Habari za Punde

MNEC - AMIN SALMIN : AONGOZA OPERESHENI AMKA NUNGWI KUMEKUCHA.

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa(MNEC) Amini Salmin Amour,akiongoza operesheni ya “Amka Nungwi kumekucha” ya kupandisha bendera za CCM katika Shehia za Kilindi,Kigunda na Tazari katika Jimbo la Nungwi akiwa pamoja na Wagombea wa nafasi ya Ubunge na Uwakilishi wa Jimbo hilo.

Na Mwandishi Wetu,Zanzibar.

WANANCHI wa Jimbo la Nungwi Shehia za Kilindi,Tazari na Kigunda wameshauriwa kutumia vizuri haki ya kidemokrasia katika Uchaguzi Mkuu wa Dola Oktoba 29,mwaka huu kuwachagua viongozi bora wanaotokana na CCM ili walete maendeleo katika nyanja za kijamii na kiuchumi.

 

Ushauri huo umetolewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa(MNEC) Amini Salmin Amour wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo hilo katika operesheni ya “Amka Nungwi Kumekucha” ya kuhamasisha na kupandisha bendera za CCM katika mashina mbalimbali ya Jimbo hilo.

 

Alisema wananchi wa jimbo hilo wakifanya maamuzi ya kuwachagua viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya Urais wa Jamhuri kumchagua Dkt.Samia Suluhu Hassan,Urais wa Zanzibar kumchagua Dk.Hussein Mwinyi pamoja na Mbunge,Mwakilishi na Madiwani wa CCM watakuwa wameliweka jimbo katika mazingira salama ya kimaendeleo.

 

Katika maelelezo yake (MNEC) Amini,amesema chama cha mapinduzi kupitia viongozi wake endapo kitapata ushindi na kuendelea kuongoza dola katika miaka mitano ijayo kimedhamiria kumaliza changamoto za upungufu wa maji safi na salama na upungufu wa ajira kwa vijana wa jimbo hilo.

 

Alisema kupitia Ilani ya CCM ya mwaka 2025/2030 imeazimia kuhakikisha wananchi hasa vijana wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wananufaika na sekta ya utalii na uvuvi ambayo ndio chimbuko la ajira kwa wananchi wa jimbo hilo.

 

"Chama Cha Mapinduzi katika miaka mitano iliyopita kimetekeleza kwa vitendo ahadi zake nyote ni mashahidi namna Serikali ilivyotekeleza miradi ya maendeleo,hivyo tupeni tena miaka mitano tuwaletee maendeleo endelevu katika sekta za elimu,afya,miundombinu ya barabara na kuongeza fursa za ajira kupitia uchumi wa buluu."alisema Amini.

 

Amini,alieleza kuwa CCM kwa sasa inaendeleza malengo yake ya kufanya mapinduzi ya kiuchumi ili kuhakikisha maisha ya wananchi wa jimbo hilo yaendelea kuimarika.

 

Pamoja na hayo amewasisitiza wananchi hao kuwapuuza na kuwakataa baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaohamasisha vurugu na chuki kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

 

Naye Mgombea Ubunge katika jimbo hilo  Mdowe Haji Kombo,amewaomba wananchi hao kumchagua kuwa mbunge ili akawawakishe katika bunge kwa kujenga hoja zitakazoleta matokeo chanya ya kimaendeleo.

 

Kwa upande wake Mgombea Uwakilishi katika Jimbo hilo Salum Soud Hamed,amesema jimbo hilo linahitaji viongozi wenye uzalendo,uaminifu,uchapakazi na wenye nia ya dhati ya kuwatumikia wananchi bila ubaguzi wa kisiasa,kidini na kikabila wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi.

" Nimeomba nafasi hii ya Uwakilishi sio tu kuwa kiongozi bali ni kuwa mtumishi wa kuleta mageuzi ya kimaendeleo,changamoto zote nazijua na endapo mtatupa ridhaa ya kuongoza tutazitafutia ufumbuzi wa kudumu'"alisema.

 

Naye Mkaazi wa Shehia ya Kendwa Farid Issa Mohamed,amewasihi wananchi kujitokeza kupiga kura ili wapate viongozi watakowawakilisha katika vyombo vya maamuzi.

 

Farid,alieleza kuwa maendeleo ya Zanzibar yataendelea kuimarika endapo wananchi watalinda amani na utulivu wa nchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.