za Uzamili (PhD), wakiwemo Dkt. Cosmas Mwaisobwa na Dkt. Ayubu Chacha Rioba, waliothibitisha kuwa vitambulisho hivyo vinatambua hadhi yao ya kitaaluma.

Dkt. Mwaisobwa alisema, "Hatukutarajia kama kuna siku vitambulisho vyetu vitasomeka 'Dkt', hii ni heshima kubwa kwetu kwa sababu safari ya kufikia ngazi ya Uzamivu haikuwa rahisi. Tumeisotea sana PhD, sasa kuona cheo hiki kikiwa sehemu ya utambulisho wetu rasmi ni faraja isiyo na kifani."

Bodi ya Ithibati ni nini na Majukumu yake ni yapi?

Bodi ya Ithibati ni chombo cha kitaaluma kilichoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, kifungu cha 11, ili kukuza taaluma ya uandishi wa habari nchini.
Waziri mwenye dhamana ya habari ndiye aliyepewa mamlaka ya kuteua wajumbe wa bodi hii, na hadi sasa wajumbe sita kutoka taasisi za habari, vyama vya kihabari, taasisi za elimu na za serikali wameteuliwa.

Majukumu makuu ya Bodi ya Ithibati ni, kuthibitisha na kutoa vitambulisho kwa waandishi wa habari kwa mujibu wa Sheria hii, kusimamia uzingatiaji wa maadili ya taaluma ya Waandishi wa Habari, kuzingatia viwango vya kitaaluma na kukuza maadili mazuri na viwango miongoni mwa waandishi wa habari;

Majukumu mengine ni kuishauri Serikali katika masuala yanayohusu elimu na mafunzo kwa waandishi wa Habari, kwa kushauriana na taasisi nyingine zinazohusiana na masuala ya habari, kuweka viwango vya taaluma na mafunzo kwa waandishi wa Habari, kuanzisha ushirikiano na taasisi zingine za aina hiyo ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano.

Pia, Bodi ina jukumu la kushauriana na Baraza na kuandaa mafunzo kwa waandishi wa Habari pamoja na kutunza orodha ya waandishi wa habari waliothibitishwa.

Hadi kufikia Oktoba 2025, Bodi imetekeleza jukumu moja la kuthibitisha na kutoa vitambulisho vya uandishi wa Habari maarufu Press Card kwa Waandishi zaidi ya 3,720 huku ikiendelea kuthibitisha wanaoendelea kujisajili.

Faida za ithibati kwa waandishi wa habari ni pamoja na;Kwanza ni kuwa na Utambulisho wa Kitaaluma, mwandishi anayetambulika kisheria ana uhalali wa kufanya kazi za kihabari kwa uhuru na kupewa heshima yake.

Pili, Ulinzi na Haki, kitambulisho kinampa mwandishi ruhusa ya kuingia katika maeneo maalum na kumwezesha kutekeleza majukumu yake bila kizuizi na kimtambulisha kwa mamlaka mbalimbali kumpa mwandishi msaada anapokutana na changamoto kazini.

Bodi haijaundwa kwa lengo la kuminya uhuru wa habari. Wakili Patrick Kipangula, Kaimu Mkuu wa Bodi, anasema:"

Bodi haijaundwa kuumiza uhuru wa habari, bali ni kusaidia sekta kuwa rasmi, kuipa heshima na kuongeza umuhimu wa kusimamia maadili na weledi. Uhuru wa waandishi wa habari unahakikishwa na Sheria ya Huduma za Habari."

Vitambulisho vya Uandishi wa Habari, vinatoa nafasi sawa kwa waandishi wenye ulemavu au waandishi chipukizi kuonekana na kuthaminiwa.

Seif Nindilo, mwandishi mwenye ulemavu wa macho, alipokabidhiwa kitambulisho chake alisema, "Ninachohitaji si huruma, bali ni kutambuliwa kama mwandishi wa habari mwenye ithibati, ninayeweza kutekeleza majukumu yangu sawasawa na wengine. Vitambulisho vya JAB vinafungua milango ya usawa na jumuishi."
Kwa upande wake Sista Paulina Mshana, mwandishi chipukizi mkoani Tanga, aliongeza, "Kadi ya JAB imenijengea kujiamini. Sasa naweza kusimama kwa ujasiri nikiwa na sauti inayosikika sawasawa na wengine. Hii inaonyesha uandishi wa habari ni wito unaoweza kushirikiana na miito mingine ya kijamii na kidini, mradi tu mwandishi awe na ithibati."

Ili kupata Kitambulisho kupitia Mfumo wa kidijitali Mwandishi wa Habari anatakiwa kujaza taarifa zake wakati wa kujisajili na kisha kupakia nakala ya vyeti vya kitaaluma, barua ya mwajiri au udhamini wa chombo cha habari, picha ndogo na nyaraka nyingine zinazohitajika.
Baada ya kukamilisha maombi Mwandishi atalipia malipo ya TSh 50,000 kwa kitambulisho kilicho na muda wa matumizi wa miaka miwili kwa wale wa Kitaaluma na 20,000 kwa wanafunzi wa mafunzo kwa vitendo kama ilivyoainishwa katika Sheria na Kanuni.

Kila mwandishi anayepata ithibati anathibitisha kuwa ana ujuzi, weledi, na sifa stahiki za taaluma, tofauti na wale wanaofanya kazi bila ithibati.Ithibati, Nguzo ya Heshima na Uaminifu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.